Na SELINA MATHEW, Dodoma
SERIKALI imeainisha hatua ambazo zimechukuliwa kuwezesha nchi kupanda katika masuala ya michezo chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Samia Suluhu Hassan.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni na Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba wakati akijibu swali la papo kwa papo la Mbunge wa Amani Zanzibar, Abdul Yussuf Maalim.
Katika swali lake, mbunge huyo alisema nchi imekuwa na mwendelezo mzuri katika sekta za michezo ambapo timu za taifa na klabu zinafanya vizuri.
Alihoji, nini mkakati wa kudumu serikali kutambua vipaji kuanzia ngazi za chini pamoja na kujenga miundombinu ya kisasa ili kuendana na hadhi ya kimataifa kuanzia ngazi za shule.
Akijibu swali hilo, Dk. Mwigulu alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dk. Samia imechukua hatua nyingi za kuwezesha nchi kupanda kiwango katika masuala ya michezo.
Alitaja hatua hizo ni pamoja na kutenga shule 56 nchi nzima kuwa maalumu kwa ajili ya masuala ya michezo ambapo vijana wataendelea kufundishwa kuanzia ngazi za awali.
Mbali na hilo, alisema serikali imeongeza msisitizo katika mashindano ya vijana wa shule za msingi kupitia UMITASHUMTA na shule za sekondari kupitia UMISSETA na kwamba wameelekeza taasisi za serikali zinazoweza kudhamini mashindano hayo zifanye hivyo ili kuimba nyimbo za uzalendo kuhamasisha.
Kadhalika, alisema serikali imeendelea na ujenzi wa miundombinu ambapo mbali na viwanja vitakavyotumika fainali za Kombe la Taifa Afrika (AFCON 2027), imetenga baadhi ya viwanja vitakavyoboreshwa kwa ajili ya mazoezi ambavyo vipo maeneo mbalimbali nchini.
“Nitoe rai kwa halmashauri zetu kote nchini kuendelea kutunza maeneo ya wazi yanayofaa kwa ajili ya michezo, kumekuwepo na utaratibu wa kila eneo la wazi kuuzwa na hivyo kusababisha vijana, watoto kukosa maeneo ambayo wanaweza kufanya mazoezi na masuala ya michezo.
“Leo tuna baadhi ya wachezaji ambao wanacheza timu ya taifa aina ya Feisal Toto, Dickson Job na Shomari Kapombe ni zao la mazoezi yao waliyoanza katika maeneo ya wazi,
“Nitoe rai halmashauri zetu mipango miji kuhakikisha kwamba kila wanaponga, wasiuze maeneo ya wazi yanayotumiwa na vijana wetu kwa ajili ya mazoezi,” alisema Dk. Mwigulu
Alisema wamekaa na wizara ya kisekta kuangalia uwezekano wa kuwa na mashindano mengi ambayo yatafanya vijana nchini kupata utumamu na kujiandaa kuweza kufanya vizuri zaidi katika michezo.
Kadhalika, aliungana na Rais Dk. Samia kuipongeza Taifa Stars kwa kuweka rekodi ya kucheza katika hatua ya 16 bora AFCON 2025, huku akizitakia kila la kheri klabu ambazo zinaendelea katika mashindano ya kimataifa hatua ya makundi za Simba, Yanga, Singida Black Stars na Azam FC.




