Na MWANDISHI WETU
TIMU ya soka ya Simba imeendeleza kasi ya ushindi katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu baada ya jana kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Namungo.
Wekundu hao wa Msimbazi walipata ushindi huo ugenini katika Uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa mkoani Lindi.
Katika mtanange huo, mabao ya Simba yaliwekwa kimiani na Libasse Gueye, Anicet Oura na Ellie Mpanzu wakati bao la Namungo likifungwa na Eliuter Makambo.
Ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa Simba katika Ligi Kuu Bara baada ya wiki iliyopita kuifunga Fountain Gate mabao 3-0 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Katika mtanange wa jana, kikosi hicho cha Kocha Steve Barker, kilimaliza kipindi cha kwanza kikiongoza kwa mabao 2-1.
Gueye alikuwa wa kwanza kuifungia Simba katika dakika ya 12 kabla ya Oura kuongeza bao la pili dakika ya 22.
Hata hivyo, dakika 12 baadaye, Namungo ilipata bao la kwanza kupitia kwa Makambo aliyefunga kwa penalti, kufuatia kiungo wa Simba, Yusuph Kagoma kushika mpira ndani ya eneo la hatari.
Kipindi cha pili, Mpanzu aliyeingia akitoka Selemani Mwalimu, alikamilisha karamu ya mabao kwa shuti la mguu wa kushoto.
Kufuatia ushindi huo, Simba inaendelea kusalia nafasi ya pili kwa pointi 42 baada ya kushuka dimbani mara 19, ikiwa chini ya kinara Yanga yenye pointi 47 katika mechi 19.
Namungo FC: Mussa Malika, Bakari Hussein, Machela Julius, Hamisi Halifa, Hamisi Mgunya, Rodgers Gabriel/Cyprian John, Hashimu Manyanya, Heritier Makambo/Fabrice Ngoy, Abdulkarim Kiswanya na Jacob Masawe.
Simba:Mohamadou Kassali, Shomari Kapombe, Libasse Gueye, Yusuph Kagoma, Selemani Mwalimu/Elie Mpanzu, Anicet Oura, Inno Loemba/Neo Maema, Rushine De Rueck, Ismael Toure, Anthony Mligo na Clatous Chama.



