Na MWANDISHI WETU
KUFUATIA kuimarishwa kwa mfumo wa udhibiti wa biashara haramu ya madini unaofanywa na Wizara ya Madini kupitia Kikosi Kazi (Taskforce), madini aina ya dhahabu Gramu 4,402.20 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.2, yamekamatwa wakati yakitoroshwa.
Hayo yamesemwa leo Julai 27, 2026 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.
Amesema serikali kupitia Wizara ya Madini iliunda Kikosi kazi ambacho kinahusisha vyombo vya dola ili kudhibiti biashara haramu ya madini na utoroshaji na hii, ni sehemu tu ya kazi ambazo zimeendelea kufanywa na Kikosi kazi hicho katika kuimarisha mfumo wa ufanyaji biashara ya madini.
“Ndugu zangu, dhahabu hii yenye zaidi ya thamani ya bilioni 1.2 haikupitia katika mfumo rasmi wa ufanyaji biashara ya madini, hivyo kupelekea serikali kukosa mapato ambayo yangeisaidia kuimarisha utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi,” amesema Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde amebainisha kuwa, dhahabu hiyo iliyokamatwa imetaifishwa kwa mujibu wa taratibu za sheria na imehifadhiwa Benki Kuu ya Tanzania.
Vilevile, Waziri Mavunde amekielekeza Kikosi Kazi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, kumhoji vizuri mtuhumiwa aliyekamatwa na dhahabu hizo kufahamu alikotoka na alikuwa anapeleka wapi, ili kutibu kabisa mzizi wa vitendo hivyo.
Pia, ameelekeza kuwa, kama mtuhumiwa huyo ana leseni ya ufanyaji biashara ya madini, afutiwe mara moja na kuingizwa kwenye orodha maalumu ya watu ya wenye makosa (blacklisted), ili asiruhusiwe tena kufanya biashara hiyo.




