Na MWANDISHI MAALUMU
MAKAMU wa Rais, Deogratius Ndejembi, amewataka watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kuongeza bidii, uwajibikaji na kuachana na utendaji kazi kwa mazoea.
Pia, wahakikishe majukumu ya serikali yanatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.
Ndejembi alitoa wito huo jijini Dodoma, alipofanya ziara yake ya kwanza katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), iliyopo Mtumba, ambako alipokelewa na wafanyakazi pamoja na menejimenti ya wizara hiyo.
Alisisitiza umuhimu wa watumishi, kubadili mitazamo na namna ya kufanya kazi, akitaka kila mmoja kuwa mbunifu na kuweka mipango inayolenga kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi na taifa.
Makamu wa Rais, aliwasihi watumishi kutumia nafasi zao kutoa huduma yenye thamani kwa Watanzania na kutambua dhamana waliyonayo katika kuwahudumia wananchi.
Pia, aliwataka kubadili mitazamo na namna ya kufikiri, kuwa wabunifu na kuhakikisha mipango inayowekwa inakuwa na tija na matokeo chanya katika shughuli zinazotekelezwa kwa maslahi mapana ya Taifa.
Ndejembi aliwataka kuongeza jitihada katika kudumisha Muungano kwa kuwa na mipango endelevu, inayolenga kutatua changamoto mbalimbali na kutoa elimu ya fursa zilizopo katika Muungano.
Aliwasihi viongozi na watumishi wa wizara hiyo, kuwa na mipango endelevu katika utekelezaji wa ajenda ya ulinzi na uhifadhi wa mazingira kwa kutumia vizuri kampeni za upandaji miti, usafi wa majiji na miji kwa kuweka nyenzo zitakazosaidia kufanya hali hiyo kuwa endelevu.
Vilevile, Ndejembi alisisitiza umuhimu wa kuwa na mpango maalumu utakaosaidia wananchi kuhama katika shughuli za kila siku zinazoharibu mazingira.
MHANDISI HAMAD YUSSUF MASAUNI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, alimpongeza Makamu wa Rais kwa kuaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, katika nafasi hiyo na kumhakikishia ushirikiano kutekeleza majukumu mbalimbali yanayohusu Ofisi ya Makamu wa Rais.
DK. RICHARD MUYUNGI
Akiwasilisha taarifa kuhusu shughuli zinazotekelezwa na idara mbalimbali zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk. Richard Muyungi, alisema wizara hiyo ina Idara nne, vitengo vinane na taasisi mbili zinazotekeleza majukumu mbalimbali, ukiwemo utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika masuala ya Muungano na Mazingira.
Wakati huohuo, Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, anatarajiwa kuwasili leo mkoani Kilimanjaro kwa ziara binafsi ya kifamilia.
Lengo la ziara hiyo ni kusalimia na kupewa baraka na familia yake iliyopo Kata ya Bondeni, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Ziara hiyo, imekuja zikiwa zimepita siku mbili tangu kuapishwa kwake kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania akichukua nafasi ya Dk. Emmanuel Nchimbi aliyejiuzulu kabla ya Chama Cha Mapinduzi kumfuta uanachama.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema hiyo ni ziara binafsi ya Makamu wa Rais.
Babu alisema Ndejembi anatarajiwa kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro asubuhi na kwenda moja kwa moja Mbuyuni, Manispaa ya Moshi, Kata ya Bondeni.




