Na SUPERIUS ERNEST
MWAKA unajumla ya siku 365 au 366. Huo ni muda mrefu sana kwa maisha ya mwanadamu anayeishi duniani.
Ukiona mwaka unaanza na unamalizika ukiwa mzima wa afya; una kila sababu ya kumshukuru Mungu na kujitathimini katika majukumu mbalimbali uliyoyafanya. Kufahamu wapi uliposhindwa na pale ulipofanikiwa.
Mtu binafsi lazima ajitathimini kwa vile alivyojenga uchumi, pale aliposhindwa na alipofanikiwa. Pia, kujitafakari mchango wake kwa Taifa.
Ikiwa leo Desemba 31 ni siku ambayo ilisubiriwa na kila mtu anayeishi duniani, kwani ifikapo saa 6:01 usiku, mwaka wa 2025 utamalizika na kuanza mpya wa 2026, kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake akijua maisha hayana ‘extra time’.
Kwa umuhimu huo, wadau wa maendeleo na wataalamu mbalimbali wa masuala ya kiuchumi wameeleza namna ambavyo wananchi wanaweza kuingia mwaka mpya wa 2026, kwa mafanikio na kutimiza malengo yao binafsi na kuchangia maendeleo kwa taifa.
SAUTI ZA WADAU
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dodoma, (UDOM), Profesa Wineaster Anderson, alisema ni jambo kubwa la kumshukuru Mungu kumaliza mwaka na kuanza mwingine.
Alisema mwaka unapoanza, ni vyema kufahamu mipango binafsi ya maendeleo na mipango ya Taifa inayotakiwa kutekelezwa katika kuchochea maendeleo.
“Kama Taifa tunaongozwa na Dira 2050, Ilani ya Chama 2025-2030 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Miongozo yote hii na mingine, inatupa mwanga na matumaini.
Kama ilivyo kaulimbiu ya serikali yetu, isemayo “Ni Kazi na Utu, Tunasonga mbele” tuikeleze na kuiishi, kwani hayo yatakayotuvusha katika taifa lenye vijana ambao ni zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wote”alisema.
Alisisitiza vijana kufanya kazi kwa bidii, kutambua wajibu wa kujenga, kulinda na kuendeleza taifa lao kwa sasa na baadaye.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kampasi Kuu ya Kivukoni, Dk. Philip Daninga alisema ni jambo kubwa kupata kibali cha kuvuka mwaka, ni suala la kumshukuru Mungu, kwani mwaka unamzunguko mkubwa na mambo mengi yanatekelezwa ndani ya mwaka huo.
Dk. Daninga alieleza kuwa, pamoja na changamoto na mambo mengi ambayo mtu anayapitia ndani ya mwaka mzima, lazima maisha yaendelee ya kujenga uchumi wake na taifa kwa ujumla.
“Kila wakati na majira yake, tunapomaliza na kuanza mwaka mpya lazima kila mmoja ajipange upya, ajitathimini na kujitafakari anavyoweza kuchochea maendeleo na mafanikio zaidi ya vile alivyokuwa mwaka huo,”alisema.
Alisisitiza kuwa, kila mwananchi anatakiwa kujipima na kuanza kivingine kuanzia pale alipoishia apige hatua zaidi ya ile aliyokuwa nayo awali.
Kwa mujibu wa Dk. Daninga, kila mwananchi anatakiwa kujitathmini maendeleo yake, apige hatua asidumae kimaendeleo atafute njia ya kuongeza uzalishaji wake.
Dk. Daninga alieleza kuwa, kama ni mkulima ajitume zaidi, kulingana na hali iliyopo atumie mvua vizuri zinazonyesha kutengeneza uzalishaji zaidi ambao ndio chakula na uchumi.
“Katika mwaka huu mpya, tufahamu kuwa, muda ni mali, asiwepo wa kupoteza muda, bali uwe na thamani kwa kila mmoja katika kuzalisha, tuzidi kujenga nchi kila mmoja atimize ahadi yake muda wa maneno umeisha mwaka mpya ufanye vitendo kufikia malengo,”alisema.
