Na IRENE MWASOMOLA
BAADHI ya wataalamu wa uchumi wameeleza faida nane zitakazopatikana, kufuatia uwekezaji na uboreshaji utakayofanyikakatika reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Kauli za wataalamu hao zimekuja zikiwa zimepita siku chache tangu serikali iingie mkataba mpya na kampuni ya CCEC ya nchini China, itakayowekeza sh. trilioni 3.45 kwa kujenga vituo vya kisasa na kuboresha miundombinu ya reli hiyo.
Walitaja baadhi ya faida hizo ni kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, pato la taifa, fursa za ajira, kuboresha huduma za usafirishaji wa bidhaa, idadi ya wasafiri na kuifanya Tanzania kuwa kituo Kikuu cha Usafirishaji na Usambazaji Bidhaa Afrika Mashariki (Logistic Hub).
Akizungumza naUHURU, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Mtaalamu wa Uchumi Profesa Abel Kinyondo, alisema uboreshaji utakayofanyika, utachochea huduma za usafiri na ufanisi Bandari ya Dar es Salaam.
“Reli hii itasaidia kuunganisha Bandari yetu ya Dar es Salaam na nchi za Zambia, DRC na Malawi, itafanya Tanzania kuwa Logistic Hub kwasababu mizigo itatoka kwa haraka bandarini watu watafanya biashara.“alisema.
Pia, Profesa Kinyondo alisema uboreshaji wa Reli ya TAZARA utasaidia kuongeza mapato, kwa kuwa idadi ya abiria watakaotumia usafiri huo wataongezeka.
Vilevile, Profesa Kinyondo, alitaja faida nyingine ni kupunguza foleni ya malori ya kusafirisha mizigo katika barabara za mikoa ya Mbeya, Songwe hasa Tunduma.
Profesa Kinyondo alisema faida nyingine ni kusaidia miundombinu ya barabara kuwa salama, kwasababu magari yaliyokuwa yanabeba mizigo ya tani nyingi kupita kiasi itakuwa ikisafirishwa kupitia treni.
Naye Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu Huria (OUT) Dk. Timoth Lyanga alisema uboreshaji huo utatoa fursa za ajira kwa vijana kupitia shughuli mbalimbali za biashara zitakazofanyika.
Pia, Dk. Lyanga alisema reli hiyo itasaidia kuongeza mzunguko mkubwa wa biashara na bidhaa utakao kua kwa kasi.
Dk. Lyanga alisema mkataba mpya utaendelea kuimarisha ushirikiano na kukuza diplomasia ya uchumi kati ya Tanzania na China.
“Baada ya uwekezaji na mkataba mpya tutarajie kuongezeka kwa mapato, idadi ya wasafiri wataongezeka na kurahisisha usafiri, tutatengeneza ajira kwa vijana.
“Lakini hatua hii itakwenda kuimarisha ushirikiano wetu na China na kuwaenzi marais wetu waliofanikisha ujenzi huu mwaka 1970 Mwalimu Nyerere, Kaunda na Mao wa China,”aliongeza.
Kwaupande wake Mtaalamu wa Uchumi Dk. Donald Mmari, alisema sekta ya usafirishaji ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi, hivyo uwekezaji katika reli hiyo utaongeza tija na uzalishaji.
Juzi Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Gerson Msigwa lisema, Tanzania na Zambia, zimeingia makubaliano na China kupitia kampuni ya CCECC, ambapo China itawekeza dola za Marekani bilioni 1.4, sawa na zaidi ya sh. trilioni 3.45.
Alieleza kuwa, uwekezaji huo, unalenga kuboresha miundombinu ya reli ya Tazara, kujenga vituo vya kisasa, kununua treni za abiria na kujenga kituo kikubwa cha ‘Kidatu Trans shipment Joint Facility.’
Kituo hicho, kitawezesha mizigo kutoka reli ya kati yenye kiwango cha MGR, kuhamishiwa katika reli ya Tazara yenye kiwango cha Cape Gauge, hivyo kuongeza ufanisi wa usafirishaji.
Msigwa, aliongeza kusema pamoja na uboreshaji wa miundombinu, Kampuni ya CCECC, itatekeleza mradi huo kwa miaka mitatu na kuendesha reli ya Tazara kwa kipindi cha miaka 30.
Katika kipindi hicho, Serikali ya Tanzania, itakuwa inapokea Dola za Marekani milioni 30 kila mwaka, sawa na sh. bilioni 75, tofauti na hali ya sasa ambayo inalazimika kutoa zaidi ya sh. bilioni 28 kila mwaka kuchangia uendeshaji wa reli hiyo.
Ujenzi wa reli ya TAZARA ulifanyika kati ya mwaka 1970 na 1975 kupitia fedha za mkopo usio kuwa na riba kutoka nchini China na kukabidhiwa rasmi kwa Tanzania na Zambia mwaka 1976.
Mradi huu ni wa kihistoria ambao uliasisiwa na Rais wa Awamu ya Kwanza Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Zambia Keneth Kaunda na Rais wa China Mao Zedong.




