Na ATHNATH MKIRAMWENI
UFAULU wa Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) mwaka 2026, umeongezeka hadi kufikia asilimia 85.22 kutoka asilimia 81.80 mwaka jana huku watahiniwa 970,876, wakipata ufaulu mzuri.
Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Profesa Said Mohamed, alisema ufaulu huo, umeongezeka kwa asilimia 3.42, ikilinganishwa na mwaka jana.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, jumla ya watahiniwa 1,168,718, walisajiliwa kufanya mtihani huo uliofanyika Septemba mwaka huu.
Kati ya hao, wasichana walikuwa 637,214 ambao sawa na asilimia 54.52 na wavulana 531,504 sawa na asilimia 45.48.
Kati ya watahiniwa waliosajiliwa 1,139,318 sawa na asilimia 97.48 walifanya mtihani, wakiwemo wasichana 624,976 na wavulana 514,342. Watahiniwa 29,400 ambao ni asilimia 2.52, hawakufanya mtihani.
Katika matokeo hayo, wavulana wameongoza kwa ufaulu kwa asilimia 86.18 sawa na watahiniwa 443,254 huku wasichana wakipata asilimia 84.43 sawa na watahiniwa 527,622.
Hata hivyo, ufaulu wa wasichana, umeongezeka kwa asilimia 3.22 kutoka asilimia 81.21 mwaka 2025, wakati wavulana umeongezeka kwa asilimia 3.67 kutoka asilimia 82.51.
UBORA WA UFAULU
Katika ubora wa ufaulu, Profesa Mohamed, alisema watahiniwa 429,667 sawa na asilimia 37.72, wamepata madaraja ya A na B, sawa na ongezeko la asilimia 0.82, ikilinganishwa na mwaka jana.
Kwa upande wa shule, kati 20,010 zilizofanya mtihani huo, 12,914 sawa na asilimia 64.54, zimepata wastani wa daraja C na shule 5,670 sawa na asilimia 28.33, zimepata wastani wa madaraja A na B.
Shule zilizopata wastani wa madaraja A hadi C, zimeongezeka hadi 18,584 sawa na asilimia 92.87 mwaka 2026, ikilinganishwa na shule 17,727 mwaka 2025.
Katika masomo ya lugha, Kiswahili kimeongoza kwa ufaulu wa asilimia 93.13, ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.56 ikilinganishwa na mwaka jana, wakati somo la kingereza likipata asilimia 50.
Kwa kuzingatia ubora wa ufaulu, Kiswahili kimeonesha ongezeko la watahiniwa waliopata madaraja A na B hadi asilimia 73.81 kutoka asilimia 59.65 mwaka 2025, huku lugha ya kingereza ikifikia asilimia 22.56 kutoka asilimia 20.95.
MASOMO MENGINE
Katika masomo ya sayansi jamii, Uraia na Maadili, yamekuwa na ufaulu wa asilimia 90.12, huku Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi, ikifikia asilimia 76.53, sawa na ongezeko la asilimia 6.24 ikilinganishwa na mwaka jana.
Somo la Hisabati nalo limeonesha kuongezeka kwa ufaulu hadi asilimia 62.56 kutoka asilimia 56.66 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 5.90.
Hata hivyo, somo la Sayansi na Teknolojia, limeonesha kushuka ufaulu hadi asilimia 80.34 kutoka asilimia 84.43 mwaka 2025, sawa na upungufu wa asilimia 4.09.
MATOKEO YALIYOZUIWA NA KUFUTWA
Katika hatua nyingine, NECTA imezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 371 waliougua na kushindwa kufanya mtihani kwa idadi kubwa ya masomo au masomo yote, huku wakipewa fursa ya kurudia mtihani huo mwakani.
NECTA pia, imefuta matokeo yote ya watahiniwa 26 waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani na wengine watano walioandika lugha ya matusi katika maandishi yao ya majibu.
Profesa Mohamed, alieleza kuwa matokeo ya mwaka huu, yatatolewa bila majina ya watahiniwa kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Ulinzi wa Taarifa Binafsi, namba za mtihani zitatumika kuwatambua watahiniwa.
Profesa Mohamed, alisema matokeo hayo yanapatikana kupitia tovuti za www.necta.go.tz, www.moe.go.tz na www.tamisemi.go.tz, huku Baraza likiyawasilisha kwa mamlaka zinazohusika kwa uchaguzi wa watahiniwa watakaojiunga na elimu ya sekondari.




