• ePaper
Saturday, November 15, 2025
Subscribe
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
No Result
View All Result
Home Habari

NI MARIDHIANO

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
November 15, 2025
in Habari, Kitaifa, Siasa
0
NI MARIDHIANO

RAIS DK. SAMIA SULUHU HASSAN

0
SHARES
1
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na MUSSA YUSUPH,
Dodoma

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ametangaza msamaha kwa vijana watakaobainika kufuata mkumbo na kushiriki vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.

Amemwagiza Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuwaachia vijana hao iwapo watathibitika kutenda makosa ya uhalifu kwa kufuata mkumbo.

Pia, ametangaza kuundwa kwa tume maalumu ya kuchunguza vurugu hizo kubaini chanzo chake kwamba, matokeo ya tume hiyo, yatasaidia kufanyia kazi changamoto zitakazobainika na kuliunganisha taifa.

Aidha, amesisitiza Tanzania imejengwa kwa misingi ya haki, uhuru na mshikamano, hivyo nguvu yoyote ya kuharibu misingi hiyo, haitakubalika.

Katika hotuba yake iliyotumia saa moja na dakika 34 (sawa na dakika 94), aliyoitoa wakati akilizindua Bunge la 13, bungeni jijini Dodoma, Rais Dk. alisisitiza uadilifu, uwajibikaji na utawala wa sheria, kuhakikisha wananchi wananufaika kupitia rasilimali zilizopo, ukiwemo upatikanaji huduma na serikali yake, itakoleza moto dhidi ya vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.

Alisisitiza kuwa, tume aliyoiunda itaiongoza serikali katika mazungumzo ya kuleta amani na maelewano nchini.

“Mimi binafsi, nimehuzunishwa sana na tukio lile, natoa pole kwa familia zote zilizopoteza familia zao.

“Tunaomba waliofariki wapumzishwe kwa amani, majeruhi tunawaombea wapone haraka na waliopoteza mali zao tunawaomba wawe na ustahimilivu,” alieleza.

Dk. Samia alisema serikali imechukua hatua ya kuunda tume ya kuchunguza yaliyotokea, chanzo cha tatizo kibainike kisha taarifa ya uchunguzi itaongoza mazungumzo ya kuleta maelewano na amani.

“Kwa kuwa wananchi wa Tanzania wamenipa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi hii, sitachoka kunyoosha tena mkono wa maridhiano.

“Ni matumaini yangu, wadau wa kisiasa wataupokea kwa dhati mkono wa maelewano ili kwa pamoja, tujenge mazingira mwafaka kwa maendeleo ya taifa letu,” alieleza.

Dk. Samia, alisema katika vurugu hizo, wapo baadhi ya vijana walitumbukia katika kadhia hiyo kwa kufuata mkumbo na kushitakiwa kwa makosa ya uhaini, wakati hawakujua madhara ya kile walichokifanya.

“Kuna wakati vijana hufuata mkumbo wa uhalifu kwa ushabiki, ninatambua kwamba, vijana wengi waliokamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini, hawakujua wanachokifanya.

“Nikiwa Mama na Mlezi wa Taifa hili, ninavielekeza vyombo vya sheria na hasa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kuangalia kiwango cha makosa yaliyofanywa na vijana wetu. “Kwa wale ambao wanaonekana walifuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu, wawafutie makosa yao.

MSISITIZO KWA VIJANA

Katika hotuba yake, ambayo iliwavutia wabunge ambao mara zote waliiunga mkono kwa kugonga meza, alitoa nasaha kwa vijana, kutokubali kushikiwa akili na kushawishiwa katika kuiharibu nchi kwa sababu ya ushawishi kutoka kwa watu wasiolitakia mema taifa.

“Pamoja na kuwa uchaguzi ulifanyika, kulijitokeza vurugu za uvunjifu wa amani ambao ulisababisha uharibifu wa mali, kupoteza maisha na kuhatarisha usalama wa nchi.

“Tunapoenda mbele, niwasihi sana Watanzania, tuongozwe na dhamira ya maelewano, ushirikishwaji, kujirekebisha na umoja.

Alisisitiza: “Kwa wanangu vijana wa Taifa hili la Tanzania, niseme kwamba, nchi hii imejengwa katika misingi ya amani na utulivu wa kisiasa.

“Sisi wazazi wenu kama tungeyafanya mliyoyafanya wakati huu, nchi hii isingekuwa yenye neema na maendeleo mnayoyaona leo.”

“Hivyo, niwasihi sana wanangu vijana wa Taifa hili, nchi hii ni yenu kwa shida zozote zile zinazowakabili, msikubali hata siku moja kushawishishiwa kuichoma nchi yenu wenyewe.

