Na MUSSA YUSUPH
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa ahadi tano zitakazofungua uchumi wa wananchi wilayani Igunga mkoani Tabora.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa kampeni wilayani Igunga mkoani Tabora, Dk. Samia, aliwaomba wananchi kuipa ridhaa CCM kushika hatamu ya uongozi katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Dk. Samia, alisema serikali yake pindi itakapoingia madarakani, itajenga stendi ya kisasa ya mabasi katika mji huo.
Vilevile, aliahidi kujenga soko la kisasa, ambalo likikakamilika, linafungua na kuongeza wigo wa biashara na kuvutia uwekezaji.
Aliahidi kujenga kwa kiwango cha lami barabara ambazo zinapita katika maeneo ya uzalishaji wa mpunga, mbaazi, dengu, choroko na madini hatua ambayo, itachangia ukuaji uchumi.
Alisema pamoja na kazi kubwa katika kusambaza umeme katika vijiji na vitongoji na kuahidi kujenga kituo cha kupokea na kupooza umeme katika wilaya hiyo.
Dk. Samia, alisema Igunga itaanzisha kongani ya viwanda na kuongeza thamani ya mazao.
Kuhusu changamoto ya wanyamapori, alisema serikali itakuja na njia sahihi ya kudhibiti wanyamapori waharibifu ambao wamekuwa kero kwa wananchi wa vijiji vinavyopakana na hifadhi.
Pia, aliahidi kuendelea kuimarisha huduma za afya, maji na elimu hasa kutokana na kuwepo kwa uhitaji wa huduma hizo kwa wananchi.
“Ili tuyafanye haya na mengine ambayo yako katika ilani ya uchaguzi kwa Igunga ni lazima ushindi kwa CCM. Sina mashaka na Igunga kuwa tutapata ushindi.
“Tunachotaka siyo ushindi pekee, bali ushindi wa heshima tuwazibe midomo wale wengine.”
“Kumekuwa na idadi kubwa ya kuhudhuria mikutano, nawapongeza kwa hilo, sasa uwingi huu wa watu, pia ukaonekane katika sanduku la kura,” alisema.