• ePaper
Sunday, November 16, 2025
Subscribe
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
No Result
View All Result
Home Habari

DK. SAMIA AWAONYA WATU WENYE NIA OVU

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
October 21, 2025
in Habari, Kitaifa, Siasa, Uchaguzi
0
DK. SAMIA AWAONYA WATU WENYE NIA OVU

Dk. Samia Suluhu Hassan, Mgombea Urais kupitia CCM CCM,

0
SHARES
4
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na MUSSA YUSUPH

RAIS na Amiri Jeshi Mkuu, Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa onyo kwa watu wenye nia ovu yakutaka kuvuruga amani nchini katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Dk. Samia, amewahakikishia wananchi hakutatokea tishio la usalama wala maandamano katika uchaguzi mkuu, kwani vyombo vya dola, vimejipanga kuimarisha ulinzi na usalama huku akitoa wito kwa wananchi, kujitokeza kwa wingi kupigakura.

Dk. Samia, ametoa msisitizo huo katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika viwanja vya Leaders Club, wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

“Niwahakikishie tarehe 29 mwezi huu wa 10, niwaombe tokeni mwende mkapigekura. Ninayeongea hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa nchi hii.

“Nataka niwaambie, maandamano yatakayokuwepo ni watu kwenda vituoni kupigakura. Hakuna maandamano mengine yatakayokuwepo hapa. Hakuna tishio la kiusalama litakalokuwepo.

“Anayesema hapa ni Amiri Jeshi Mkuu wa nchi. Niwaombe ndugu zangu, twendeni mkapigekura. Baba ukitoka, hakikisha umetoka na familia umekwenda kupigakura,” amesema.

Ametoa wito kwa mabalozi, kuhakikisha wanahamasisha wananchi kwenda kutimiza haki yao ya kidemokrasia ifikapo Oktoba 29, mwaka huu.

“Twendeni tukaheshimishe Chama Cha Mapinduzi. Twendeni tukaiheshimishe Tanzania. Tukapigekura kwa usalama turudi kwa usalama.

“Mengine niachieni mimi. Matusi niachieni mimi nayabeba kwa niaba yenu. Manabii wetu, Bwana Yesu alisurubiwa kwa kukomboa watu kwa amri ya Mungu lakini alikuwa anafanyakazi ya watu.

“Nabii Muhammad alipigwa hadi akatolewa meno kwa kufanyakazi ya kukomboa watu kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Samia Suluhu aliapa kuitumikia Tanzania, ndicho ninachokifanya,” alisisitiza huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliofurika katika viwanja hivyo.

Dk. Samia ambaye pia ni Mgombea Urais kupitia CCM, alisema ameapa kuilinda katiba, kujenga utu wa Mtanzania, kazi ambayo anaendelea kuifanya kwa mafanikio makubwa.

Amesema anapowafikishia wananchi huduma muhimu kama za maji, afya, elimu, umeme na usalama huko ndiko kuheshimisha utu wa Mtanzania.

“Sina uchungu ndugu zangu wa kubeba matusi yote yanayotolewa kwa sababu, nafanyakazi hii. Sina uchungu hata kidogo wala sijutii. 

“Niwaombe sana ndugu zangu, tunawaomba kura. Kama nilivyosisitiza hata kibati cha soda hakitapasuka, twendeni tukapige kura,” ameeleza.

MRADI WA MWENDOKASI

Katika hotuba yake, Dk. Samia, alizungumzia mkakati wa serikali kuimarisha usafiri jijini Dar es Salaam kupitia mradi wa mabasi ya mwendokasi (BRT).

Alisema katika kipindi cha miaka minne, serikali imejenga kilometa 94.9 za miundombinu hiyo na kuwa, jumla ya sh. trilioni 2.1 zimetumika.

Alibainisha kuwa, ujenzi wa awamu zote za mradi wa BRT, serikali inakwenda kukamilisha barabara zote huku ikisimamia uamuzi wa kushirikisha sekta binafsi.

“Tutakapomaliza barabara zote ni fursa muhimu kwa sekta binafsi, kupata kazi ya kubeba abiria na kurudisha.

