Na NASRA KITANA
IKISALIA wiki moja kabla ya kucheza mechi zake za kwanza za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), Simba na Yanga zinatarajiwa kucheza mechi za kirafiki kujifua.
Katika CAFCL wiki ijayo, Yanga iliyopo kundi B inatarajiwa kuchuana na FAR Rabat ya Morocco wakati Simba iliyopo kundi D, ikicheza na Petro de Luanda.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema timu yao imeshaanza mazoezi kwa wachezaji ambao hawapo katika timu ya taifa na mwalimu ameomba mchezo mmoja wa kirafiki kabla ya kuchuana na Petro de Luanda.
Amesema mwalimu wao ametaka mchezo huo ikiwa ni moja ya maandalizi katika mechi ya kimataifa kwani anahitaji kuona wapi kuna mapungufu afanye marekebisho ya mapema.
Ahmed amesema lengo kubwa la mchezo huo wa kifariki ni kuwaweka sawa wachezaji wao ambao hawajaitwa katika kikosi cha Stars.
Naye Ofisa habari wa Yanga Ally Kamwe amesema timu yao leo inatarajiwa kushuka dimbani kupambana na KMC katika mchezo wa kirafiki.
Amesema mchezo huo ni muhimu kwa wachezaji wao kwani itakuwa ni moja ya maandalizi kabla ya kushuka dimbani kumenyana na FAR Rabat.
“Tunajua tunaingia katika mchezo mgumu hivyo mwalimu ameona bora kupata mchezo wa kirafiki dhidi ya KMC kujiweka sawa kabla ya kukabiliana na wapinzani wetu,” amesema.
Katika kundi B, Yanga imepangwa na timu za Al Ahly ya Misri, AS FAR ya Morocco na JS Kabyile ya Algeria wakati Simba ikiwa kundi D na Esperance kutoka Tunisia, Petro De Luanda ya Angola na Stade Malien kutoka Mali.



