Na MWANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewatakia Watanzania kheri ya maadhimisho ya miaka 64 ya Uhuru, ambapo aliwashauri wananchi kuitumia siku hiyo kwa mapumziko nyumbani.
Salamu za Rais Dk. Samia ziliwasilishwa jana kwa niaba yake na Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba, kupitia taarifa aliyotoa kwenye vyombo vya habari.
“Ndugu wananchi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, anapenda kuwatakia wananachi wote kheri ya Sikukuu ya Uhuru wa Tanzania Bara inayoadhimishwa kila mwaka Desemba 9,”alisema Dk. Mwigulu.
Tanzania ilivyobadili utaratibu wa kusherehekea sherehe za uhuru katika miaka kumi kutoka mwaka 2015 hadi mwaka 2025, zimeahirishwa mara sita na fedha zilizokuwa zimetengwa kwa madhimisho ya sherehe hizo zikipelekwa kufanya kazi za kusaidia huduma za jamii nchini.
Rais Dk. Samia alipotangaza Novemba 24, mwaka huu maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania Bara yamesitishwa, fedha zilizotengwa zilielekezwa kukarabati miundombinu ya umma iliyoharibiwa wakati wa vurugu za Oktoba 29.
Hii ilikuwa mara ya tatu tangu aingie madarakani Machi 21, 2021 kuchukua uamuzi kama huo, hatua inayoendeleza utamaduni ulioanzishwa na mtangulizi wake, Hayati Rais Dk. John Magufuli, ambaye mara kadhaa alisitisha sherehe za kitaifa ili kutoa kipaumbele kwa mahitaji ya dharura ya wananchi.
Utaratibu wa maadhimisho hayo yamegeukia katika huduma za jamii, maendeleo na tafakuri ya wajibu wa pamoja badala ya shamrashamra za kijeshi na tamasha.
Siku ya uhuru inazidi kuwa siku si ya kukumbuka historia pekee, pia kuonesha dhamira ya kuendeleza ustawi wa jamii.
Mabadiliko ya kwanza yalitokea Desemba 2022, chini ya mwaka mmoja tangu aingie madarakani.
Serikali ilitangaza hakutakuwa na maadhimisho ya kitaifa, na badala fedha zilizotengwa zipelekwe kujenga mabweni kwa wanafunzi wenye uhitaji maalumu nchini.
Serikali za mikoa na wilaya ziliagizwa kuadhimisha siku hiyo kwa miradi ya kijamii na shughuli za maendeleo.
Desemba 4, 2024, sherehe za uhuru zilisitishwa na taasisi za umma zikaelekezwa kuelekeza fedha zilizotengwa kufanya huduma za kijamii.
Kusitishwa sherehe za mwaka huu ni uponyaji majeraha ya vurugu za Oktoba 29 zilizoleta vifo, majeruhi, uharibifu wa mali na kuharibu miundombinu.
Awali, Dk. Mwigulu alitangaza agizo la Rais Dk. Samia kuwa hakutakuwa na maadhimisho ya uhuru na fedha zielekezwe kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa.
Mwaka huu 2025, Tanzania Bara inatimiza miaka 64 ya Uhuru tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1961.




