ATHNATH MKIRAMWENI
NA ELIZABETH JOHN
MABALOZI na wanadiplomasia, wamesema hatua ya Umoja wa Mataifa (UN), kuitaja Tanzania kuwa rejea ya amani Afrika na duniani, ni uthibitisho kwamba inakubalika kimataifa.
Juzi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, alisema Tanzania imekuwa rejea muhimu ya amani na mshikamano wa kijamii barani Afrika na duniani kote.
Guterres alisema hayo, baada ya kupokea ujumbe wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, uliowasilishwa kwake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
BALOZI POSI
Akizungumza na UHURU, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Ofisi za Umoja wa Mataifa Geneva, Uswisi, Balozi, Dk. Abdallah Possi, alisema hatua ya Rais Samia kutuma ujumbe maalumu kwa Katibu Mkuu wa UN, ni ishara ya kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu kati ya pande hizo mbili.
Alisema muda mrefu, Tanzania imejijengea jina katika jumuiya ya kimataifa kuwa taifa la amani, lenye misingi imara ya maridhiano na mshikamano wa kitaifa.
“Nchi imekuwa ikiaminiwa kushiriki katika operesheni mbalimbali za kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa, hali iliyoipa heshima na uaminifu mkubwa duniani
“Ujumbe uliowasilishwa, umejikita katika masuala muhimu ya haki za binadamu na amani,”alisema.
Alisema Tanzania kama baadhi ya mataifa mengine, imewahi kupitia vipindi vigumu katika historia yake, lakini imekuwa ikijifunza na kuimarika kutokana na misingi yake ya amani.
Dk. Possi, alisema kitendo cha kuundwa Tume ya Uchunguzi kuchunguza vurugu za Oktoba 29, mwaka huu ni hatua muhimu ya kujenga imani kwa wananchi na jumuiya ya kimataifa.
Pia, alisema Tanzania imeendelea kushiriki kikamilifu katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.
Alisema serikali imeendelea kufanya mazungumzo na wadau wa kimataifa, wakiwemo wawakilishi wa nchi mbalimbali na taasisi za kiraia, kujenga maelewano na uelewa wa pamoja.
Alieleza kuwa, kauli ya Guterres, inathibitisha dhamira ya Tanzania kuendelea kujenga taifa la amani, lenye mshikamano na heshima kwa jumuiya ya kimataifa.
BALOZI MULAMULA
Kwa upande wake, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Afrika, kuhusu Wanawake, Amani na Usalama, Balozi Liberatha Mulamula, alipongeza hatua ya Rais Samia kutuma ujumbe kwa Katibu Mkuu wa UN.
Alisema anaamini maudhui ya ujumbe huo, yalikuwa kumhakikishia Katibu Mkuu wa UN, Tanzania ni salama.
Alieleza kuwa, Guterres alitambua umuhimu wa Tanzania kama nchi ya amani na mfano wa kuigwa.
BALOZI MSTAAFU LIUNDI
Balozi Mstaafu, Christopher Liundi, alisema kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu wa UN ni mtazamo rasmi wa jumuiya hiyo.
Alisema kauli ya Guterres, inaakisi picha halisi ya juhudi zinazofanywa na Tanzania, ambazo zinaendelea kuimarika na kuonesha dhamira ya taifa linalopenda amani.
Aliendelea kusema Tanzania ina utamaduni wa kukaa pamoja, kusikilizana na kufikia mwafaka katika masuala mbalimbali, hatua inayothibitisha misingi ya amani ipo imara na inaendelea kuimarishwa.
MHADHIRI DANINGA
Naye Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi na Uongozi wa Chuo cha Mwalimu Nyerere, Dk. Philip Daninga, alisema Tanznia ni nchi iliyozungukwa na upendo, ndiyo maana amani haiwezi kuvurugika.
MHADHIRI AMANI
Mhadhiri wa Masuala ya Diplomasia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Godwin Amani, alisema utambulisho wa Tanzania katika mataifa mengine duniani, unatokana na amani na mshikamano.
BALOZI HAJI
Kaimu Mwakilishi wa Kudumu Tanzania, Umoja wa Mataifa, Balozi Dk. Suleiman Haji Suleiman, alisema Tanzania na Umoja wa Mataifa, zimezidi kuimarisha uhusiano kufuatia kikao maalumu kati ya ujumbe wa Tanzania na Katibu Mkuu wa UN.
Dk. Suleimani, alisema anaamini Guterres amevutiwa na Tanzania kwa kuwa, inatambulika kimataifa kupitia amani pia, alifurahishwa na taarifa kuwa, hali ya utulivu imerejea nchini baada ya kutokea tukio la Oktoba 29, mwaka huu.
Dk. Suleimani, alisema Guterres alisifu uamuzi wa Rais Samia kuunda Tume ya Uchunguzi chini ya Jaji Othman Chande, ambaye anaheshimika kimataifa na ndani ya Umoja wa Mataifa.
Taarifa iliyotolewa juzi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki, ilisema taswira ya Tanzania ni kielelezo cha amani.




