IRENE MWASOMOLA NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amewabana wawekezaji wa nje wanaofanya ‘usanii’ wa kuwamilikisha hisa watu ambao siyo halisi wakiwemo madereva wa teksi katika kampuni zao za madini.
Pia, amewataka wasambazaji wazawa wanaotoa huduma hafifu migodini kutojificha katika kichaka cha uzawa.
Mavunde alisema hayo jijini Mwanza, alipofungua Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji Watanzania katika sekta ya madini.
Mavunde alisema amebaini baadhi ya wawekezaji, wametafuta madereva taksi na kuwasainisha hisa asilimia 20.
“Wale ambao mlitaka kuingia ubia, mmeingia nchini, ujanja umefanyika mkaenda kutafuta madereva teksi mkawasainisha (hisa) zile asilimia 20,”alisema.
Alisema tayari kuna kampuni moja serikali imeipa mwaka mmoja, imalizie muda wake iondoke nchini na kazi iliyokuwa inaifanya, itafanywa na Watanzania wenyewe.
Mavunde alisema lazima kila kampuni za uwekezaji, zifuate na kuheshimu sheria zilizotungwa nchini, licha ya kwamba wamekuja na mitaji.
“Hii ni nchi, lazima iheshimiwe, tutaendelea kutoa usaidizi kuhakikisha tunaboresha mazingira ya uwekezaji,”alisema.
Alisisitiza kuwa, hakuna mwekezaji wa kuipangia serikali na kujificha katika kichaka cha mitaji.
“Nimesikia wawekezaji mnasema mmekuja na mitaji, halafu mnapangiwa cha kufanya, nataka niwaambie mmekuja na mitaji madini mmeyakuta hapa Tanzania,”alisema
Mavunde alisema anaamini mwekezaji anapokuja kuwekeza nchini anakuwa ameelewa sheria na taratibu .
Aidha Mavunde alisema baada ya kuwepo kwa changamoto hiyo serikali imefanya mabadiliko ya kanuni na kutibu.
Mavunde, alisema wizara yake, imejizatiti kuona Watanzania wananufaika na asilimia 20 huku akiuagiza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kusaidia kubaini hilo.
TANZANIA YA TANO AFRIKA
Waziri huyo, alisema Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hivi sasa ina hifadhi tani 28 za dhahabu ambayo inaiwezesha kuingia miongoni mwa benki tano kati ya 10 zenye hifadhi kubwa ya madini hayo barani Afrika.
Alisema nchi inayoongoza kuwa na hifadhi ya madini kupitia benki kuu ni Algeria, ambayo ina tani 174 na ya mwisho ni Msumbiji ambayo ina tani 6.85
“Ndani ya muda mchache leo Benki ya Tanzania ina hifadhi ya dhahabu tani 28 na kuingia tano bora ndani ya miezi 19, haya ni mafanikio chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,”alisema
Kwa mujibu wa Mavunde, awali Tanzania haikuwepo katika nchi 10 bora ambazo zina uhifadhi mkubwa wa dhahabu kupitia benki kuu yake.
Mavunde, alisema mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na marekebisho ya sheria, ambayo yameiwezesha BoT kuwa na hifadhi hizo.
Alisema mafanikio hayo, yalitokana na uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan, mwaka 2024 kuelekeza kufanya marekebisho ya sheria ya madini.
“Rais Samia alitoa maelekezo mwaka 2024, tukafanya marekebisho ya sheria kwa wakati ule kilikuwa kifungu cha 59, kifungu kile kikafanyiwa marekebisho kikawa kinasomeka ifuatavyo, mmiliki yeyote wa leseni atatenga asilimia zisizopungua 20 za madini yanayozalishwa kwa uchakataji, usafishwaji, uyeyushwaji na kufanyiwa biashara ndani ya nchi.
“Hayo ndiyo marekebisho ya sheria, ambayo tuliyofanya, baada ya marekebisho hayo ya sheria, Benki Kuu ya Tanzania (BOT), ilipata nafasi ya kuanza kuwa mnunuzi wa dhahabu Oktoba Mosi 2024, ilianza rasmi kununua dhahabu,”alisema.
Kuhusu mafanikio katika sekta ya madini nchini, Mavunde alisema sekta hiyo, imechangia mfuko wa maendeleo serikali zaidi ya sh. trilioni 1.3 hadi kufikia Juni 30, mwaka huu.
Alisema kutokana na mapato hayo sekta hiyo imeongoza kwa mapato katika mapato yasiyo ya kikodi.
Pia, alisema Watanzania 16, 695 wameajiriwa katika ajira rasmi na wengine milioni 6 wakinufaika na sekta hiyo katika mnyororo wa thamani wa madini pamoja na fursa ya nafasi ya watendaji wakuu wa kampuni za migodi.
Akizungumzia ufunguzi wa migodi mipya ya madini, Mavunde alisema hadi hivi sasa serikali imeshaingia mikataba na kampuni 13 zitakazofungua shughuli za uchimbaji katika migodi.
Alisema ufunguzi wa migodi hiyo kutaongeza idadi ya migodi iliyopo hivi sasa, huku akiwataka wasambazaji huduma kujiandaa.
“Migodi hiyo inakuja, kazi zinakuja mtachoka kazi je mko tayari, kajiungeni mfanye kazi fursa hii isiwatoke najua mna uwezo wa kufanya kazi,”alisema.
Katika ujenzi wa viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotumika katika migodi, Mavunde alisema serikali imepokea maombi ya kampuni 31 kutoka nje ya nchi kufungua viwanda hivyo.
Waziri Mavunde alitoa rai kwa sekta binafsi kutumia fursa hiyo, huku akisema katika maombi yaliyotolewa bado hakuna kampuni za wazawa zilizojitokeza.
Alisema serikali imetenga eneo la Buzwagi mkoani Shinyanga, kuwa eneo maalumu la viwanda vinavyozalisha bidhaa za migodini.
Alisema tayari wamepokea maombi yapatayo 31 kutoka kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi.
MHANDISI YAHYA SAMAMBA
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mhandisi Yahya Samamba, alisema serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta ya madini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
AMIR MKALIPA
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, aliipongeza wizara kwa jitihada zake za kuendelea kuvutia uwekezaji mkoani humo.
Alisema uwekezaji huo umechangia kuanzishwa kwa Mgodi wa Dhahabu wa Sotta Mining, ambao unatarajiwa kutoa ajira 1,500 utakapoanza uzalishaji.
DK. JANET LEKASHINGO
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dk. Janet Lekashingo, alisema jukwaa hilo limekuwa na manufaa makubwa katika kuchochea ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo.
Alisema mafanikio hayo yanaonekana kupitia ongezeko la uwasilishaji wa mipango ya ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta hiyo kutoka mipango 51 mwaka 2018 hadi kufikia mipango 1,312 mwaka jana.




