Na MUSSA YUSUPH
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali imejipanga kuhakikisha kahawa inayozalishwa nchini inaongezwa thamani kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.
Alieleza hayo katika mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa VETA mjini Songea ambapo alisema Januari, mwaka huu, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa nchi 25 za Afrika zinazozalisha kahawa.
Dk. Samia alisema katika mkutano huo, liliwekwa lengo la ndani ya miaka 10 ijayo (2025-2035) asilimia 50 ya kahawa bora inayozalishwa Afrika iwe inasindikwa kabla ya kuuzwa nje ya Afrika.
Alibainisha lengo la serikali kutekeleza azimio hilo, ambapo CCM imeweka ahadi kuweka mitambo ya kukoboa kahawa kabla haijauzwa.
Alisema serikali imetekeleza mradi wa ujenzi maghala 28 ya kuhifadhia mazao mkoani Ruvuma akiainisha Halmashauri ya Wilaya ya Songea ina maghala 11, Madaba (tisa), Namtumbo (saba) na ghala moja kwa Manispaa ya Songea.
Aidha, alisema katika Manispaa ya Songea, serikali itakamilisha ujenzi wa soko la kisasa Manzese A na B.
“Soko hilo ambalo mmelisubiri kwa muda mrefu hivi sasa linajengwa na hatujawasahau wanangu wamachinga mtakuwa na sehemu katika soko hilo.
“Niseme pia mkoa huu umebarikiwa kuwa na madini mengi kuanzia dhahabu, shaba, makaa ya mawe, madini ujenzi na vito hadi urani yanapatikana ndani ya mkoa huu,” alisisitiza.
Dk. Samia alieleza endapo CCM ikipatiwa ridhaa, serikali yake itaanzisha na kuendeleza kongani za viwanda zinazohusiana na madini.
Aliongeza hatua hiyo itasaidia kuongeza thamani ya madini kabla ya kuuzwa huku kipaumbele kikiwa katika uchimbaji na wachimbaji wadogo.