Na HANIFA RAMADHANI,
Zanzibar
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuanzisha kituo maalumu cha utoaji huduma za kitabibu kwa watu wenye ulemavu.
Hatua hiyo ni dhamira yake ya kuhakikisha kundi hilo, linapata huduma bora za afya na haki sawa katika jamii.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo, wakati akizungumza na kundi la watu wenye ulemavu, ukiwa ni mwendelezo wa kampeni zake za kukutana na makundi mbalimbali, Kikwajuni, Mjini Unguja.
Alisema anatambua kuwa, watu wenye ulemavu, wanahitaji kituo au sehemu maalumu ya kupata matibabu yao, akasisitiza serikali imelifikiria kazi jambo hilo, litatekelezwa.
“Tutaweza kuanzisha kituo maalumu cha utoaji huduma za watu wenye ulemavu kwa vitu vingi ambavyo wanavihitaji, waweze kuvipata sehemu moja,” alisema.
Alisema kitengo muhimu katika utoaji huduma za watu wenye ulemavu ni kitengo cha tiba ya mazoezi ya viungo ‘physiotherapy’.
Alisema hiyo ni sehemu muhimu katika kusaidia kundi hilo, kurejea katika hali bora ya afya na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Alibainisha kuwa, hatua hiyo inalenga kuboresha huduma za afya na ustawi wa kundi hilo muhimu katika jamii.
Dk. Mwinyi, alisema serikali itahakikisha huduma hizo, zinatolewa katika viwango vya juu na kuendelea kutekeleza sera na mipango inayolenga kuimarisha usawa na fursa kwa watu wote.
UWEZESHAJI KWA WENYE ULEMAVU.
Alisema anatambua kuwa, wenye ulemavu wana mahitaji matatu katika uwezeshaji ambayo ni mafunzo ya ujasiriamali, mazingira mazuri ya kufanyia shughuli na kupatiwa mikopo isiyo na riba.
Alisema hayo yote, serikali yake katika awamu iliyopita imeshayaanza na kuahidi kuyaendeleza katika awamu ijayo kwa nguvu kubwa Zaidi.
Pia, alisema atahakikisha kuwa, mafunzo yanatolewa kwa watu wenye ulamavu ambao ni wajasiriamali waweze kuendesha vizuri shughuli zao.
Vilevile alisema wataendelea kuweka mazingira bora, wajasiriamali wote hususan wenye ulamevu, wapate maeneo ya kufanyia shughuli zao kila eneo lililotengwa.
Kuhusu suala la mitaji, Dk. Mwinyi, alisema serikali inaendelea kutoa mikopo ambapo ipo isiyo na riba, inayozingatia kundi hilo.
Aliahidi kuendelea kuwapatia mikopo hiyo na kuhakikisha kundi kubwa la watu wenye ulemavu, linapata mikopo hiyo.
AJIRA KWA WENYE ULEMAVU
Katika eneo la ajira, alisema katika serikali kuna sera ambayo ina mazingatio maalumu kwa watu wa kundi hilo kupatiwa ajira.
Hivyo, alisema katika vyombo vya utungaji sheria, atahakikisha kuwa kuna idadi nzuri ya watu wenye ulemavu.
Alisema watazingatia suala la ajira kwa watu wenye ulemavu kama ilivyo kwa wengine.
Aidha, alisema hata katika nafasi za uongozi, atahakikisha kundi hilo linakuwa kubwa zaidi.
Dk. Mwinyi, alibainisha kuwa, serikali yake itaendelea kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu katika vyuo vya amali.
Aliahidi kuendelea kuweka mkazo wa kuangalia mahitaji maalumu ya wanafunzi wenye ulemavu katika vyuo vya mafunzo ya amali.
KUONDOA USHURU
Kuhusu upatikanaji wa vifaa visaidizi kwa watu wenye ulamvu, Dk. Mwinyi alisema, serikali itaendelea kulisaidia kundi hilo, kupata vifaa hivyo visaidizi bila ya malipo.
Pia, aliahidi kuondoa ushuru kwa wafanyabiashara wanaouza visaidizi vya watu wenye ulemavu ili bei ya visaidizi hivyo ishuke.
Alisema serikali itahakikisha kuwa, kwa kiwango kikubwa, vifaa hivyo vinatolewa kwa watu wenye ulemavu bila malipo yoyote.




