• ePaper
Wednesday, September 9, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Habari

WAZIRI AONYA, ATOA SIKU 60 WENYE SILAHA HARAMU

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
September 1, 2026
in Habari, Kitaifa
0
WAZIRI AONYA, ATOA SIKU 60 WENYE SILAHA HARAMU
0
SHARES
15
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na SELINA MATHEW, Dodoma

SERIKALI imeagiza kuanza zoezi la kitaifa la uhakiki wa umiliki na mienendo ya silaha nchini.

Imesema lengo ni kutambua kila silaha, wamiliki wake na namna zinavyomilikiwa na watu.

Waziri Katambi, amesema ametolewa siku 60 kwa wenye silaha haramu, kuzisalimisha bila kushtakiwa.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, alitoa agizo hilo jana, alipozindua kampeni ya msamaha wa usalimishaji silaha haramu kwa hiyari jijini Dodoma.

Alisema uhakiki huo, utafanyika sambamba na mpango wa kuweka taarifa za silaha kwa mfumo wa kidijitali, kurahisisha ufuatiliaji na kuzuia silaha kuingia katika mikono isiyo salama.

Katambi alisema hatua hiyo, inatokana na kuwepo baadhi ya wamiliki kutumia silaha kinyume cha masharti, wakiwemo wanaojionyesha hadharani na kubeba bila vielelezo vinavyohitajika huku wengine wakizisahau katika maeneo ya hoteli, nyumba za kulala wageni au usafiri wa umma.

“Nakuagiza IGP, anzisha zoezi jingine la uhakiki wa umiliki wa silaha ili tuwe na taarifa kidijitali, tujue zinaenda wapi, ‘movement’ ya silaha,” alisema Katambi.

Alisema uhakiki huo, utasaidia mamlaka kutambua wamiliki wanaofuata masharti na wanaokiuka utaratibu, akisisitiza umiliki wa silaha ni haki inayokwenda na wajibu wa kufuata sheria.

Aliwataka wamiliki halali wa silaha hizo, kujihakiki na kuhakikisha wana leseni zinazotambulika, wamelipa ada zinazohitajika na wana vielelezo vya umiliki.

Aliwataka wanaosafiri na silaha, kuhakikisha wanakuwa na vibali vinavyotakiwa.

Alisema mtu anayemiliki silaha kihalali, ameshindwa kutimiza masharti ya umiliki, anaweza kupoteza sifa ya kuendelea nayo, kwa kuwa uhalali wa silaha, unatokana na kufuata masharti yaliyowekwa kisheria.

Pia, alikemea tabia ya baadhi ya wamiliki kutumia silaha kama mapambo au njia ya kujitafutia umaarufu, akisema silaha haipaswi kuwa chombo cha kujionesha mbele ya jamii.

“Hatumiliki silaha kwa fasheni, tunamiliki silaha pale palipo na matishio ya kiusalama. Siyo sifa na wala hatumiliki kwa kutafuta sifa kwenye jamii,” alisema.

MSAMAHA URASIMISHAJI SILAHA

Katambi alitangaza msamaha kwa watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria, watapewa fursa ya kuzisalimisha bila kushtakiwa kuanzia leo hadi Oktoba 31, mwaka huu.

Alisema usalimishaji huo, utafanyika vituo vya polisi, ofisi za serikali za mitaa na ofisi za watendaji wa kata kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni.

“Serikali inawasihi wananchi wanaomiliki silaha isivyo au kinyume cha sheria, mjitokeze kwa wingi, mtumie fursa hii kusalimisha silaha mnazomiliki,” alisema.

Katambi alionya baada ya kipindi cha msamaha kumalizika, yeyote atakayekutwa na silaha haramu, atachukuliwa hatua za kisheria, akisisitiza wananchi wasisubiri hadi dirisha hilo lifungwe.

Alisema kampeni hiyo, itafanyika nchi nzima kwa kushirikisha Jeshi la Polisi, viongozi wa mikoa na wilaya, viongozi wa kata, vijiji na mitaa, taasisi za dini, asasi za kiraia na vyombo vya habari.

Aliwataka wananchi wanaofahamu watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria, kutoa taarifa kwa mamlaka ili uchunguzi ufanywe kubaini uhalali wa umiliki huo.

Katambi alisema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali za kuzuia uzagaaji silaha haramu na kuimarisha amani na usalama wa wananchi,.

Alisema silaha zisizodhibitiwa, zinaweza kutumika katika uhalifu na kuhatarisha maisha pamoja na mali za watu.

Alilipongeza Jeshi la Polisi chini ya IGP, Camillus Wambura, kwa juhudi za kubaini na kukamata silaha zilizokuwa zikimilikiwa kinyemela na zile zilizokuwa zimetoroshwa.

Alisema uhakiki wa umiliki wa silaha, utasaidia pia uchunguzi wa uhalifu, kwa kuwa mamlaka zitakuwa na uwezo mkubwa wa kufuatilia chanzo na historia ya silaha inayohusishwa na tukio fulani.

ONYO WANAOTUMIA VIBAYA MITANDAO

Katika hatua nyingine, Katambi aliwataka Watanzania kutotumia uhuru wa kujieleza katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, kuchochea migawanyiko, ubaguzi wa kidini, kikabila, kisiasa na kutoa taarifa za uongo zinazoweza kuhatarisha amani ya nchi.

Alisema serikali inaheshimu uhuru wa maoni, kujieleza, kupata na kutoa habari kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba, lakini uhuru huo haupaswi kutumiwa kama kisingizio cha kuvunja sheria.

“Uhuru wa maoni, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kutoa habari na kupashana habari upo kwa mujibu wa Ibara ya 18. Tutaisimamia kwa wivu mkubwa ili haki hiyo iendelee kuwepo, lakini tusitumie uhuru tulionao kuliangamiza taifa letu,” alisema.

