Na MWANDISHI WETU
WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa uboreshaji mkubwa uliofanyika katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwake.
Pia, wamempongeza Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, Yusuph Mwenda, kwa kuifanya TRA kuwa rafiki kwa wafanyabiashara na kukusanya kodi kistaarabu hali ambayo imeongeza mapato.
Walitoa pongezi hizo jijini Dodoma kwa nyakati tofauti, walipochangia bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2026/20227 na katika mahojiano maalumu.
SAASHISHA MAFUWE
Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe, aliipongeza TRA kwa hatua ilizochukua ambazo zimechangia kuleta utulivu na kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara nchini.
Alisema uboreshaji unaofanywa na TRA, umeongeza uelewano kati ya mamlaka na wafanyabiashara, jambo linalowapa fursa ya kutekeleza shughuli zao katika mazingira yenye utulivu na kujiamini.
Mafuwe, alisema TRA imeendelea kuonesha dhamira ya kujenga ushirikiano na walipakodi kwa kusikiliza maoni yao, kuboresha utoaji wa huduma na kuweka mifumo inayorahisisha utekelezaji wa majukumu ya kodi.
Mbunge huyo, alieleza kuwa, hatua hizo, zimeongeza imani ya wafanyabiashara kwa mamlaka na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara, kuendelea kushirikiana na TRA kwa kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiyari na kwa wakati.
Alisema kuwa, mapato ya kodi ndiyo msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi.
JOSEPH KASHEKU
Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku ‘Musukuma’, alimpongeza Mwenda kwa utendaji kazi uliotukuka ambao umeifanya mamlaka hiyo kuwa rafiki na wafanyabiashara.
“Huyu Kamishna Mkuu wa TRA ni mtu mstaarabu, apewe maua yake, zamani wakati wa bajeti kama hii, wafanyabiashara wangekuwa hapa bungeni kushawishi mambo yao yaende, leo tunajadili bajeti bila kuichokonoa TRA, kwa kweli wanakusanya pesa za kutosha bila kuumiza wafanyabiashara wanastahili pongezi,” alisema
HAMIS TABASAMU
Mbunge wa Sengerema (CCM), Hamis Tabasamu alisema mamlaka hiyo imepata Kamishna Mkuu muungwana sana, ambaye amefanya mabadiliko makubwa ndani yake na kuifanya kuwa na ufanisi mkubwa.
“Huyu Kamishna wa TRA ni muungwana sana kodi leo hii inakusanywa kiungwana sana, zamani ilikuwa mfanyabiashara ukitoka nje unakutana na askari kama 10 na mitutu ya bunduki, lakini leo hii tunalipa kodi kiungwana, haya ni mafanikio makubwa sana lazima tupongeze,” alisema
“Waziri wa Fedha pamoja na kupongeza mamlaka hii, tunaomba maslahi ya watumishi wake yaangaliwe na walindwe na maana wanafanya kazi kubwa kwa nchi,” alisema.
ADO SHAIBU
Mbunge wa Tunduru Kaskazini, (ACT Wazalendo), Ado Shaibu, alisema TRA imefanya uboreshaji mkubwa ambao umewafanya wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiyari na kuachana na mtindo wa zamani.
“Nafurahia kuona kodi inakusanywa kirafiki na hali hii ikiendelea, itasaidia kuwafanya wafanyabiashara kuona umuhimu wa kulipa kodi kwa hiyari na kwa mtindo huu serikali itakusanya fedha mapato mengi,” alisema
ERICK SHIGONGO
Mbunge wa Buchosa (CCM), Erick Shigongo, alisema katika miaka 30 ya mamlaka hiyo, ameshuhudia makusanyo yakiongezeka mwaka hadi mwaka na kuvunja rekodi za ukusanyaji wa mapato.
“TRA imevunja rekodi kwa miaka 11 mfululizo kwa hiyo nawaambia Watanzania kuwa kazi kubwa sana inafanywa na TRA na napenda kuwaambia chini ya Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo, waendelee kukusanya kodi kwani ndiyo msingi wa maendeleo tunayoyaona,” alisema.
ESTHER MATIKO
Mbunge wa Tarime Mjini (CCM), Esther Matiko, alisema mamlaka hiyo imekuwa ikifanya vizuri kila mwaka kwa kuvuka malengo yake ya ukusanyaji kodi.
“Tumeshuhudia wakiweka malengo na kuyavuka na inatokana na utoaji wa elimu kwa wananchi ambao wamekuwa wakiendelea kulipa kodi kwa hiyari yao tofauti na miaka ya nyuma,” alisema Matiko
SARAH MSAFIRI
Mbunge wa Mvomero (CCM), Sarah Msafiri, aliipongeza TRA kwa kazi kubwa ya kukusanya mapato waliyoifanya miaka 30 tangu kuanzishwa kwake
Alisema mafanikio makubwa yanayoonekana kwenye sekta mbalimbali kama nishati, elimu, kilimo, afya, miradi mikubwa ya kimkakati kama Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere ni kutokana na kodi zinazokusanywa na TRA.
“Kwa hiyo tunapolipa kodi ndipo tunaboresha huduma za kijamii, nawapongeza TRA wamejitahidi kutoa elimu kubwa ya kodi kwa umma, huduma za kijamii zikiboreshwa hata gharama za maisha zinapungua,” alisema.
“Kwa miaka yote 30 TRA wamekuwa wakivunja rekodi wanayojiwekea katika makusanyo na ndani ya miezi 11 iliyopita wamevunja rekodi kwa makusanyo makubwa nawapongeza,” alisema
DK. YAHAYA NAWANDA
Mbunge wa Newala Vijijini (CCM), Dk. Yahaya Nawanda, alisema TRA ndiyo roho ya nchi, serikali inategemea makusanyo kutoka kwa mamlaka hiyo kukamilisha miradi ya maendeleo.




