Na MWANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wapya aliowaapisha kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, ushirikiano na usawa, wakitanguliza mbele maslahi ya taifa.
Ameyasema hayo leo Ikulu,Tunguu Zanzibar, baada ya kuwaapisha Naibu Makatibu Wakuu wawili na kushuhudia viongozi wengine wanne wakila Kiapo cha Uadilifu kwa Viongozi wa Umma.
Pia, ameiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais kuimarisha usimamizi wa masuala ya Muungano na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinatatuliwa kwa ushirikiano, huku akisisitiza umuhimu wa usimamizi wa mazingira na uhifadhi wa rasilimali za taifa.
Aidha, ameitaka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kuboresha usimamizi wa watumishi ili kuongeza ufanisi, huku akiagiza sekta ya uchukuzi kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya reli, barabara, bandari, meli pamoja na kutathmini fursa za kupanua biashara ya anga ya Shirika la Ndege la Tanzania.
Vilevile, ameielekeza Wizara ya Katiba na Sheria kuimarisha upatikanaji wa haki na kampeni za msaada wa kisheria nchini.
Katika hatua nyingine, Rais Dk. Samia ameitaka TANTRADE kuimarisha ukuzaji wa biashara na usimamizi wa maonesho ya biashara, TANAPA kuongeza ulinzi wa hifadhi na rasilimali za utalii, huku TBC ikiagizwa kuendelea kuwa sauti ya taifa kwa kuboresha maudhui na weledi wa watumishi wake.
Walioapishwa ni Dk. Latifa Mohammed Khamis na Prisca Burton Lwangili kama Naibu Makatibu Wakuu, huku Ephraim Balozi Mafuru, Salum Nassor Mnuna, Massana Gibril Mwishawa na Asha Dachi Mbaruk wakila Kiapo cha Uadilifu kwa Viongozi wa Umma.