“Kazi hiyo kwa kiasi kikubwa, hatutaki kuifanya serikali, bali sekta binafsi wataingiza mabasi wafanye uendeshaji wa shughuli hizo.

“Tayari tumeshapata watoa huduma kwenye awamu ya kwanza kampuni ya ENG yenye mabasi 177.

“Awamu ya pili, kampuni ya Mofat yenye mabasi 255 na mabasi ya Mofat tayari yameingia njiani.

“Kampuni ya YG Link yenye mabasi 166, nayo yatakuja kuingia njia zingine zikimalizika na kampuni ya Metro Link City yenye mabasi 334 nayo itaingia kutoa huduma,”alisema.

Dk. Samia, alitoa ahadi kwa wananchi kuanzia Januari, mwakani, wakazi wa Dar es Salaam watashuhudia mageuzi makubwa katika utoaji huduma za miundombinu ya BRT.

Alieleza kuwa, mradi wa mabasi ya mwendokasi kwa hatua iliyofikia, umeuletea sifa Tanzania kimataifa katika uwekezaji ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

“Niwahakikishie wakazi wa Kinondoni, Ubungo na Dar es Salaam kwa ujumla. Kwa mageuzi yaliyofanyika katika uendeshaji, tutalinda sifa hiyo kimataifa na mradi wa BRT utaleta mapinduzi ya usafiri ndani ya jiji,”alisema.

NEEMA KWA WENYE DALADALA

Kuhusu daladala, alisema serikali ipo katika mpango wa kukamilisha ujenzi wa stendi ya daladala Mwenge.

“Kwa ndugu zetu wenye daladala, kipindi hiki tulikamilisha ujenzi wa stendi pale Mwenge kwa wenye daladala.

“Tunapokwenda mbele tunakwenda kufanya ukarabati, kuziboresha stendi za daladala za Kawe, Bunju B na Tegeta Nyuki,”alisema.

Alisema hatua hiyo, itaziwezesha daladala kuwa na maeneo maalumu ya kutoa huduma.

MIGIRO ATAJA SIFA ZA DK. SAMIA

Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Asha- Rose Migiro, alisema Dk. Samia ni kiongozi mwenye maono, aliyeleta nguvu na kasi mpya katika ukuaji uchumi wa taifa.

“Chini ya uongozi wake, tumeona maboresho ya bandari, tumeona maboresho ya miundombinu mbalimbali. Tumeona akizungumzia programu mbalimbali za uwezeshaji wanachi kiuchumi.

MWIGULU AFUNGUKA

Mgombea Ubunge Jimbo la Iramba na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema wakati Dk. Samia anaingia madarakani, taifa lilikuwa na miradi mikubwa ambayo hata majirani walihofu utekelezaji wake.

Hata hivyo, alisema Dk. Samia amekamilisha miradi hiyo ikiwemo ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, reli ya SGR na madaraja.

Alisema Dk. Samia amesimamia uchumi wa Tanzania ili mfumuko wa bei usiwaumize Watanzania ambapo alianza kutoa ruzuku kwa maeneo mbalimbali.

Alitaja miongoni mwa ruzuku hizo ni sh. bilioni 100 katika mafuta ya petroli, kupunguza tozo katika mafuta ya kupikia na ruzuku ya mbolea.

WENJE APIGILIA MSUMARI

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje, alisema mamlaka ya nchi hayapatikani kwa kukimbia uchaguzi, kwani hakuna nchi duniani ambayo mfumo wake wa uchaguzi upo vizuri kwa asilimia 100.

Alibainisha kuwa, licha ya nia nzuri ya serikali kuanzisha mchakato wa katiba mpya, bado vipo vyama vya siasa ambavyo vitasusia mchakato huo.

“Mimi nilikuwa mjumbe wa kamati kuu ya CHADEMA kwa zaidi ya miaka 10. Wapo watu wanaandika katika mitandao kwamba, CHADEMA imezuiwa na serikali kushiriki uchaguzi,” alisisitiza.

Alisema CHADEMA kupitia vikao vya kamati kuu, ndiyo iliamua kutoshiriki uchaguzi huo na kukataa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi mkuu.

