Na ABDUL DUNIA
Kwa mara ya kwanza katika historia, timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imefanikiwa kutinga hatua ya 16 bora ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Taifa Stars imefuzu hatua hiyo kama moja ya timu bora zilizomaliza nafasi ya tatu (best losers), baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Tunisia katika mchezo wa mwisho wa Kundi C uliochezwa kwenye Uwanja wa Prince Moulay, Rabat nchini Morocco.
Matokeo hayo yaliifanya Tanzania kufikisha jumla ya pointi mbili, na kuwa miongoni mwa timu nne zilizokusanya pointi nyingi zaidi kati ya timu zilizomaliza nafasi ya tatu katika makundi mbalimbali.
Katika kundi lake, Tanzania ilimaliza katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi mbili, baada ya kutoka sare michezo miwili na kupoteza mchezo mmoja. Taifa Stars ilianza mashindano kwa kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Nigeria, kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Uganda na kisha sare nyingine ya bao 1-1 dhidi ya Tunisia.
Kwa upande wa timu zilizofuzu kama best losers, Tanzania imeungana na Msumbiji, Benin na Sudan ambazo kila moja ilikusanya pointi tatu, huku Tanzania ikipata pointi mbili.
Hata hivyo, Tanzania imefanikiwa kuzipiku Angola na Comoro zilizokusanya pointi sawa, kutokana na kuwa na faida ya kufunga mabao mengi zaidi, hivyo kukata tiketi ya kusonga mbele katika michuano hiyo ya bara la Afrika




