Na MWANDISHI WETU
MWENYEKITI wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Kiomoni Kibamba amesema wanasubiri Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu aitishe Mkutano Mkuu na kutoa ratiba ya uchaguzi ili kuanza rasmi mchakato huo.
TFF, inatarajia kusimamia uchaguzi wa viongozi wa klabu ya Simba utakaofanyika Januari, mwakani.
TFF imeamua kuusimamia uchaguzi huo kwani ina mamlalaka kisheria baada ya kuona kuna baadhi ya dosari zilizojitokeza ndani ya uongozi wa klabu hiyo.
Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kibamba alisema hivi sasa wanasubiri Mangungu aitishe mkutano wa Simba ikiwemo kutoa ratiba ya uchaguzi na mchakato utakavyoanza rasmi.
Alisisitiza baada ya kutoka ratiba ya uchaguzi, wanachama watajua utaratibu wa kuchukua na kurudisha fomu kwa wajumbe watakaowania nafasi mbalimbali.
“Hivi sasa bado hakuna kinachoendelea, hivyo tunasubiri Mwenyekiti Mangungu aitishe tarehe ya mkutano wa klabu baadaye ratiba ya uchaguzi ambapo mchakato mzima ndipo utaanza kulingana na ratiba itakayotolewa.
“Wanachama wanatakiwa kujua kwamba lini wanatakiwa kuanza kuchukua fomu na kurudisha ukiwemo mchakato mzima wa ratiba husika,” alisema.
Awali, Mangungu alisema hakuna haja ya kutishana kwani wao wanatambua kwamba Simba ipo moja.
Alisema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakizungumzia kwamba kuna mpasuko na viongozi kugawanyika pande tofauti, lakini wao wanatambua Simba ipo moja.
“Sisi tunatambua Simba ni moja, mtu anaweza kusema chochote, hivi sasa jambo la uchaguzi lipo chini ya TFF.
“Mimi mwenye mamlaka ya mkutano, muda utakapofika nitaitisha mkutano kwa mujibu wa utaratibu, sisi hatuna hitilafu na mambo yanakwenda vizuri,” alisema Mangungu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori, alisema hakuna mpasuko, licha ya kuwepo kwa maoni tofauti kuhusu uchaguzi na uendeshaji.
Magori alisema Simba ni klabu ya wanachama na wawekezaji, hivyo tofauti za kimtazamo ni sehemu ya demokrasia na hazipaswi kutafsiriwa kuwa ni mgawanyiko.
“Ndani ya klabu yetu hakuna mpasuko wowote ule bali ni tofauti za maoni zinazohusu uchaguzi na kwa hivi sasa kila kitu kinakwenda sawa kuhakikisha klabu yetu inafikia malengo tuliojiwekea msimu huu,” alisema Magori.
Hata hivyo, Magori alisema yeye hana mpango wa kugombea nafasi yoyote katika uchaguzi huo.
“Nasema yeyoyote mwenye uwezo wa kugombea anaruhusiwa kufanya hivyo kwa mujibu wa kanuni,”alisema.
Mfadhili wa zamani wa Simba, Azim Dewji alisema anaishukuru TFF kwa kutumia ustaarabu na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa maslahi ya klabu.
Hata hivyo, Dewji alisema uchaguzi hauwezi kuleta athari kwa matokeo ya timu, hivyo anaamini watapata viongozi wapya watakaoendeleza mafanikio ya Simba.
“Ninaishukuru TFF kwa kutambua ukubwa wa klabu ya Simba na kuingilia kati uchaguzi kwa maslahi mapana ya klabu, tunaamini tutapata viongozi wapya watakaoendeleza mazuri yaliyofanywa na viongozi wanaomaliza muda wao,” alisema Dewji.
DANADANA
Awali, Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, ilitangaza mkutano mkuu na uchaguzi wa viongozi wapya.
Mkutano huo, umepangwa kufanyika Januari 3, mwakani lakini baadaye Mangungu aliibuka na kusisitiza kamati iliyotoa taarifa hiyo ilikuwa batili.
Mangungu alisema hakuna haja ya kutishana kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakifanya hivyo.
Kutokana na mvutano kati ya pande mbili, TFF iliingilia kati na kusema itasimamia yenyewe uchaguzi huo kwa mujibu wa sheria na katiba ambapo ni lazima ufanyike kabla ya Januari 29, mwakani.
Mara ya mwisho uchaguzi wa Simba ulifanyika Januari 29, mwaka 2023 ambapo muda wao wa miaka minne kukaa madarakani upo ukingoni kumalizika.




