Na NJUMAI NGOTA,
Songwe
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema iwapo kitapewa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi, kitahakikisha huduma za afya, zinapatikana kwa kila Mtanzania ndani ya umbali wa kilometa tano kutoka mahali anapoishi.
Ahadi hiyo, ilitolewa katika mkutano wa kampeni uliofanyika Chitete, Jimbo la Momba, mkoani Songwe na Mgombea Mwenza wa Urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, alipohutubia mamia ya wananchi waliokusanyika, kumsikiliza akinadi Ilani ya Uchaguzi ya Chama ya mwaka 2025-2030 na kuelezea utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2020-2025.
Dk. Nchimbi, alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, serikali ya CCM, itaendelea kusogeza huduma muhimu za kijamii kwa wananchi, hasa afya ambazo ni haki ya msingi ya kila Mtanzania.
“Tunataka kila Mtanzania awe na uhakika wa huduma ya afya ndani ya kilometa tano kutoka eneo analoishi.
“Pia, Serikali ya CCM katika miaka mitano ijayo inakwenda kuanzisha utaratibu wa bima ya afya kwa Watanzania wote.
“Tunataka ndani ya miaka mitano huduma ya afya ya kila Mtanzania pamoja kuimarika, apate huduma hiyo karibu zaidi,”alisema.
MIUNDOMBINU YAAFYA KUIMARISHWA
Akieleza mikakati ya kuboresha miundombinu ya afya katika Jimbo la Momba, Dk. Nchimbi, alisema serikali ya CCM, itakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Momba kwa viwango vya kisasa, kujenga vituo vya afya vinne, zahanati 12 na nyumba 24 za watumishi wa sekta hiyo.
ELIMU BILA MALIPO
Katika sekta ya elimu, Dk. Nchimbi, alisema serikali ya CCM, itaendeleza utaratibu wa elimu bila malipo kuanzia chekechea hadi kidato cha sita, huku ikiongeza madarasa mapya na miundombinu bora ya kujifunzia.
“Tutajenga madarasa 104 katika shule za msingi na sekondari, tuna mpango wa kujenga maabara 51 za kisasa, kuwajengea watoto wetu uwezo wa kisayansi na kiteknolojia,” alisema.
KILIMO
Kwa upande wa sekta ya kilimo, ambayo ndiyo uti wa mgongo wa wananchi wengi wa Momba na Mkoa wa Songwe, Dk. Nchimbi, alisema serikali ya CCM, itaongeza ruzuku ya mbolea, mbegu na kuhakikisha zinatolewa kwa wakati na ubora wa hali ya juu.
UFUGAJI
Akizungumzia sekta ya ufugaji, aliahidi kujengwa majosho saba, minada minne na machinjio manne, kuinua maisha ya wafugaji na kuongeza thamani ya mifugo yao.
Dk. Nchimbi, alisema katika sekta ya barabara, wanakusudia kujenga kwa kiwango cha lami, changarawe na ujenzi wa madaraja mbalimbali, kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa vijijini na mijini.
Kuhusu huduma ya maji, Dk. Nchimbi, alisema katika miaka mitano ijayo, wakipewa ridhaa ya kuongoza, wataendeleza miradi mikubwa ya maji, kwa lengo la kuongeza upatikanaji huduma hiyo, kutoka asilimia 44 hadi asilimia 80, ndani ya jimbo hilo.
Katika mkutano huo, Dk. Nchimbi, alimwombea kura Mgombea Urais wa CCM, Rais Dk. Samia, wagombea ubunge na udiwani wanaotokana na Chama.
Dk. Nchimbi, aliwasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, mwaka huu, kwa kukichagua Chama kwa ushindi wa kishindo
CONDESTER SICHALWE
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Momba kwa tiketi ya CCM, Condester Sichalwe, aliwahimiza wananchi kuendelea kuiamini CCM kwa kuangalia utekelezaji mkubwa wa miradi ya maendeleo iliyofanyika katika kipindi cha miaka minne na nusu chini ya uongozi wa Dk. Samia.
“CCM ni Chama chenye uwezo, sera madhubuti, na dhamira ya dhati ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli. Tunaomba kura zenu kwa Dk. Samia, wabunge na madiwani wote,” alisema.
CECILIA PARESO
Kada wa CCM, Cecilia Pareso, aliwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi huo, huku akisisitiza umuhimu wa kupiga kura kwa usahihi, kwa kuwachagua wagombea wote wa CCM.
“Tupige kura zetu kwa alama ya tiki katika alama ya jembe na nyundo, tuendelee na safari ya maendeleo iliyoanza,” alisema.




