SELINA MATHEW na MUSSA YUSUPH,
Dodoma
WAZIRI Mkuu Mteule, Dk. Mwigulu Nchemba, amewataka watumishi wa umma ambao ni wazembe, wala rushwa na wenye lugha mbaya kwa wananchi wabadilike kuwezesha maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea Watanzania maendeleo yaweze kutimia.
“Watumishi wa umma na Watanzania wote tuwe tayari, lazima twende kwa gia ya kupandia mlima, lazima twende kwa gia ya kupita kwenye bahari yenye mawimbi, lazima twende kwa gia ya kupita kwenye anga lene mawingu, lazima hombo kifike salama na watu wake wakiwa salama.
“Kwa watumishi wavivu, wazembe nitakuja na fyekeo na rato. Lazima maono ya Mheshimiwa Rais na ahadi ambazo amewaahidi Watanzania zitekelezwe,”alisema Dk. Mwigulu.
Dk. Mwigulu aliyasema hayo bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akitoa shukurani baada akuthibitishwa na Bunge kufuatia uteuzi wa Rais Dk. Samia kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia, Dk. Mwigulu alitumia fursa hiyo kuwahakikishia Watanzania kwamba yote yaliyoahidiwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025/2030 na yaliyoahidiwa na Rais Dk. Samia na Makamu wa Rais Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, yatatekelezwa iwapo wataendelea kumtanguliza Mungu na kudumisha amani.
“Spika, katika kipindi cha miaka mitano, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amejitambulisha kuwa ni rais anayetaka matokeo ya haraka yanayotatua matatizo ya Watanzania.
“Amefanya hivyo wakati alipoingia madarakani kukiwa na tatizo kubwa la umeme, aliweka jitihada kubwa za kukamilisha mradi mkubwa wa bwala la Mwalimu erere ambalo limemaliza tatizo la kukatika katika kwa umeme,” alisema.
Dk. Mwigulu aliongeza kuwa wakati Rais Dk. Samia alipoingia madarakani kulikuwa na tatizo la vifo vya wajawazito na watoto kutokana na upungufu wa hospitali na vituo vya afya.
“Katika kipindi kifupi amejenga zaidi ya hospitali 119 za wilaya, zaidi ya vituo vya afya 649 katika kata mbalimbali, zaidi ya zahanati 2,800 nchi nzima.”
“Katika kipindi kifupi amejenga shule mpya zaidi 2,700 za msingi na shule zaidi 1,300 za sekondari na madarasa zaidi 97,000, hivyo hivyo katika sekta zingine ikiwemo kununua CT Scan hospitali zote za mikoa na MRI katika hospitali za Kanda na mitambo ya kuchimbia visima vya maji kwenye kila mkoa na kila ukanda na hiki ndicho kilichowafanya Watanzania wamchague kwa wingi na nimetaja machache,” aliongeza.
Akizungumzia utekelezaji wa Dira mpya ya Maendeleo ya Mwaka 2050, Dk. Mwigulu alisema imebeba matumaini makubwa ya Watanzania, wakiwemo vijana ambao ndio hasa walengwa hivyo kuna kazi kubwa ya kuanza utekelezaji wake na kumalizia viporo vya dira ya 2025.
“Nitumie fursa hii kumshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kunipendekeza kushika nafasi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Natambua uzito wa majukumu haya pamoja na maratajio yake pamoja na matarajio ya Watanzania, nitafanya kazi kwa bidii, kwa uaminifu mkubwa na jitihada kubwa kuweza kukidhi matarajio haya,”
alisema Dk. Mwigulu aliyethibitishwa kwa kupata kura 369 kati ya kura 371 zilizopigwa.
AJIRA KWA VIJANA
Alisema Dk. Samia alitoa ahadi kupitia Ilani ya Uchaguzi kushughulikia tatizo la ajira kwa vijana, ambapo zitatengenezwa ajira milioni nane kwa vijana wa Tanzania jambo ambalo litaratibiwa na kusimamiwa kuhakikisha ndoto hiyo inatimia.
Alibainisha pamoja na Tanzania kuwa nchi tajiri, kuna asilimia isiyopungua nane ya Watanzania wanaoishi katika umaskini wa kupindukia huku asilimia 26 wanaishi katika umaskini wa kipato.
“Niwakumbushe Watanzania mimi umaskini wa Watanzania sijausoma katika kitabu nimeuishi, katika maisha yangu miaka takribani 32 nimeishi maisha ya umaskini, nimeishi maisha ambayo mama zetu, dada zetu wakivaa gauni huwa wanajifunga nguo kiunoni.
“Ile nguo wanayojifunga ndiyo ilikuwa yangu ya kujifunika, kwa hiyo kabla hajamaliza shughuli zake za kila siku silali mpaka akalale ili nipate shuka la kujifunika, asubuhi kabla hajaanza kazi lazima niamke ili ile nguo nimpe ajifunge aanze majukumu yake,”alisema Dk. Mwigulu. Aliongeza kuwa:
“Natambua mazingira ya kulala unaenda kuchunga ukirudi nyumba nzima inavuja na utakapolala inabidi ujifunike ngozi ili matone yanayovuja yatue katika ngozi, natambua maisha hayo.