Wenje alisema zipo sababu za ndani zilizokifanya chama hicho kutosaini kanuni hizo na kukataa kushiriki uchaguzi hivyo ipo siku ataziweka hadharani.

“Hakuna serikali iliyowazuia kushiriki uchaguzi. Mimi nilikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA zipo sababu za ndani zilizokifanya chama changu kukataa kushiriki uchaguzi na siku wakiletapang’ang’a nitaziweka hadharani,” alisisitiza.

UJENZI DARAJA LA JANGWANI

Mgombea Ubunge Jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega, alisema zaidi ya sh. bilioni 93, zimetolewa kujenga Daraja la Jangwani litakalokuwa na urefu wa mita 400 sawa na viwanja vinne vya mpira wa miguu.

Alieleza kuwa, Dk. Samia amedhamiria kuondoa msongamano wa magari kwa kujenga barabara za juu eneo la Mwenge, Morocco na Magomeni.

Ulega ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, alisema ujenzi wa barabara hizo, upo hatua za mwisho huku, akisema awamu ya sita ya mradi wa mwendokasi, utafanyika kutoka Tegeta hadi Bunju.

MKAKATI KUKOMESHA UHABA WA MAJI

Mgombea Ubunge Jimbo la Pangani na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alisema Dk. Samia ametoa sh. bilioni 21 kutoa maji katika visima vya Kimbiji kuja Jiji la Dar es Salaam kuimarisha upatikanaji huduma hiyo.

Alieleza kuwa, sh. trilioni moja zimetolewa katika jiji hilo kuboresha upatikanaji maji ambapo sh. bilioni 600 zitatumika kwa upande wa maji safi na sh. bilioni 400 zitatumika kuboresha miundombinu ya maji taka.

Kuhusu changamoto ya Kibamba na Ubungo kupata maji, alisema baada ya Dk. Samia kutoa maelekezo kwa kutoa sh. bilioni 5.2 limejengwa tenki la maji lenye ujazo wa lita milioni sita.

Alisema mkakati huo utahusisha na uboreshaji huduma ya maji kwani mkakati ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma hiyo.

WAGOMBEA UBUNGE

Kwa upande wake, Mgombea Ubunge Jimbo la Kibamba, Angela Kairuki, alieleza kuwa, Dk. Samia ni kiongozi mwenye kujali wananchi.

Alisema Dk. Samia amekuwa akisisitiza watendaji na viongozi serikalini kumfikiria mwananchi katika kila sekta.

Angela ambaye pia ni Mshauri wa Rais katika masuala ya wanawake na matumizi ya nishati safi, alisema jimbo hilo katika afya zimetolewa sh. bilioni 3.4 kutekeleza miradi.

Pia, alisema katika barabara zaidi ya sh. bilioni 200 zimetolewa huku sh. bilioni 1.7 zimetumika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.

Mgombea Ubunge Jimbo la Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo, alisema ilani ya CCM yenye vipaumbele tisa na ahadi zaidi ya 200 inatekelezeka vyema.

Alibainisha kuwa, katika kipindi cha uongozi wa Dk. Samia, jimbo hilo limenufaika kutimiza kipaumbele cha ujenzi wa barabara za mitaani.

Alisema jimbo hilo lenye kata nane na mitaa 46 lina mtandao wa barabara za lami zaidi ya kilometa 100 ambapo barabara za lami zilikuwa kilometa 32.7.

Profesa Kitila, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, alibainisha kuwa baada ya Dk. Samia kushika madaraka barabara za mtandao wa lami ndani ya jimbo hilo zimefikia kilometa 78.9 sawa na ongezeko la asilimia 46.8.

“Uliidhinisha mradi muhimu wa DMDP kwenda Wilaya ya Ubungo awali haukuwepo Kigamboni na Ubungo. Matokeo yake tumepata kilometa 25.1 zikiwemo barabara 12 Kata ya Sinza, barabara mbili kata za Manzese na Makulumla na barabara tatu Kata ya Kimara.

“Tunayo barabara korofi ya Kimara – Bonyokwa – Kinyerezi inayounganisha Ubungo na Ilala, hatimaye mwaka jana uliruhusu zikatoka fedha na mkandarasi ameanza kazi,” alisisitiza.