“Msikubali kukata tawi la nchi mliyoikalia msikubali kabisa, hili nawaomba mlikatae kwa nguvu zenu zote, ninyi ndiyo wajenzi wa Taifa hili, nawasihi kamwe msiwe wabomoaji wa Taifa hili,” alisisitiza Dk. Samia.

Mbali na mikopo, alisema serikali itafungua fursa mahsusi kuhamasisha vijana wakiwemo wamiliki wa biashara ndogo kupata elimu ya biashara, kuweza kujisajili katika Mfumo wa Kielektroniki wa Manunuzi ya Serikali (TANSIS).

Vilevile, alieleza kuwa, kupitia vyuo vya ufundi stadi serikali itaongeza programu maalumu za mafunzo ya ufundi stadi na kuunganisha programu hizo, kupitia miradi ya mikakati kama reli ya kisasa (SGR) uendelezaji wa bandari, uchumi wa buluu, madini na gesi ili vijana wapate uzoefu waweze kuajirika.

“Serikali itaanzisha kanda za kuendeleza ujuzi zitakazowawezesha vijana kupata ujuzi unaohitajika katika kampuni ya sekta binafsi na kuangalia uwezekano wa kutoa vivutio maalum kwa kampuni zitakazotoa nafasi nyingi za ajira kwa vijana.

“Tutaweka mazingira ya kuhakikisha tunakuza vijana kwenye uongozi kwa kuwezesha vyuo vyetu kufanya mafunzo ya ulezi na ukuzaji wa vijana viongozi.

Aliongeza: “Tutaitizama mikopo ya asilimia 10 ya makusanyo ya halmashauri zetu ili kuboresha upatikanaji wa mikopo hiyo kwa walengwa.

“Vilevile, ni vyema walengwa wakajua kuwa, fedha hizi ni mkopo na siyo msaada. Ni mbegu na siyo mavuno, ni mtaji na siyo ruzuku, hivyo marejesho na tija yake lazima ionekane.”

“Matamanio yangu ni kuona ifikapo mwaka 2030, tuwe tumetengeneza wawekezaji vijana ambao watatoa ajira kwa vijana wenzao.

“Kwa kushirikiana na sekta binafsi, wadau wa maendeleo tutahamasisha ufadhili kwa biashara za wanawake kuwasaidia wanawake wanaofanya kazi katika masoko, tutaongeza na kuratibu mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kurasimisha biashara zao na kuwawezesha kukopesheka.” alieleza.

WIZARA MAALUMU YA VIJANA KUUNDWA

Katika kuonesha kujali mahitaji ya vijana, Dk. Samia, alisema serikali yake, imedhamiria kuanzisha wizara maalumu itakayokuwa ikishughulikia masuala ya vijana pamoja na kuwepo Washauri wa Rais watakaomshauri kuhusu mambo ya vijana zikiwemo changamoto zao.

Alisema zaidi ya asilimia 60 ya watu nchini ni vijana, serikali yake, itaweka kipaumbele katika sera na programu zitakazopanua fursa za kiuchumi, kutengeneza kazi, ajira, kuongeza wigo wa hifadhi za jamii na kuwajengea kesho iliyo bora zaidi.

 Ili kuhakikisha vijana wanapata nafasi ya kushiriki katika kujenga mustakabali mwema wa Taifa, alisema serikali itaweka kipaumbele katika ushirikishwaji wa vijana kwenye masuala ya maendeleo.

“Natambua kumekuwa na majukwaa mengi ya kuwafikia vijana ila bado shughuli zao zinafifishwa na masuala ya kisiasa na majukwaa hayo kupoteza malengo na mvuto kwa vijana.  

“Mimi na wenzangu katika serikali tumefikiria kuwa na wizara kamili itakayoshughulikia mambo ya vijana.

“Tumeamua kuwa na wizara kamili, badala ya kuwa na idara iliyo na mambo mengi. Vilevile nafikiria kuwa na washauri wa mausala ya vijana ndani ya Ofisi ya Rais,” alisisitiza.

Pia, alisema suala lingine lililopangwa kutekelezwa ndani ya siku 100 za awali za kazi ni kuchukua hatua za kuongeza mitaji wa shughuli za kiuchumi za vijana na wanawake kwa kutenga sh. bilioni 200.

Alibainisha kuwa, serikali inaendelea kuangalia njia nzuri ya kuimarisha mfuko huo kwa lengo la kuongeza ufanisi kwa walengwa ambapo kwa kushirikiana na sekta binafsi, serikali itaanzisha madirisha ya uwekezaji kwa vijana.

Alieleza kuwa madirisha haya yatatoa mikopo nafuu na mitaji ya uwekezaji kwa biashara za vijana.

