Na NASRA KITANA
TIMU ya soka ya Simba leo itashuka dimbani dhidi JKT Tanzania katika mchezo wa kuwania kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Mchezo huo unatarajiwa kupigwa saa 1:00 usiku katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni, Dar es Salaam.
Katika ligi hiyo, JKT Tanzania ipo nafasi ya tano kwa pointi saba katika mechi tano wakati Simba ipo nafasi ya saba kwa alama sita katika mechi mbili, yeyote kati ya hizo ina nafasi ya kukaa kileleni mwa msimamo kama itavuna pointi tatu katika mtanange wa leo.
Miamba hiyo ipo chini ya Yanga iliyopo nafasi ya nne kwa alama saba katika michezo mitatu, Mashujaa, Dodoma Jiji na Mbeya City ambayo kila moja ina pointii nane zikicheza mechi sita.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kocha Msaidizi wa Simba, Suleiman Matola, alisema wataingia katika mchezo huo kwa kuwaheshimu wapinzani lakini watahakikisha wanapata pointi tatu muhimu.
Kocha Matola alisema JKT ni timu nzuri yenye wachezaji wenye viwango bora hivyo wataingia kwa tahadhari kubwa na kufanya mashambulizi ya kushtukiza kupata ushindi.
“Ni mchezo mgumu lakini tunaiheshimu JKT Tanzania, tutaingia kwa tahadhari na kupambana mwanzo mwisho, tunataka kupata ushindi na kujizolea pointi tatu muhimu,” alisema Matola.
Kocha huyo alisema hana hofu na kikosi chake kwani kila mchezaji anajua jukumu lake la kuipambania timu katika kila mchezo wanaocheza.
Matola alisema kuwa wachezaji wote wapo fiti isipokuwa kipa wake Moussa Camara atakosekana kutokana na majeraha lakini wana kikosi kipana chenye ushindani.
Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally alisema timu yao imejipanga vizuri kupambana na Simba japokuwa ina wachezaji wazuri wenye viwango bora.
Alisema hawana presha na mchezo huo kwani wamefanya maandalizi ya kutosha na anaifahamu vyema Simba hivyo ataingia na mbinu mbadala kupata ushindi.
“Simba ni timu kubwa na yenye wachezaji bora, lakini hatuna presha kwani tumejipanga vyema kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo huo hasa katika uwanja wa nyumbani,” alisema Ahmad.