Mgombea Ubunge Jimbo la Kinondoni, Abass Tarimba, alieleza kuwa asilimia 65 ya maeneo ya jimbo hilo yamepitiwa na mito.

Alieleza kuwa, katika jimbo hilo Mto Ng’ombe ulisababisha kadhia kwa wananchi hususan kipindi cha mvua, hata hivyo baada ya ujenzi wa kingo za mto changamoto ya mafuriko imeondoka.

Kuhusu changamoto ya Mto Mzimbazi, alisema zaidi ya sh. trilioni moja zimetolewa kuondoa adha hiyo ikiwemo ujenzi wa daraja la Jangwani.

Pia, alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo jimbo hilo litajengwa barabara za jui tatu Magomeni, Mwenge na Morocco.

Aliwasilisha ombi kurasimishwa kwa makazi ambayo yalikuwa katika maeneo yasiyopimwa kwani serikali imeshadhibiti hali ya mafuriko.

Mgombea Ubunge Viti Maalumu, Ummy Nderiyananga, alibainisha kuwa, Oktoba 29 mwaka huu wenye ulemavu watampigia kura Dk. Samia katika uchaguzi mkuu.

Alisema Dk. Samia alipoingia madarakani alikuta vyama vya wenye ulemavu vikiwa havina fedha, alitoa sh. bilioni mbili pamoja na ofisi za vyama hivyo.

“Kule Dodoma umetoa fedha zako sh. milioni 36.7, umetununulia kiwanja. CCM ndiyo chama cha kwanza chenye mfano Afrika kutengeneza Ilani yenye kukidhi mahitaji ya wenyeulemavu.

“Kwa wale wenye changamoto ya kuona umetoa ilani yenye nukta nundu, kwa wenye ualbino umetoa ilani yenye maandishi makubwa. Umekuwa wa mfano Afrika kwa kuanzisha programu ya wenyeulemavu kusoma nyumbani ambapo watoto zaidi ya 600 wanasoma,” alisisitiza.

Ummy ambaye pia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, alisema katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, Dk. Samia amejenga mabweni mawili kwa wanafunzi wenye ulemavu.

Kwa upande wake, Mgombea Ubunge Jimbo la Kawe, Godfrey Thimos, alisema jimbo hilo, limenufaika kupitia ujenzi wa hospitali ya wilaya Kinondoni ambayo imejengwa Mabwepande hatua ambayo imerahisisha huduma kwa wananchi wa jimbo hilo.

Vilevile, alisema wamenufaika kupitia ujenzi wa vituo viwili vya afya huku upande wa elimu zimejengwa shule mpya nne na madarasa 84 katika shule mbalimbali.

“Ulitupa sh. bilioni 2.1 ambazo tumezitumia kununua mitambo ya ukarabati wa barabara hatua ambayo imesaidia kuboresha barabara za jimbo hilo,” alisisitiza.

Previous Post

DK. NCHIMBI : TUTAKAMILISHA BANDARI YA UVUVI KILWA

Next Post

DK. NCHIMBI AAHIDI HUDUMA ZA AFYA KWA WATANZANIA

Next Post
DK. NCHIMBI AAHIDI HUDUMA ZA AFYA KWA WATANZANIA

DK. NCHIMBI AAHIDI HUDUMA ZA AFYA KWA WATANZANIA

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

DK. SAMIA AAHIDI MKAKATI WA NGANO

DK. SAMIA AAHIDI MKAKATI WA NGANO

1 month ago
WASIRA AONYA WANAOTOLEA MACHO UMEYA

WASIRA AONYA WANAOTOLEA MACHO UMEYA

2 months ago

Popular News

  • YANGA, SIMBA KAZI KAZI

    YANGA, SIMBA KAZI KAZI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • KETE YA KWANZA KWA GAMONDI STARS LEO

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • TRA YAHAWAHAKIKISHIA WAFANYABIASHARA WA KARIAKOO USALAMA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • MAAGIZO MATATU KWA DK. NCHEMBA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • NI MARIDHIANO

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
error: Content is protected !!
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2025 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.