Na HANIFA RAMADHANI, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema katika kipindi cha miaka 62 ya Mapinduzi, Zanzibar imeendelea kupata mafanikio makubwa.
Amesema Zanzibar, imeweka rekodi mpya kwa mara ya kwanza, kuwa na barabara ya juu (Flyover).
Rais Mwinyi, aliyasema hayo, katika hafla ya uzinduzi wa ‘flyover’ namba 1 iitwayo Hussein Ali Hassan Mwinyi Mwanakwerekwe, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi.
Alisema hatua hiyo, ni ushahidi wa dhamira ya serikali ya kujenga miundombinu ya kisasa inayokidhi mahitaji ya wananchi hivi sasa na baadaye.
Alieleza kuwa, barabara hiyo, ni mradi wa kimkakati unaolenga kupunguza msongamano wa magari katika eneo hilo, kuongeza usalama wa watumiaji na kurahisisha usafiri wa watu na usafirishaji mizigo.
Alisema ‘flyover’ hiyo ni matokeo ya uwekezaji mkubwa wa serikali katika sekta ya miundombinu kwa kuwa, barabara ya kiwango bora ni nguzo muhimu ya kukuza uchumi, kuvutia wawekezaji na kuchochea shughuli za kibiashara.
“Slogan (kaulimbiu) yetu ya uchaguzi ni ‘uongozi unaoacha alama na leo (jana), tumeitekeleza kwa vitendo dhamira hiyo, hizi ndizo alama tunazozungumza,” alisema.
Alifafanua zaidi kuwa, serikali itaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa lengo la kuimarisha ustawi wa wananchi na kuinua uchumi wa Zanzibar.
NENO LAKE KWA WANANCHI
Rais Mwinyi aliwasihi wananchi, kuitunza na kuitumia ipasavyo miundombinu hiyo idumu muda mrefu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Hata hivyo, aliwataka wananchi kuwa tayari kupisha miradi ya maendeleo, akaahidi serikali italipa fidia stahiki.
Akaeleza kuwa, mtu anayekaidi kupisha ujenzi wa miundombinu, hana dhamira njema kwa sababu maendeleo yanayofanyika yanawanufaisha watu wote.
“Kwa yule ambae bado ana mashaka, namtoa hofu kuwa, serikali itatoa fedha stahiki na hatutomdhulumu yeyote, kila mtu atapata haki yake, tupeni nafasi ya kuleta miradi ya maendeleo na msiwe kikwazo,” alithibitisha.
ATAHADHARISHA
Aliwasisitiza wananchi kucha kujenga katika hifadhi ya barabara, kwani serikali inakusudia kupitisha huduma za maji, umeme na mawasiliano.
Alipongeza wizara husika kwa kazi kubwa ya ujenzi wa barabara waliyofanya katika maeneo ya mijini na vijijini, visiwani Unguja na Pemba.
Pia, aliipongeza Kampuni ya CCECC kwa kazi nzuri wanayofanya ya ujenzi wa barabara zenye viwango.
WAZIRI WA UJENZI
Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Mohammed, alimpongeza Rais Mwinyi kutokana na kazi kubwa anayoifanya kwa kusema kama kuna mtu haoni, basin i mpinga maendeleo.
Alisema mafanikio yanayoenekana ni maono na busara za Rais Dk. Mwinyi katika kuteleleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi na ahadi zake, alizozitoa kwa wananchi mwaka 2020, mojawapo ilikuwa kufumua mfumo mzima wa barabara mjini na vijijini na kujengwa kwa kiwango cha lami na ubora wa hali ya juu Unguja na Pemba.
Khalid alisema Rais Mwinyi aliahidi ‘flyover’ mbili kwa lengo la kuondosha msongamano, ametekeleza kwa kukamilisha moja ambayo inafanya Zanzibar kuweka rekodi mpya.
RC MJINI MAGHARIBI
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mohammed Ali Abdallah, alisema Zanzibar imeweka rekodi nyingine ya Mapinduzi yaliyoasisiwa na Mzee Karume, kwani nchi inashuhudia maendeleo kupitia sekta mbalimbali.
KATIBU MKUU WA WIZARA
Akitoa taarifa ya kitaalamu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Mhandisi Ali Said Bakar, alisema barabara ya juu (Flyover) Mwanakwerekwe, ni ujenzi wa barabara za mjini zenye urefu wa kilometa 100.9, unajumuisha ‘flyover’ mbili ikiwemo iliyojengwa Amani.
Alisema ujenzi wa ‘flyover’ namba moja, ulianza rasmi Desemba Mosi, 2023 na kukamilika Desemba 31, 2025, umegharimu kiasi cha sh. bilioni 23.7.
Mhandisi Ali, alisema ujenzi wa ‘flyover’ hiyo, umejumuisha daraja lenye nguzo 48 zenye upana wa futi tatu, ‘zilizozikwa’ kwa kina kati mita 29 hadi 32, ujenzi wa nguzo mbili zenye upana wa mita 18 na nguzo zenye urefu wa mita 14.4, ambazo zinabeba mzigo uliopo juu ya daraja hilo.




