Na MWANDISHI WETU
WATOTO 160 wamepatikana kupitia upandikizaji mimba unaofanywa katika Kituo cha Kairuki Green IVF (KGIVF), kilichoko Bunju ‘A’ jijini Dar es Salaam, tangu kuanzishwa kwake miaka mitatu iliyopita.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa kituo hicho, Dk. Clementina Kairuki, alipozungumzia Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya IVF ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo Julai 25.
Dk. Clementina alisema hayo alipoeleza namna kituo hicho kinavyofanya shughuli za upandikizaji mimba na kusaidia familia zenye changamoto ya uzazi.
Alisema Julai 25 ya kila mwaka imepangwa kuwa siku ya IVF duniani, kwa sababu mtoto wa kwanza alipatikana kwa njia ya upandikizaji mimba ambaye hivi sasa amefikisha miaka 47.
“Tunawapongeza watu waliogundua hii IVF kwa sababu haikuwa rahisi kwani waligundua baada ya kujaribu mara karibu mara 103 ndipo wakafanikiwa mtoto wa kwanza akazaliwa, hata magazeti ya wakati ule Uingereza yanaonesha habari zote ziliandika tukio hilo,” alisema.
Alisema tangu kuzaliwa kwa mtoto huyo wa kwanza, teknolojia ya upandikizaji mimba imeongezeka siku hadi siku na inafanyika kwa njia za kisasa zaidi kuliko ilivyokuwa zamani.
“Mpaka kufikia Julai 23, mwaka huu tulikuwa na watoto 158, jana (juzi) wamezaliwa wawili katika Hospitali ya Kairuki Mikocheni, hivyo wamefika 160. Tunashukuru uelewa wa wananchi kuhusu upandikizaji mimba unaendelea kukua siku hadi siku na tunatoa elimu,” alisema.
Alisema watoto waliozaliwa kwa njia ya upandikizaji baada ya kuanza kituo hicho, wameanza shule na wazazi wao wanatoa ushuhuda namna wanavyofanya vizuri shuleni.
“Nimefanya kazi katika fani hii kwa zaidi ya miaka 24 kwa hiyo nina uzoefu mkubwa wa kutosha, nina furaha kubwa kuona wanawake ambao awali ilishindikana kuwapa huduma hii, hivi sasa kutokana na teknolojia kukua, tunawapa huduma na wakapata watoto,” alisema.
Alisema huduma hiyo katika miaka iliyopita, watu walilazimika kuifuata nje ya nchi kwa gharama kubwa, lakini kutokana na kuanzishwa kwa KGIVF, watu hivi sasa hawana haja ya kupanda ndege kwenda nje ya nchi, kwa sababu wanahudumiwa nchini.
“Kituo chetu kimepata ithibati ya kimataifa ya ubora kwa sababu kinatoa huduma bora ambazo zingepatikana katika mataifa makubwa yaliyoendelea kwa gharama kubwa, hivi sasa wakija hapa kwetu wanapata huduma hizo,” alisema.
Kwa upande wake, Muuguzi Mbobezi wa KGIVF, Khadija Seif, alisema hivi karibuni alihudhuria kongamano la upandikizaji mimba London, Uingereza ambako alijifunza mambo mengi kuhusu teknolojia ya kisasa ya shughuli hiyo.