Alisisitiza kuwa,kama hayo yatatekelezeka mwaka mpya utakuwa wa mapinduzi katika maendeleo na kuandika ukurasa mpya wa mafanikio.
Kuhusu familia, Dk.Daninga alisema ni vyema wanafamilia wakajitathimini waliposhindwa kutimiza malengo ya maendeleo na uhusiano, hivyo kuamua kusongambele kwa kasi kubwa kuhakikisha mipango mipya inatekelezeka bila kukwamishwa na changamoto za mwaka uliopita.
Aliongeza “Mapinduzi yanakuja kutokana na changamoto, hivyo kwa magumu tuliyopitia mwaka 2025, iwe chachu ya mafanikio zaidi kwa mwaka mpya kufikia malengo kusudiwa,”alisema.
Aliwasisitiza vijana kuwa na mawazo chanya ya maendeleo, kutumia vyema mitandao ya kijamii kupata mawazo chanya ya maendeleo, kutafuta maarifa sio kuchezea mitandao ya kijamii kwa mambo yasiyo na tija.
Daninga alieleza, hivi sasa digitali ni sehemu kubwa ya maendeleo ya kiuchumi, waitumie kupata ujuzi mpya kadiri wanavyoweza, fursa za ujasiriamali, kilimo kwa kuuza mazao, kwani njia hiyo itafanikisha mapinduzi ya kiuchumi, kuongeza uzalishaji na ufugaji huku akisisitiza, kazi ndiyo itamwezesha kijana kuwa wa tofauti na mwingine wakati wote.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Utafiti Tanzania, Dk. Donald Mmari alisisitiza wananchi wafanye kazi kwa bidii na kuzingatia nidhamu ya fedha wanapoingia mwaka mpya.
Alisema mwanzo wa mwaka ndiyo wa kuweka malengo na siyo kuingia bila ya kuwa na mipango, kwani hautakuwa na msukumo wa kutekeleza jambo lolote la maendeleo.
Mwenyekiti wa Mawakili wa Serikali Tanzania, Wakili Addo Novemba, alisisitiza kuwa ni jambo kubwa la kumshukuru Mwenyezi Mungu kumaliza mwaka, kwani siyo jambo rahisi.
Alisema mwaka unapoanza ni vyema kila mwananchi akafahamu kuwa, mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe siyo vinginevyo, kila mtu ajipange kutekeleza hilo.
Novemba alisema katika mwaka 2025, yapo mambo mengi yamefanyika kwa taifa hususan maboresho ya sheria, kutoa fursa zaidi kwa wananchi.
Alieleza kuwa, kwa sasa Tanzania imeendelea kuandika ukurasa mpya kimataifa kwani inaakiba ya tani 10 za dhahabu, ikiwa ni mara ya kwanza kuandika rekodi hiyo.
Pia, kumekuwepo na mabadiliko ya kupunguzwa kodi yaliyochochea kufikiwa lengo la kukuza uchumi mkubwa wa taifa katika uongozi wa Rais Dk. Samia, hivyo kuingia mwaka mpya kutakuwa na mafanikio zaidi kwa msingi huu imara.
“Pamoja na mengi kufanyika, ni vyema kufahamu hakuna haki pasipokuwa na wajibu, kila mmoja awajibike kulipa kodi, kuitetea na kuisemea vyema Tanzania ndani na nje ya nchi, kwani ndiye mlezi wetu na mama yetu wakati wote,”alisema.
Alisisitiza 2026, kila mmoja awekeze katika kufanya kazi zaidi, kwa bidii kudumisha upendo, ushirikiano kuondokana na ubaguzi kwa kila mmoja, kufuata sera nzuri na imara.
Alisisitiza kuwa, kila mtu akitimiza wajibu wake, katika maendeleo yake binafsi na taifa atakuwa na mafanikio makubwa zaidi ya vile alivyokuwa mwaka jana.