Alisema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kutoa kauli zinazolenga kuligawa taifa, kuchochea ubaguzi au kuleta taharuki kwa wananchi.

Pia, alisema baadhi ya watu wanaosambaza takwimu za serikali zisizo sahihi na kutoa taarifa za uongo kuhusu mipango na utekelezaji, hali ambayo inaweza kuleta taharuki na kupotosha wananchi.

Alisisitiza vyombo vya habari na watumiaji wa mitandao, wanapaswa kuwa makini na taarifa wanazochapisha au kusambaza kwa kuwa, matumizi yasiyo sahihi ya majukwaa hayo, yanaweza kuathiri amani na utulivu wa taifa.

Alisema serikali itaendelea kusimamia sheria dhidi ya watakaokiuka mipaka ya uhuru wa kujieleza, huku akisisitiza hatua hizo hazilengi kuzuia haki za wananchi bali kuhakikisha haki hizo zinatumika kwa kuzingatia sheria.

Waziri huyo, alisema Tanzania inapaswa kuendelea kujifunza kutokana na nchi mbalimbali duniani zinazokumbwa na migogoro inayochochewa na tofauti za kisiasa, kidini, kikabila na makundi.

IGP WAMBURA

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Camillus Wambura, alisema serikali imetoa fursa kwa wananchi wanaomiliki silaha haramu, kuzisalimisha kwa hiyari bila kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kwa mujibu wa kifungu cha 66 cha Sheria ya Udhibiti wa Silaha na Risasi ya mwaka 2021, mtu anayesalimisha silaha haramu kwa hiyari, anapata kinga dhidi ya mashtaka.

“Ujumbe wetu kwa wananchi ni mmoja na uko wazi; kama una silaha haramu, huu ni wakati wa kuisalimisha kwa hiyari. Usisubiri silaha hiyo itumike katika tukio la uhalifu, usisubiri ukamatwe nayo,” alisema.

Alisema Jeshi la Polisi, limeendelea kuchukua hatua dhidi ya umiliki na matumizi ya silaha kinyume cha sheria, ambapo katika kipindi cha miaka mitatu na miezi sita, kuanzia mwaka 2023 hadi sasa, silaha 990 zilikamatwa kupitia operesheni za kuzuia uhalifu.

Aidha, alisema silaha nyingine 32 zilizokuwa zikimilikiwa kihalali, ziliibwa kutoka kwa wamiliki wake katika kipindi hicho.

IGP Wambura, alisema kampeni hiyo si mbadala wa operesheni za kipolisi, bali ni nyenzo ya ziada ya kuzuia silaha haramu zisitumike katika uhalifu kabla madhara hayajatokea.

Alitoa wito kwa viongozi wa serikali, dini, kimila, watendaji wa maeneo, vyombo vya habari na wananchi, kushirikiana kuwafikia watu wanaomiliki silaha hizo na kuwaelimisha kuhusu fursa ya kuzisalimisha.

Alisema kati ya mwaka 2023 na Juni, mwaka huu, wamiliki 60 walisitishiwa umiliki wa silaha kwa kukiuka masharti ya umiliki na matumizi.

MKUU WA MKOA

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, aliipongeza Serikali, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi, kuendelea kuimarisha usalama nchini.

Alieleza kuwa, hali ya usalama Dodoma, imeendelea kuwa nzuri na kuwawezesha wananchi kutumia muda mrefu kufanya shughuli za maendeleo.

“Wananchi wa Dodoma wanapata muda mwingi wa kushughulika na maendeleo kuliko kushughulika na usalama,” alisema.

Mbunge wa Jimbo la Dodoma na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Pascal Chinyele, alisema silaha haramu ni tishio kwa usalama wa wananchi katika vijiji na mitaa.

Alisema kwa kuwa Tanzania inapakana na nchi mbalimbali, baadhi ya silaha zinaweza kujipenyeza na kuingia katika jamii, huku akiwataka ndugu wa watu waliokuwa na silaha halali, lakini wamefariki dunia, kuzisalimisha.

Previous Post

NDEJEMBI MZIGONI RASMI, AKEMEA KAZI KWA MAZOEA

Next Post

RAIS DK. SAMIA, NDEJEMBI TURUFU YA MAENDELEO KWA WATANZANIA

Next Post
RAIS DK. SAMIA, NDEJEMBI TURUFU YA MAENDELEO KWA WATANZANIA

RAIS DK. SAMIA, NDEJEMBI TURUFU YA MAENDELEO KWA WATANZANIA

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

DK. NCHIMBI AAHIDI HUDUMA ZA AFYA KWA WATANZANIA

DK. NCHIMBI AAHIDI HUDUMA ZA AFYA KWA WATANZANIA

11 months ago
PAWASA, MTEMI WAZIPA MCHONGO YANGA, SIMBA

PAWASA, MTEMI WAZIPA MCHONGO YANGA, SIMBA

8 months ago

Popular News

  • RAIS DK. SAMIA, NDEJEMBI TURUFU YA MAENDELEO KWA WATANZANIA

    RAIS DK. SAMIA, NDEJEMBI TURUFU YA MAENDELEO KWA WATANZANIA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • WAZIRI AONYA, ATOA SIKU 60 WENYE SILAHA HARAMU

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • NDEJEMBI MZIGONI RASMI, AKEMEA KAZI KWA MAZOEA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • TUME MIPANGO, NIRC WAJADILI UBORA MIRADI YA UMWAGILIAJI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • MASAUNI AANIKA UMAHIRI WA TANZANIA INAVYOLINDA UDONGO, MATUMIZI MBOLEA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Not enough quota to unlock this post
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?