Na MWANDISHI WETU
JESHI la Polisi nchini, limetoa onyo kali dhidi ya wanaoendekeza upotoshaji na uzushi wa nyeti za wanaume kutoweka na kuusambaza katika mitandao ya kijamii, ambao umeshasababisha madhara makubwa kwa watu na familia zao.
Limeelekeza kwa yeyote anayejirekodi, anayetengeneza vichekesho kwa kutumia uzushi huo na wanaosambaza nao wasakwe, wakamatwe kwa hatua za kisheria.
Onyo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki kupitia taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime.
Kwa mujibu wa Misime, imani hizo potofu za uzushi na za kusingizia watu wengine mpaka hivi sasa zimesababisha vifo vya watu saba ndani ya siku nne na wengine majeruhi wakiendelea na matibabu hospitalini.
“Jeshi la Polisi linatoa onyo kali dhidi ya wanaoendekeza upotoshaji na uzushi huo na kuusambaza katika mitandao ya kijamii na matokeo yake umeshasababisha madhara makubwa kwa watu na familia zao.
“Maelekezo ya ziada yanatolewa kwa yeyote anayejirekodi, anayetengeneza vichekesho kwa kutumia uzushi huo na wanaosambaza nao wasakwe wakamatwe kwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria ya Makosa ya Mtandaoni na Sheria zingine za nchi,” aliagiza Misime.
Juzi, jeshi hilo lilitoa taarifa ya kukemea tabia potofu iliyozuka hivi karibuni ya kusingizia watu kuwa, wamemgusa mtu fulani begani na matokeo yake aliyeguswa sehemu zake za siri zimetoweka.
Misime alisema tabia hiyo ya uzushi na inayosukumwa na imani za kishirikina, mihemko ya kishabiki na nia ovu ilianzia Tunduma, mkoani Songwe, Aprili Mosi, mwaka huu, kisha jijini Mbeya na Dar es Salaam.
“Pia, juzi (Aprili 4, 2026) ilitokea jijini Dodoma, majira ya mchana na usiku kule mkoani Rukwa na kwa bahati mbaya Mwalimu wa Shule ya Msingi wa mkoani Songwe, Henry Shubati Myuwanga, alisingiziwa amechukuwa sehemu za siri za kijana mmoja muuza duka eneo la Kilyamatundu, Kata ya Laela, baada ya kushindwana bei ya sabuni ambazo mwalimu huyo huwa anauza.
“Baada ya kushindwana bei ndipo kijana huyo kumkomoa kutokana kushindwa kushawishi auziwe kwa bei nafuu, aliamua kumsingizia mwalimu huyo kwa kupiga kelele kuwa, amechukua sehemu zake za siri, ndipo wananchi walijichukulia sheria mikononi na kumshambulia kwa silaha za jadi hadi kumuua, kisha kumchoma moto,” alisema.
Misime alisema Zanzibar pia mkazi wa Mwanza, Said Hussein Said, Mkazi wa Mwanza, akiwa katika daladala alimsingizia abiria mwenzake kuwa, amemgusa begani na matokeo yake nyeti zake zimetoweka, jambo lililowalazimu askari polisi waliokuwa eneo hilo kumwokoa aliyesingiziwa.
Aidha, aliyemsingizia mwenzake alifanyiwa uchunguzi na madaktari na ikaonekana hana tatizo lolote.
Alisema kutokana na kitendo hicho, kijana huyo anashikiliwa kwa mahojiano na uchunguzi zaidi, kubaini wanaofanya uhalifu huo nini kilichopo nyuma yao na malengo yao.
“Imani hizi potofu, za uzushi na za kusingizia watu wengine mpaka hivi sasa zimesabisha vifo vya watu saba ndani ya siku nne na wengine majeruhi wanaendelea na matibabu hospitalini,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Kibaya zaidi pamoja na madhara ambayo yameshashuhudiwa wapo baadhi ya watu wanaoendelea kushabikia na kusambaza upotoshaji huo katika mitandao ya kijamii na wengine wameamua kuutumia kutengeneza vichekesho na kusambaza katika mitandao yao na mingine kwa lengo la kutafuta wafuasi (followers) au kwa malengo mengine wanayofahamu wao.”
Jeshi hilo limeendelea kutoa wito kwa kila mmoja kuendelea kuelimishana kuanzia ngazi ya familia, kuachana na tabia hizo potofu za kishirikina zinazoleta madhara makubwa, yakiwemo mauaji na fedheha kubwa katika karne ya sayansi na teknolojia.




