Na NASRA KITANA
WAKATI kikosi cha timu ya Taifa Stars kikianza mazoezi rasmi kwa maandalizi ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Kuwait, Kaimu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi amesema kuwa anajivunia kikosi alichokuwa nacho kuwa kitaienda kufanya vizuri.
Gamond ambaye ni Kocha wa Singida Black Stars, ameiongoza Stars kwa mara ya kwanza katika maandalizi hayo baada ya kurithi mikoba ya aliyekuwa mtangulizi wake Hemed Suleiman ‘Morocco’.
Stars inatarajiwa kushuka dimbani Novemba 15, mwaka huu katika mchezo wa kirafiki Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa (FIFA) dhidi ya Kuwait utakaochezwa Uwanja wa Al Salam jijini Cairo nchini Misri kuanzia saa 1:00 usiku.
Akizungumza baada ya mazoezi yake ya kwanza alisema anajivunia wachezaji wote aliowaita kikosini na kwamba ana imani kila mmoja atatimiza majukumu yake katika mchezo huo.
Alisema kutokana na wachezaji wote kuwa wanazitumikia klabu zao, hivyo anaamini wapo fiti na atafanya uboreshaji mdogo ili kuwa na kikosi kitakachompa matokeo chanya.
Alisema kuwa muda ni mchache umekabia wa kufanya maandalizi, ana imani kuwa kila mchezaji aliyenaye kikosini ana uzoefu wa kucheza mechi kubwa.
“Tumeanza mazoezi yetu na nafurahi kuona kila mchezaji yupo fiti na amejipanga vyema, mimi nitarekebisha mapungufu nitakayoyaona ili niweze kuwa na kikosi imara na kitakachofanya vizuri katika mchezo huo muhimu.
“Ninafurahia wachezaji nilionao kikosini kwani wanatoka katika klabu tofauti, hivyo ninaamini tutafikia malengo ya kufanya vyema katika mechi zitakazotukabili,” alisema Gamondi.
Kocha huyo alisema kuwa ana imani kila mchezaji ataonyesha uwezo mkubwa aliokuwa nao na kuipambania timu kupata ushindi.
Hata hivyo Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo alisema kuwa maandalizi yote ya safari yapo vizuri na leo saa 5 asubuhi kikosi kitaondoka kwenda nchini Misri.
“Maandalizi yote yapo vizuri, timu itaondoka kesho (leo) saa 5 asubuhi kwenda Misri kwa maandalizi ya mwisho ya mchezo huo,” alisema Ndimbo.
Ndimbo alisema Watanzania wanatakiwa kuendelea kuiunga mkono timu yao kila inapocheza ili wachezaji waweze kupata morari ya kutosha ya kufanya vizuri.




