Na IRENE MWASOMOLA
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Asha Rose Migiro, amewataka wanachama na viongozi wa chama hicho kushiriki kikamilifu katika vikao vya mashina katika maeneo yao, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kukiimarisha chama na kudumisha misingi yake ya itikadi.
Aidha, amewataka Makatibu wa Itikadi na Uenezi kushirikiana kwa karibu na viongozi wa mashina katika kuendesha madarasa ya itikadi, akieleza kuwa mashina ndiyo darasa la kwanza la itikadi ambapo wanachama hujifunza misingi ya Chama Cha Mapinduzi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, katika mwendelezo wa ziara yake ya kuzungumza na Mabalozi wa Mashina na wanachama wa CCM wa Wilaya za Kinondoni na Ubungo, Balozi Dk. Migiro amesema uhai wa CCM unatokana moja kwa moja na uhai wa mashina.
Amesema kupitia vikao vya mashina, chama hupata fursa ya kujitathmini uwezo wake wa kiutendaji na kuimarisha mshikamano wa wanachama.
“Lazima tuhakikishe tunafanya vikao. Ni wajibu wa kila mwana CCM, hususan viongozi, kushiriki kikamilifu katika vikao hivyo. Kupitia vikao hivi tutabadilishana uzoefu na kupata taarifa sahihi zitakazokisaidia kukisukuma Chama Cha Mapinduzi katika ngazi zinazofuata,” alisema.
Ameongeza kuwa mashina ndiyo msingi wa kujenga kizazi chenye uelewa wa itikadi, historia ya CCM na historia ya Taifa kwa ujumla.
“Mashina ndiyo darasa la kwanza la itikadi. Kupitia mashina haya, kizazi kitaelewa historia ya Chama Cha Mapinduzi, historia ya nchi yetu na maana halisi ya kuwa mwanachama wa CCM,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Balozi Dk. Migiro aliwataka viongozi wa CCM katika ngazi zote kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji, akieleza kuwa ndiyo nguzo muhimu katika kuimarisha imani ya wanachama na wananchi kwa chama.
Balozi Dk.Migiro ameongeza kuwa, kuimarika na kudumu kwa CCM ndio mustakabali wa serikali.
Pia, amewataka viongozi wa mashina kuhakikisha wanasimamia vizuri kauli mbiu ya kazi na utu kwa kujenga utu na jamii.
“Sisi kama wana CCM tuna dhima kubwa ya kusimamia kauli mbiu yetu katika kuisimamia vyema serikali.”alisema
Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Stanley Mkandawire, alisema baada ya kukamilika kwa ziara ya Katibu Mkuu mkoani humo wamejipanga kwenda kuhuisha mashina.
Pia alimpongeza na kumshukuru Rais Dk. Samia kwa kutoa fedha nyingi za maendeleo katika Mkoa wa Dar es Salaam na kwamba CCM mkoani humo itaendelea kufuatilia kwa karibu.
Kwaupande wake Kaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) Juma Simba Gadaffy, alimpongeza Balozi Dk. Migiro kwa kuona haja ya kuimarisha CCM kuanzia ngazi ya mashina.
Akizungumza kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule, alisema mkoa huo utahakikisha miradi yote inayotekelezwa inakamilika kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Alitaja baadhi ya miradi inayotekelezwa ni ujenzi wa barabara za mwendokasi, madaraja na miundombinu mingine.
Alisema mkoa huo unajivunia kazi kubwa zinazofanywa na Mwenyekiti Rais Dk. Samia, nakwamba watahakikisha miradi yote inayotekelezwa ina kamilika kwa wakati na ubora.
Naye Mbunge wa Jimbo la Ubungo Profesa Kitila Mkumbo, akizungumza kwaniaba ya Wabunge wa Wilaya za Ubungo na Kinondoni, alisema tayari utekelezaji wa Ilani katika majimbo ya wilaya hizo unaendelea kwa kuzingatia vipaumbele.
Alisema Ilani ya CCM imeshawekwa katika mpango wa maendeleo ya taifa, tayari kwa utekelezaji.
Wajumbe Mashina
Kwaupande wake Mjumbe wa Shina namba moja Mtaa wa Mbezi Kati Wilayani Kinondoni Obedi Ndapisa, aliomba chama kuona haja ya kupitia upya idadi ya nyumba wanazo ongoza na kwamba zipungue kutoka 100 angalau ziwe 20.
Naye Mjumbe wa Shina namba tano tawi la Mzimuni Rosemary Kambena, aliomba chama kuona namna ya kuwapa semina za mara kwa mara mabalozi wa shina, ili kuongeza ufanisi katika utendaji wao.
Mjumbe wa Shina namba mbili Kibamba Hospitali Norbelt Mbena, aliomba chama kuwapatia wajumbe wa mashina vitambulisho maalumu vitakavyo watambulisha na kuwasaidia kupata huduma mbalimbali serikalini.




