Na MWANDISHI MAALUMU
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameelekeza fedha zilizokuwa zimepangwa kugharamia maadhimisho ya Sherehe za Muungano mwaka huu, zitumike kukarabati miundombinu ya barabara zilizoharibiwa na mvua inayoendelea kunyesha nchini.
Alisema hayo jijini Dodoma, ofisini kwake Mlimwa, alipouarifu umma kuhusu maadhimisho ya Miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yatakavyofanyika.
“Maadhimisho ya sherehe za miaka 62 ya Muungano, yatafanyika katika ngazi ya mikoa yote nchini, ambapo viongozi wakuu wa Kitaifa, watafanya shughuli za kutembelea, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi ya maendeleo,” alisema.
Aidha, Dk. Mwigulu alisema imeelekezwa kuwa, wakuu wa mikoa watembelee, waweke mawe ya msingi na kuzindua miradi ya maendeleo pamoja kushiriki shughuli za usafi wa mazingira, kupanda miti na kufanya mashindano ya michezo mbalimbali.
“Ninamshukuru Rais Samia kwa kuelekeza fedha ambazo zingetumika kwa kufanya maadhimisho haya kwa gwaride na michezo ya halaiki, zitumike katika shughuli nyingine za maendeleo, ukiwemo ukarabati wa miundombinu ya barabara zilizoharibiwa na mvua inayoendelea kunyesha nchini,” alisema.
Pia, Waziri Mkuu aliagiza majengo yote ya serikali kunakshiwa kwa rangi za Bendera ya Taifa kuanzia jana hadi Aprili 26, mwaka huu, siku ya kilele.
“Majengo yote ya Serikali Tanzania Bara, yapambwe kwa vitambaa vya rangi ya Bendera ya Taifa, picha za waasisi wa Muungano na picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.
Aliongeza kuwa, upande wa Zanzibar, majengo yapambwe kwa vitambaa vya rangi sahihi za Bendera ya Taifa, picha za waasisi wa Muungano na picha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na picha ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
“Nitumie fursa hii kuwahamasisha wananchi wote kushiriki ipasavyo katika shughuli za kijamii, midahalo na makongamano katika kila mkoa, kujadili maendeleo endelevu yaliyofikiwa na nchi yetu kipindi cha miaka 62 ya muungano.
Aidha, ni muhimu Wananchi wote waendelee kuulinda uungano wetu kudumisha umoja, amani na mshikamano wetu,” alihimiza.
Shughuli nyingine zitakazoambatana na maadhimisho hayo ni pamoja na mashindano ya michezo na sanaa mbalimbali, mashindano ya uandishi wa insha kwa shule za msingi na sekondari; mahojiano maalumu na wazee maarufu, midahalo na makongamano kuhusu Muungano na hatua ya maendeleo iliyofikiwa hadi hivi sasa.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni Miaka 62 ya muungano: amani, umoja na mshikamano ni msingi wa maendeleo endelevu.
WADAU WANENA
Wadau wa maendeleo na wanasiasa, waliipongeza serikali kwa uamuzi wake wa kuzielekeza fedha za maadhimisho hayo zitumike kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.
ABDUL KAMBAYA
Mdau wa maendeleo nchini, Abdul Kambaya, alisema huo ni uamuzi mzuri ulifanywa na serikali wa kwenda kujenga barabara nchini.
Alisema inatambulika hivi sasa serikali ipo katika utekelezaji wa barabara nyingi nchini, fedha hizo zitakwenda kujenga miundombinu hiyo.
“Naipongeza serikali kwa hatua hiyo ya kuchukua fedha za sherehe za Muungano na kwenda kutekeleza miradi ya kimaendeleo kama ujenzi wa barabara nchini,”alisema.
Alisema ni wazi inaonekana kuwa, Rais Dk. Samia ni kiongozi anayeendeleza yale yalioachwa na Hayati Rais Dk. John Magufuli na kuanzisha mengine ambayo yana manufaa kwa taifa.
“Tunaona wazi Rais Dk. Samia anavyofanya kazi zake katika uongozi wenye maono kwa sababu, ameendeleza miradi mingi ambayo ina manufaa kwa taifa letu ikiwemo Bwawa la Mwalimu Nyerere na ujenzi wa madarasa kwa shule za msingi na sekondari,”alisema.
HASSAN DOYO
Aliyekuwa mgombea Urais wa Chama cha NLD, Hassan Doyo, alisema serikali inatekeleza yale mambo yenye manufaa kwa taifa.
“Nakumbuka Hayati Rais Dk. John Magufuli, alishawahi kuelekeza fedha za sikukuu ya Muungano zijenge kipande cha barabara ya Bagamoyo kutoka Morocco hadi Mwenge na ilifanyika hivyo na Watanzania tunapenda maendeleo kama hayo,”alisema.