TANZANIA IMEKOMAA KIDEMOKRASIA

Dk. Samia, alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika misingi ya demokrasia, lakini bado ipo haja ya kukaa pamoja, kisha kupitia maeneo ambayo yamekuwa na changamoto ili kuimarisha zaidi mfumo wa utawala unaozingatia maridhiano na maslahi ya umma.

“Tanzania imekuwa na miongo mingi ya kidemokrasia. Neno demokrasia, linaweza kutafsiriwa katika namna yoyote ile, lakini sisi ni wakomavu wa demokrasia.

“Pamoja na hayo, katika safari yetu ya kuendesha Tanzania ya kidemokrasia tuko tayari kujifunza na kujirekebisha.

“Niviombe makundi yote ya Watanzania hasa vyama vya siasa, tukae pamoja tuzungumze, tuangalie tumekosea wapi. Tuendelee na safari yetu ya kujenga taifa lenye amani na utulivu na hayo yatafanyika kwa kufuata mila na desturi zetu, siyo kwa shinikizo,” alieleza.

Aliongeza: “Hapana shaka kwamba Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia, ila neno demokrasia kamili linaweza kutafsiriwa kwenye mitazamo tofauti kwani haina kanuni moja. Kama Taifa tunaendelea kujifunza na kujirekebisha.”

Rais Dk. Samia, alitoa wito kwa Watanzania kuitumia fursa ya kipindi hiki kuendelea kujifunza, kurekebisha na kukubaliana kuhusu namna bora ya kuendesha nchi kidemokrasia kwa kuzingatia utamaduni na desturi za taifa.

“Sote kwa umoja wetu tunapaswa tutumie fursa hii kuendelea kujifunza, tukirekebishe na tukubaliane jinsi ya kuendesha nchi yetu kidemokrasia kwa kuzingatia tamaduni, mila na desturi zetu na sio za kuletewa,” alisema.

Alisema kuwa, marekebisho ya Katiba ni miongoni mwa hatua zilizoagizwa ili kufikisha taifa katika maelewano na maridhiano ya kweli ambapo serikali itaanza rasmi kushughulikia suala la mabadiliko ya katiba katika kipindi cha siku 100 za mwanzo wa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Sita hatua itakayoanza kwa kuundwa tume ya usuluhishi na maelewano.

ONYO KWA WATUMISHI WA UMMA

Katika hatua nyingine, Dk. Samia aliwaahidi wananchi kwamba ataunda serikali itakayowajibika, kuendeleza mageuzi ya sera zinazogusa maslahi ya wananchi, hivyo ni lazima viongozi wa ngazi zote za serikali kuwa karibu na wananchi.

“Hivyo basi lazima viongozi wa serikali kwa ngazi zote, kuanzia Mawaziri hadi Maofisa Tarafa, wawe karibu na wananchi ili kuweza kufahamu changamoto zao na kuwajibika kwao. Kwa kuwa ahadi tulizotoa ni nyingi, matamanio ni mengi, matarajio ni makubwa na muda wa kuyatimiza haya ni mchache, tutaongeza kasi ya utekelezaji wa mipango ya serikali ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea.

Aliongeza: “Nayasema haya mapema kwa watendaji waliopo serikalini, wakiwemo Makatibu Wakuu na wale nitakaowateua kwa ajili ya kujitayarisha kisaikolojia na kujipanga vyema kufanikisha malengo hayo.”

“Kwa watendaji waliopo serikalini na wale nitakaowateua, wajiande kisaikolojia wajipange vema kukamilisha malengo ya serikali ya kuwatumikia wananchi, wananchi wanahitaji mabadiliko chanya na maendeleo, watendaji msipobadilika kuendana na matarajio ya wananchi tutawabadilikia,” alisisitiza.

MSISITIZO KIMATAIFA

Rais Dk. Samia alisema Tanzania inathamini ushirikiano wa kimataifa kwani ingependa kuishi na mataifa mengine kwa misingi ya kuheshimiana na kufaana kwani serikali ina dhamira ya dhati kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo na nchi marafiki pamoja na mashirika ya kimataifa.

“Daima tutajielekeza katika kuongeza marafiki na kupanua fursa za kiuchumi kwa nchi yetu na watu wake. Kama Taifa, tunapenda tuheshimiwe kama sisi tunavyoheshimu mataifa mengine. Na katika kulinda maslahi ya nchi, hakuna mbadala.

“Ni lazima tuhakikishe tunalinda utu, heshima na uhuru wetu. Tutaendelea kuongozwa na misingi ile ile ya sera ya nje iliyoasisiwa na waasisi wa nchi yetu ya kutofungamana na upande wowote.

Dk. Samia alisisitiza: “Msimamo wetu ni umoja na ushirikiano badala ya mgawanyiko, majadiliano badala ya amri au mabavu, haki badala ya visasi. Taifa la Tanzania limejengwa kwenye misingi ya amani na utulivu wa kisiasa, nguvu yoyote inayokusudia kuchafua misingi hiyo hatutokubaliani nayo.”  

