Na NASRA KITANA
KAIMU Kocha Mkuu wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Miguel Gamondi, leo atakabiliwa na mtihani wake wa kwanza atakapoiongoza miamba hiyo katika mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Kuwait.
Taifa Stars itachuana na Kuwait saa 1:00 usiku katika mechi iliyopo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), itakayopigwa Uwanja wa Al Salam uliopo jijini Cairo, Misri.
Gamondi ataiongoza Stars kwa mara ya kwanza ikiwa siku kadhaa tangu alipopewa mikoba baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuachana na mzawa Hemed Suleiman Morocco.
Akizungumzia mechi ya leo, Gamondi amesema pamoja na timu yao kushindwa kufanya maandalizi ya kutosha, lakini ana imani watashinda katika mchezo huo.
Amesema ana imani kubwa na kikosi chake kwani kila mchezaji ametoka katika mashindano katika klabu hivyo hana hofu na viwango vyao.
Gamondi amesema anafurahi kuona kila mchezaji ana morali ya kutosha kuhakikisha wanatumia vyema kila mbinu aliyowapatia.
“Tunaingia katika mchezo huo kwa kuwaheshimu wapinzani na kucheza kwa tahadhari kubwa, lengo kuhakikisha tunapata ushindi, nina imani hilo linawezekana kutokana na ubora mkubwa tuliokuwa nao,” amesema.
Kocha huyo amesema atahakikisha anakipanga vyema kikosi chake kwa kutumia mbinu tofauti kupata matokeo ya ushindi.
Nyota wa timu hiyo, Shomari Kapombe, amesema wachezaji wamejipanga vizuri kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo.
Amesema anajua mchezo utakuwa mgumu lakini atahakikisha anapambana kupata matokeo.
Kapombe amesema wachezaji wote wana morali ya kutosha na kila mmoja ana uhitaji mchezo huo.
Naye mshambuliaji wa timu hiyo, Kelvin John, amesema huo ni mchezo muhimu kwao kujipima kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), kujua wapi walipo na wapi wanatakiwa kufanya marekebisho.
“Huu ni mchezo muhimu kwetu hasa kuelekea katika mashindano ya AFCON, mwalimu atapata nafasi ya kujua nini aongeze na kipi apunguze kwa hiyo ni mechi nzuri ya kujipa na kujua wapi tunakosea hivyo tutapambana kuonyesha ubora tuliokuwa nao,” alisema.




