Na MUSSA YUSUPH
ZIKIWA zimebaki siku tatu kwa Watanzania kuingia katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuvutia maelfu ya wananchi kupitia ahadi zake katika mikutano ya kampeni.
Katika mikutano yake, ahadi za Dk. Samia, zimeyagusa makundi mbalimbali ndani ya jamii huku msisitizo mkubwa ni katika kujenga uchumi jumuishi.
Miongoni mwa makundi hayo ni wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini na kuwa, Dk. Samia, kupitia mikutano yake ametilia mkazo lengo la serikali yake ni kugusa maisha ya Mtanzania kuanzia maeneo ya vijijini.
Msisitizo huo, unathibitishwa na ahadi ambazo Dk. Samia, amezitoa kwa wananchi zenye kuwagusa moja kwa moja wananchi wa vijijini, hatua ambayo itachochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi hao.
RUZUKU NA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA KILIMO
Moja ya eneo ambalo Dk. Samia amelitilia mkazo ni matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kilimo.
Katika mikutano yake, Dk. Samia alisema miaka mitano ijayo, serikali itajikita kuleta mapinduzi katika matumizi ya teknolojia sekta ya kilimo.
Alisema mkakati huo, utajikita katika kuongeza uzalishaji mazao, upatikanaji masoko, maabara za utafiti, kuimarisha mawasiliano na taarifa za hali ya hewa.
“Vilevile miaka mitano ijayo tunataka kuchukua hatua za makusudi kudumisha mila, tamaduni na desturi zetu siyo zile zenye madhara.
“Tutaongeza matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo akili unde (AI) kuimarisha ufanisi katika uzalishaji na utoaji huduma ikiwemo kilimo.
“Katika kilimo tumeanza kwa kufanya tafiti kwa njia za kisasa ambazo ni tafiti za mbegu, udongo na tafiti mbalimbali katika kilimo ambazo tunazifanya kwa kutumia teknolojia ya kisasa,”alisema.
Dk. Samia alisema Julai, mwaka huu alipata fursa kufungua maabara kubwa ya kitaalamu mkoani Dodoma ambayo itafanyakazi za tafiti katika kilimo.
Pia, alisema mwaka jana, alifungua maabara katika Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) itakayotumika kuwafundisha vijana namna ya kuzalisha mazao kitaalamu kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
“Katika masuala ya vipimo tumeanza kuona katika uzalishaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa ambapo wale wanaokwenda kuuza mazao NFRA (Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula) wakifika pale ni teknolojia inayotumika kutoa unyevu wa mahindi na mizani za kisasa kujua uzito.
“Hapo hapo mkulima anapata risiti yake kwa mashine na anapokea meseji katika simu yake kwamba umeleta mzigo fulani, unyevu upo kiasi fulani na gredi ya mazao yako kiasi fulani hivyo fedha zako kwa bei ni kiasi fulani,” aliwaeleza wananchi.
Pia, alisema matumizi ya teknolojia yatatumika kuimarisha mawasiliano na ufuatiliaji hali ya hewa.
Mbali na matumizi ya teknolojia, Dk. Samia aliendelea kusisitiza serikali itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea na pembejeo kwa wakulima nchini.
UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
Tangu Rais Dk. Samia alipoingia madarakani mwaka 2021, thamani ya mikopo kwa wajasiriamali imeongezeka kutoka sh. trilioni saba hadi kufikia sh. trilioni 14 mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la asilimia zaidi ya 100.
Hatua hiyo, inadhihirisha dhamira yake ya kuunga mkono sekta hiyo muhimu katika uchumi wa taifa ambayo inagusa maisha ya wananchi ambao wengi wamejiajiri kupitia shughuli mbalimbali za ujasiriamali.
Dk. Samia katika mikutano yake ya kampeni, aliahidi kutenga sh. bilioni 200 za mikopo ya wajasiriamali wadogo ikiwa ni sehemu ya mfuko maalumu wa mikopo nafuu lengo ni kuboresha biashara zao na kujikwamua kutoka katika umaskini.
