Na ELIZABETH JOHN
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amesema taifa halijawahi kugawanyika kama inavyodaiwa na baadhi ya watu, bali ni mitazamo tofauti inayojitokeza kutokana na uhuru wa mawazo na demokrasia iliyoimarika.
Akizungumza katika kipindi cha Morning Trumpet kinachorushwa kituo cha televisheni cha UTV, Wasira alisema madai ya kuwepo kwa mgawanyiko ni hoja zinazotokana na mitandao ya kijamii, ambazo mara nyingi hujenga taswira isiyo halisi ya hali ya kisiasa na kijamii nchini.
“Wapo wanaoeneza mitazamo kwamba, taifa limegawanyika, ukweli ni kuwa, Watanzania wameendelea kuwa wamoja. Wanaunganishwa na amani, upendo na malengo ya pamoja ya maendeleo,” alisema.
Alisisitiza kuwa, idadi kubwa ya watu wanaohudhuria mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali nchini ni ushahidi tosha kwamba, Watanzania wanaendelea kuwa wamoja.
Alisema hata wale walio nje ya viwanja, wamekuwa wengi kuliko waliopo ndani, jambo linaloonesha hamasa kubwa ya wananchi kushiriki masuala ya kitaifa.
Aliongeza kuwa, ni haki ya msingi kwa wananchi, kuwa na maoni tofauti kuhusu masuala ya kisiasa au maendeleo, tofauti hizo, haziwezi kuwa, kigezo cha kudhani taifa limegawanyika, kwani kila nchi yenye demokrasia, haiwezi kukosa sauti tofauti.
Wasira, alisema serikali imeendelea kutekeleza kwa vitendo ahadi zake kwa wananchi, ukiwemo uboreshaji wa huduma za kijamii kama elimu, afya, nishati na miundombinu, jambo linaloonesha dhamira ya dhati ya kuhakikisha ustawi wa Watanzania wote.
“Tumefanya mengi, hasa sekta za nishati na elimu. Tuliahidi kumaliza changamoto ya umeme na sasa, Bwawa la Umeme linaendelea kujengwa, jambo litakaloongeza upatikanaji wa nishati nchini,” alisema.
Pia, alisema dhamira ya serikali ni kujenga uchumi jumuishi, unaowagusa Watanzania wote, bila kujali makundi yao, wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, machinga na wajasiriamali wadogo, kuongeza kipato na ajira nchini.
Vilevile, aligusia ajenda ya katiba mpya, akisema bado ipo mezani, itajadiliwa kwa umakini zaidi baada ya uchaguzi, kwa kushirikisha vyama vya siasa na wadau mbalimbali, kuhakikisha matokeo yake yanakubaliwa na wote.
Alisema licha ya changamoto zilizopo, serikali imeendelea kushughulikia masuala ya usalama, maoni ya wananchi na marekebisho ya sheria, kuhakikisha kila Mtanzania, ananufaika na maendeleo ya taifa.
“Matatizo yapo, hakuna nchi isiyo na changamoto, tumeamua kuyashughulikia kwa umakini. Muhimu ni umoja na nia njema ya kujenga taifa letu,” alisema.
Aliwataka wananchi, kuendelea kudumisha amani, mshikamano na kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu, akisema mamlaka yote ya kuongoza nchi, iko mikononi mwa wananchi kama inavyosema Ibara ya nane ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.



