Na NASRA KITANA
BAADA ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya St. George ya Ethiopia, Kocha Msaidizi wa Yanga, Simo Dladla amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa ‘dabi’ dhidi ya Simba.
Yanga ilicheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya St George uliopigwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam ambapo ilishinda kwa bao 1-0 katika kipindi hiki ambacho Ligi imesimama kupisha mechi za timu ya taifa.
Baada ya mapumziko hayo, Yanga itakuwa na kibarua cha mechi ngumu dhidi ya wapinzani wao Simba mchezo utakaochezwa Jumamosi, Oktoba 10, 2026, kuanzia saa 1:00 usiku Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Simo alisema baada ya mapunziko hayo wanajua wana mchezo mgumu dhidi ya SImba na wapo tayari.
“Niseme tu kuwa kama klabu tupo tayari kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Simba na tuna imani tunaenda kufanya vizuri na kupata ushindi katika mchezo huo muhimu,” alisema.
Simo alifafanua kuwa wataendelea kucheza mechi nyingi za kirafiki kwani lengo lao kubwa ni kuhakikisha wanakuwa na kikosi bora na chenye ushindani.
Simo alisema anajivunia kikosi cha Yanga kwa vile kimejaa wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kupata matokeo mazuri.
Pia, alisema katika kipindi hiki cha mapumziko ya Ligi, wamepanga kurekebisha kasoro zote zilizojitokeza katika mechi zilizopita zikiwemo za Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara.
MANQOBA ATIMKIA AFRIKA KUSINI
Kocha Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi ameondoka nchini kwenda Afrika Kusini kwa mapumziko mafupi, wakati kikosi chake nacho kikipewa nafasi ya kupumzika kabla ya kurejea kambini kuanza maandalizi ya mechi inayofuata dhidi ya Simba.
Taarifa kutoka Yanga zilisema Manqoba ameondoka kwa ajili ya mapumziko ya siku chache na wachezaji nao watapewa mapumziko mafupi.
Kocha huyo aliyetua Jangwani msimu huu akitokea Golden Arrows, amekuwa na mwanzo mzuri baada ya kuiongoza Yanga kushinda mechi zote sita ilizocheza katika Ligi Kuu Bara mwezi Agosti na kuchaguliwa kuwa Kocha Bora wa Mwezi huo.
Pia, Yanga iliendelea na mwendo huo mwezi huu, baada ya kuichapa Geita Gold bao 1-0 katika mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa KMC Complex, ushindi ambao uliwaweka mabingwa hao katika nafasi nzuri.
Mapumziko hayo yanakuja katika kipindi ambacho ratiba ya ligi imepisha majukumu ya timu za Taifa, huku Yanga ikiwa na wachezaji 11 walioitwa kwa ajili ya programu ya kimataifa.
Hivyo, Manqoba atakapokuwa Sauzi, baadhi ya wachezaji wake watakuwa kwenye majukumu ya timu zao za taifa kutoka kwenye mataifa mbalimbali.
YANGA YATOZWA FAINI YA MILION TANO
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeitoza faini ya Sh milioni tano klabu ya Yanga baada ya mashabiki wake kutenda kosa la kuwarushia chupa benchi la ufundi la Geita Gold katika mchezo uliomalizika kwa Yanga kushinda 1-0.
Mbali na faini hiyo, Yanga imepewa onyo kali kwa kutofuata mtiririko wa matukio ya mchezo (Match Countdown), ambapo wachezaji watatu waliingia uwanjani kwa ajili ya kupasha misuli joto saa 12:00 jioni badala ya saa 12:10 jioni kama ilivyopangwa.
Aidha, Ofisa Ulinzi na Usalama wa Yanga, Eddie Evance, amepelekwa Kamati ya Maadili ya TFF kwa kosa la kukaidi maamuzi ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, Evance alionekana uwanjani wakati wa mchezo huo licha ya kuwa anatumikia adhabu ya kutoruhusiwa kuingia uwanjani kwa kipindi cha miezi sita, adhabu iliyotolewa Juni 8, mwaka huu.