“Natambua mnaenda kula pamoja na watoto wote takribani ishirini katika chungu kimoja cha mboga, ugali inabidi utangulize ugali mwingine mdomoni bila mboga sababu ukisubiri mikono iishe katika chungu cha mboga chakula kitakuwa kimeisha,” alisema.
Alisema alipomaliza chuo alifanya kazi ya kubeba zege katika kiwanda cha matofali apate fedha, huku mkewe akipika mama lishe na wakati anagawa chakula kulikuwa na maneno makali.
WATANZANIA WA CHINI KUSIKILIZWA
“Niwahakikishie Watanzania hasa wa mazingira a hini, watasikilizwa katika kila ofisi ya umma, kila aliye Mtanzania hii nchi ni yake, watasikilizwa kwa nidhamu, watafikisha kero zao na watumishi wa umma watakwenda katika maeneo yao kuzitatua.
“Ukiondoa miaka 32 niliyoielezea, takribani miaka 18 maisha yangu yalizungukwa na wahitaji kuliko walioridhika, natambua mahitaji na uhitaji wa Watanzania,”alisema.
ASISITIZA AMANI
Pia, alitoa rai kwa Watanzania yote yatatimia ikiwa watamtanguliza Mungu mbele katika mambo mbalimbali na taifa likiwa na hali amani huku akisisitiza bila amani haawezi kufikiwa.
“Watanzania wote tuwe na wajibu wa kuhakikisha nchi inakuwa na amani muda wote, tumtangulize Mwenyezi Mungu hata kwa yale tunayoona magumu ili atusaidie kupata ufumbuzi wake,”alisisitiza.
Kadhalika, alimpongeza Waziri Mkuu Mstaafu, Kassim Majaliwa kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa taifa bila kuchoka ya ufuatiliaji wa miradi, shughuli za serikali kwa unyeyekevu na uadilifu.
“Naamini kila Mtanzania anatambua jitihada kubwa alizofanya kumsaidia Dk. Samia,” alisema Dk. Mwigulu.
AMSHUKURU RAIS
Dk. Mwigulu alimshukuru Rais Dk. Samia kwa imani kubwa aliyoonesha kwake ya kumpendekeza kushika wadhifa huo, huku akieleza si kubwa tu kwake bali ni dhamana kubwa kwa Watanzania.
“Natambua uzito wa majukumu haya, pamoja na matarajio yake na Watanzania, nitafanya kazi kwa bidii, uaminifu na jitihada kubwa kukidhi matarajio hayo,”alisema Dk.Mwigulu.
JINA LILIVYOLETWA
Saa 3:06 alasiri mpambe wa Rais Brigedia Jenerali Nyamburi Mashauri, aliwasilisha jina la Waziri Mkuu mteule kwa Spika wa Bunge, Mussa Zungu na kusomwa kwa wabunge kwa ajili ya kumthibitisha.
Saa 03:46 alasiri Bunge lilirejea ambapo Mwansheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari alisoma azimio la Bunge la kumthibitisha Waziri Mkuu.
Pia, alitaja sifa za Waziri Mkuu mteule kuwa ni kiunganishi ha serikali na wananhi hao ni majukumu makubwa anahitaji mtu mhaakazi, mumiliu, busara na ueo.
“Uongozi wake ni kilelezo kupitia nafasi alizoshika ikiwemo Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha, Waziri wa Kilimo, Waziri wa Katiba na Sheria na Waziri wa Mambo ya Ndani na mchumi mbobevu mwenye shahada ya uzamivu.
WABUNGE WAMPONGEZA
Mbunge wa Kakonko, Allan Mvano alisema hawana shaka na utendaji wa Waziri Mkuu mteule kwa kuwa anakwenda kumsaidia Rais kwa uwajibikaji hususani kwa watumishi wa umma.
Dk. Dorothy Gwajima alisema Dk. Mwigulu ana utendaji kazi mkubwa, anapambania haki za watu na hapendi kuona watu wananyanyaswa.
Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye alisema amefanya kazi na Dk. Mwigulu muda mrefu ni mchapakazi anayependa watu, hivyo uteuzi wake unawaeleza Watanzania kwamba mtu yeyote anaweza kuwa kiongozi.
Mbunge wa Musoma Mjini, Mgore Kigera alisema Rais Dk. Samia amekidhi mioyo ya Watanzania wengi na kuweka imani kwao kupitia uteuzi huo. Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Katavi, Martha Maliki alisema uteuzi wa Dk. Mwigulu, utaleta mapinduzi makubwa hususani katika sekta mbalimbali.
Mbunge wa Jimbo la Hai, Saashisha Mafuwe alisema Dk. Mwigulu ni mtu wa mipango mwenye uzoefu serikalini na anajua mahitaji ya nchi.
Mbunge wa Manyoni, Dk. Pius Chaya alisema uzoefu wa Dk. Mwigulu na elimu yake ya udaktari, umri wake ni vigezo tosha kuwa kiongozi wa juu kama mwakilishi wa serikali bungeni.




