ULAANBAATAR, Mongolia
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema Tanzania imeweka mkazo katika elimu ya hali ya hewa, maendeleo na uwekezaji binafsi na ushirikiano kwa umma kwa lengo la kuongeza urejeshaji wa maeneo ya malisho, kila mmoja awe na wajibu wa kulinda udongo.
Pia, inakuza malisho endelevu, mipango shirikishi ya matumizi ya ardhi, urejeshaji maeneo ya malisho, miundombinu iliyoboreshwa ya maji, mifumo ya tahadhari ya mapema ya ukame na uzalishaji bora wa mifugo.
Waziri Masauni ameeleza hayo jijini Ulaanbaatar, Mongolia, Agosti 26, mwaka huu, katika kikao cha viongozi kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika cha kujadili kuenea hali ya jangwa na ukame katika eneo la kuboresha afya ya udongo na matumizi sahihi ya mbolea.
Kikao hicho ambacho kimefanyika ofisi za ubalozi wa Uingereza, kimehudhuriwa na Mwakilishi Maalumu wa Uingereza, Ruth Davis, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Beth Bechdol, Moses Vilakati, Kamishna wa Umoja wa Afrika (AU) anayeshughulikia Kilimo, Maendeleo ya Vijijini, Uchumi wa Bluu na Mazingira Endelevu pamoja na viongozi wengine kutoka mataifa mbalimbali.
“Kwa Tanzania, maeneo ya malisho ni muhimu sana kwa uzalishaji wa mifugo, usalama wa chakula, bayoanuwai, rasilimali za maji na maisha ya watu vijijini. Kutokana na idadi ya watu inayokadiriwa kufikia milioni 61.7, kuna ongezeko la shinikizo kwenye ardhi, maji na rasilimali asili,” amesema Masauni.
Amebainisha kwa mujibu wa Ripoti ya Utafiti wa Sampuli ya Kilimo wa Mwaka 2022/23 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Tanzania ilikuwa na kaya za wakulima milioni 8.97, ambapo asilimia 60.6 kati ya hizo zilijishughulisha na ufugaji hali inayodhihirisha umuhimu wa maeneo bora ya malisho kwa jamii na uchumi.
Hata hivyo, Masauni amesema maeneo ya malisho yanakabiliwa na shinikizo linaloongezeka kutokana na ukame, uharibifu wa ardhi, ufugaji kupita kiasi, mabadiliko ya matumizi ya ardhi, uhaba wa maji, uchomaji misitu na mabadiliko ya hali ya hewa.
Amefafanua kwa kutambua hilo, Tanzania imejiwekea mikakati kupitia Programu ya Kitaifa ya Kupambana na Kuenea Hali ya Jangwa na Ukame (2025-2030), unaozingatia utayari wa ukame, tahadhari ya mapema na usimamizi endelevu wa ardhi.
Waziri huyo ameeleza jitihada hizo zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hasa Nguzo ya Tatu ya Uhifadhi wa Mazingira na Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi, inayounganisha urejeshaji maeneo ya malisho na mabadiliko ya mifugo, usalama wa chakula na ustahimilivu wa hali ya hewa.
Mhandisi Masauni yupo Mongolia anakoshiriki Mkutano wa 17 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea Hali ya Jangwa na Ukame (UNCCD COP 17) ambao umeanza Agosti 24, mwaka huu