UCHAGUZI MKUU

Alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi kwa kujitokeza kisha kushiriki vyema katika hatua zote kuanzia kujiandikisha daftari la kudumu la wapiga kura, kuhakiki daftari na kupiga kura.

Alisema wananchi wamethibitisha kuwa kushiriki uchaguzi ndiyo njia ya uhakika na salama yenye kubadilisha viongozi kwani njia nyingine zozote hazina kheri wala salama ndani yake.

“Niendelee kuipongeza Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuendesha vyema uchaguzi mkuu wa kwanza tangu kuundwa upya kwa tume hiyo ambapo safari hii Wakurugenzi wa Halmashauri hawakusimamia uchaguzi, wala hakuna mgombea aliyepita bila kupingwa. Sisi tuliogombea na vyama vyetu, hatukukosa viwanja vya kufanyia mikutano.

“Kwa ujumla, kampeni zilikwenda vyema. Aidha, utaratibu uliofanyika wa kuongeza vituo vya kupigia kura ulisaidia sana kuondoa msongamano katika vituo hivyo. Kwa hakika, upigaji kura ulirahisishwa sana na haukuchukua muda mwingi wa wananchi kama ilivyozoeleka. Jambo hili limewafanya baadhi ya waangalizi wa uchaguzi kudhani kwamba wananchi hawakujitokeza kupiga kura,” alieleza.  

AHADI SIKU 100

Dk. Samia alisema katika hotuba yake ya kufungua kampeni za uchaguzi mkuu Oktoba 28 mwaka huu, alitaja mambo ambayo serikali yake ingeanza nayo ndani ya siku 100 za kazi.

Alisema CCM iliahidi kutoa ajira kwa fani za sekta ya afya na elimu ambapo jana ikiwa ni siku ya 12 tangu muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Sita uanze, tayari imeshatangaza nafasi za ajira 7,000 za walimu na nafasi za ajira 5,000 za watumishi wa afya.

Alieleza kuwa hatua hiyo ni mwanzo kujibu kiu ya wananchi ya kuboresha huduma za afya na elimu huku serikali ikijiandaa kuanza majaribio ya Bima ya Afya kwa Wote.

“Serikali itakuja kwenu Waheshimiwa Wabunge na mapendekezo ya namna ya kufanikisha majaribio hayo, niwaombe muunge mkono mapendekezo hayo ambayo yatakuwa mwanzo wa mageuzi katika upatikanaji huduma bora za afya kwa watu wote nchini. Tunadhamiria pia kuviunganisha vituo vya huduma za afya kidijitali kuhakikisha vinakuwa na vifaa na huduma za viwango stahiki kwa kila ngazi husika.

“Tunakusudia kuweka viwango vinavyofanana ili watumiaji wa bima ya afya mijini na vijijini wawe na huduma zinazolingana. Katika hatua nyingine, nimeshaielekeza Wizara ya Afya kusimamia maelekezo ya kutozuia maiti kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, wakati familia zikiendelea na taratibu za kulipa deni la matibabu kwa njia zinazolinda utu wao.

Aliongeza: “Niseme kwamba, kupitia mpango huu wa bima ya afya, kadhia hii inakwenda kukomeshwa. Kwa sababu gharama za matibabu zitalipwa na bima ya anayetibiwa. Niwasihi wananchi wote kuweka kipaumbele kwa afya zetu, kwa kila mmoja wetu kuwa na bima ya afya pamoja na wanaomtegemea.”

Previous Post

DK. MWIGULU ATUMA SALAMU KWA WALA RUSHWA, WAZEMBE

Next Post

MAAGIZO MATATU KWA DK. NCHEMBA

Next Post
MAAGIZO MATATU KWA DK. NCHEMBA

MAAGIZO MATATU KWA DK. NCHEMBA

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

DK. NCHIMBI ATAJA KIPAUMBELE CCM

DK. NCHIMBI ATAJA KIPAUMBELE CCM

1 month ago
RAIS DK. SAMIA AKABIDHIWA NYARAKA ZA KAZI

RAIS DK. SAMIA AKABIDHIWA NYARAKA ZA KAZI

2 weeks ago

Popular News

  • YANGA, SIMBA KAZI KAZI

    YANGA, SIMBA KAZI KAZI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • KETE YA KWANZA KWA GAMONDI STARS LEO

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • TRA YAHAWAHAKIKISHIA WAFANYABIASHARA WA KARIAKOO USALAMA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • MAAGIZO MATATU KWA DK. NCHEMBA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • NI MARIDHIANO

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
error: Content is protected !!
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2025 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.