Na MUSSA YUSUPH,
Mwanza
SHAMRASHAMRA za maandalizi ya mkutano wa kufunga kampeni za Uchaguzi Mkuu, zimeendelea kuutikisa Mkoa wa Mwanza ambapo Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuhutubia maelfu ya wananchi, wapenzi, wanachama na wakereketwa wa CCM.
Katika mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu, katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa, sehemu kubwa ya maandalizi, yamekamilika huku wananchi wa jiji hilo wakiwa wenye shauku kushuhudia mkutano huo ambao unatarajiwa kuvunja rekodi ya mahudhurio ya maelfu ya wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Katibu CCM Mkoa wa Mwanza, Omary Mtuwa, alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi.
“Tunawakaribisha wananchi wote, wanachama wetu na wasiokuwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kujitokeza uwanjani.
“CCM imechagua kufungia kampeni mkoani Mwanza kufuatia wingi wa wapiga kura waliopo Kanda ya Ziwa, ambao ni takribani asilimia 38 ya wapiga kura wote nchini, huku Mwanza pekee ikikadiriwa kuwa na wapiga kura takribani milioni mbili,” alieleza.
Mtuwa alisema CCM wakati wote wa mikutano ya kampeni iliyofanyika mkoani Mwanza, imefanikiwa kuwafikia idadi kubwa ya wapigakura.
Kwa sababu hiyo, alisema Chama kinatarajiwa kuibuka na ushindi wa kihistoria kuwa sababu ya kupata mwitikio mkubwa wa kuungwa mkono na wananchi wa mkoa huo wenye idadi kubwa ya wapigakura.
MSISITIZO WA AMANI
Akiweka msisitizo kuhusu amani, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amir Mkalipa ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, aliwahakikisha wakazi wa mkoa huo kwamba upo salama na tayari kwajili ya Uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Akizungumza wakati wa Tamasha la Mbio Pole pamoja na kupongeza mafanikio ya sekta ya Afya, alisema serikali imejipanga kwa Uchaguzi mkuu na ameahidi uchaguzi utafanyika kwa uhuru na amani.
“Mkoa tumejipanga kwajili ya uchaguzi na tutashirikiana kwa ukaribu sana na wananchi. Tutakabiliana na yeyote yule atakaefanya vurugu,” alisema.
KAULI ZA WANANCHI
Akizungumzia mwenendo wa kampeni za uchaguzi mkuu, Mkazi wa Kiloleni jijini Mwanza, Jospephat Magali, alieleza kwamba kampeni za mwaka huu zimefanyika kwa amani na utulivu.
“CCM kama kawaida yake kimeendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa kufanya kampeni za kistaarabu hasa Dk. Samia amekuwa akisisitiza amani na utulivu wakati wote.
“Ndiyo maana ni rahisi kwa wananchi kufika kwa wingi kwenye mikutano ya CCM kwa sababu wanajua amani imetawala hivyo ajenda zake kuwafikiwa wananchi wengi kwa urahisi,” alisisitiza.
Naye, Mkazi wa Nyakato, Mashaka Rajab alisema amejiandaa kuhudhuria mkutano huo kwani CCM kimeendelea kuwa mstari wa mbele kuwaletea wananchi maendeleo.
“Kwetu Mwanza tumenufaika kwa mambo mengi kuanzia ujenzi wa meli kubwa ya Mv Mwanza, ujenzi wa reli ya SGR na uboreshaji upatikanaji maji,” alifafanua.