Hata hivyo, Serikali ya Dk. Samia kupitia mfuko wa SELF (Self Microfinance Fund) imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 196.9 kuanzia mwaka 2021 hadi Juni 30, mwaka huu.
Wanufaika ni wajasiriamali 183,381 wakiwemo wanawake 97,000 na taasisi 549 za kifedha. Mikopo hiyo imewasaidia wajasiriamali kupata ajira 183,000 na kufikia malengo ya maendeleo yao.
Eneo lingine ni mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri za Wilaya inayotolewa kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu ambapo kwa mwaka jana serikali ilitenga sh. bilioni 227 kupitia halmashauri nchini kutoa mikopo hiyo.
HUDUMA ZA AFYA
Upatikanaji huduma bora za afya ni jambo muhimu katika jamii kwani kukosekana kwa huduma hiyo ni hatari kwa maisha ya wananchi, hivyo kudumaza maendeleo ya taifa.
Ili kuwaondolea wanawake mzigo huo, Dk. Samia katika kampeni zake, aliahidi kuendeleza kasi ya ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, hospitali na kuongeza wigo wa ajira kwa watumishi wa kada hiyo.
Katika kutekeleza hatua za haraka, Dk. Samia aliahidi ndani ya siku 100 za mwanzo pindi atakapochaguliwa kuliongoza Taifa, atatoa ajira kwa wahudumu wa afya 5,000.
Vilevile, alisema serikali yake itagharamia huduma za matibabu maalumu na vipimo vya magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, magonjwa ya moyo, figo, mifupa, mishipa ya fahamu kwa wananchi wasiokuwa na uwezo.
Pia, alisema serikali itazindua awamu ya majaribio mpango wa Bima ya Afya kwa Wote utakaoanza na makundi ya watoto, wazee, wajawazito na wenye ulemavu ambapo gharama zao za matibabu zitabebwa kupitia mfuko huo.
MATUMIZI YA NISHATI SAFI
Dk. Samia ameonesha uongozi thabiti barani Afrika katika kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia akilenga kuboresha afya za wananchi na kulinda mazingira.
Aliahidi kuwa, ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia huku akihamasisha ubunifu katika teknolojia na kuhamasisha wadau kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya nishati hiyo.
Miongoni mwa miradi hiyo ni usambazaji umeme katika vitongoji mbalimbali nchini kwa lengo la kuwezesha huduma hiyo kumfikia kila mwananchi ili aweze kutumia nishati ya umeme badala ya kuni.
Tayari Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea kugawa majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku katika mikoa mbalimbali ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia.
Dk. Samia alisisitiza kuwa matumizi ya nishati zisizo salama ya kupikia yanachangia vifo vya mapema hasa kwa wanawake na Watoto, hivyo matumizi ya nishati safi yanalenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ili kuhifadhi mazingira na kupunguza ukataji wa miti.
UBORESHAJI VIWANDA
Eneo lingine ni sekta ya viwanda ambapo Rais Dk. Samia alitangaza kufanya mabadiliko makubwa pindi atakapopewa ridhaa ya kuliongoza taifa, yatakayogusa mashamba na viwanda vilivyobinafsishwa.
Mashamba na viwanda ambavyo vitaguswa ni ya chai na mkonge ambayo yamebinafsishwa na wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza.
Katika kuthibitisha hilo, Dk. Samia alitoa maagizo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Katiba na Sheria, kupitia upya mikataba ya ubinafsishaji maeneo hayo na ile itakayobainika kukiukwa itavunjwa.
Alisema lengo la hatua hiyo ni kuiwezesha serikali na vyama vya ushirika kuyaendeleza mashamba na viwanda hivyo ili viongeze tija ya uzalishaji mazao kwa wakulima.
“Katika miaka mitano ijayo tutahakikisha viwanda vilivyobinafsishwa lakini havifanyikazi vinapatiwa wawekezaji wengine na kukabidhiwa kwa ushirika chini ya usimamizi wa serikali.




