NA MUSSA YUSUPH
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupigakura kwani nchi ipo salama wakati wote.
Dk. Samia amesisitiza kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vipo makini wakati wote kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa salama.
Msisitizo huo aliutoa katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika Segerea wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.
“Niliongea jana (juzi) nataka niongee tena leo (jana). Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ndani ya taifa hili, vimejipanga vyema, tumevijengea uwezo wa kutosha.
Alisisitiza: “Tupo salama wakati wote iwe wakati wa uchaguzi, iwe hakuna uchaguzi tupo salama wakati wowote. Hivi vimatishio vidogo wanavyovifanya kama mnawaelewa nendeni mkawaulize.”
“Niwatoe hofu wananchi, nendeni mkajitokeze mkapigekura, tupo salama wakati wote,” alisisitiza huku akishangiliwa na umati uliofika kushuhudia mkutano huo wa kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
MSISITIZO UTAWALA BORA
Akizungumzia masuala ya utawala bora, Dk. Samia alisema serikali yake iliunda tume ya haki kijani kuangalia namna haki za wananchi zinavyopatikana.
Dk. Samia alisema tume hiyo baada ya kukamilisha kazi yake iliwasilisha serikalini taarifa ambapo sasa sekta ya haki na sheria ipo vizuri.
“Haki za watu sasa hazipotei kama ilivyokuwa, sasa hivi polisi, mahakama, DPP, DCI wote wanasomana. Ule mchezo wa ndugu zetu kwenda kuweka maneno kwenye taarifa alizosema mtu sasa hivi haupo,” alibainisha.
Alisema serikali inaendelea kujenga miundombinu ya kutolea haki nchini kwa kuboresha mahakama za wilaya, mikoa na jumuishi.
Vilevile, alieleza kuwa, tume ya pili aliyoiunda ni tume ya kuangalia uhusuano wa Tanzania kimataifa.
Alieleza kuwa, baada ya tume hiyo kukamilisha kazi yake, Tanzania imefanikiwa kurejesha heshima yake kimataifa.
Dk. Samia, alisema tume nyingine ya kutengeneza Dira ya Taifa ya Maendeleo ambayo iliongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Asha- Rose Migiro.
Alifafanua kuwa, baada ya tume hiyo kukamilisha kazi yake, kila jambo linalofanywa na serikali, linazingatia mahitaji ya dira ya taifa.
Kadhalika, Dk. Samia alieleza kuwa, serikali yake iliunda tume nyingine maalumu kuangalia masuala ya kikodi nchini.
“Tume ile imemaliza kazi wakati tunaingia kipindi cha kampeni kwa hiyo wataleta taarifa yao baada ya kuunda serikali mkitupa ridhaa yenu.
“Baada ya kuunda serikali italeta taarifa yake na tutafanya mageuzi ya kodi zetu Tanzania lakini maoni yote tumeyapata kwa wananchi,” alibainisha.
Pia, alisema tume nyingine iliyoundwa ni kuangalia mgogoro uliopo Loliondo ambayo nayo imekamilisha kazi yake hivyo baada ya uchaguzi itawasilisha taarifa kisha hatua stahiki zitachukuliwa.
Alisema kuwa, tume zote hizo, zimezingatia maoni ya wananchi hatua ambayo inathibitisha uwepo wa utawala bora nchini.
“Hakuna anayejua kila kitu, ukitaka kuendesha nchi kwa amani lazima uwashirikishe wenye nchi na ndiyo demokrasia.
“Tunafanyakazi kwa ajili ya watu, hao watu ndiyo wenye mpini wa kuendesha nchi, siyo watawala wenye mpini wa kuendesha nchi hii,” alisisitiza.
Dk. Samia, alisema serikali yake imeboresha majengo yanayotoa huduma kwa wananchi ambapo watu wenyeulemavu wanaweza kufika kupata huduma kwa urahisi.
Kwa upande wa halmashauri, alisema serikali imejenga majengo 126 ya halmashauri mbalimbali nchini ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
“Ofisi zilikuwa ziko mbali, anayeshughulika kilimo yupo hapa, maji yupo kule, lakini sasa huduma zote zinapatikana ndani ya jengo moja na ni majengo ya heshima kwelikweli.
“Ili kumpa raha mwananchi, mawasiliano ni muhimu sana. Kipindi hiki cha awamu ya sita tumetenga fedha kujenga minara zaidi ya 700. Lakini mpaka sasa tunavyozungumza tumejenga minara zaidi ya 600.
Alisisitiza: “Maeneo mengi tulipopita kuomba kura wameniambia sasa mawasiliano hatupandi juu ya miti. Kila mahali tunapata mawasiliano.”
MAPATO BANDARI YAPAA
Mgombea Ubunge Jimbo la Ilala, Mussa Zungu, alisema Dk. Samia, aliwafundisha kwamba penye changamoto ndipo kuna ukuaji wa taifa.
Alieleza kuwa, maamuzi ya kuboresha Bandari ya Dar es Salaam, yamechangia ongezeko kubwa la mapato ambapo mwaka 2024/2025 yamefikia sh. trilioni 12.
Alisema ili serikali iweze kutoa huduma za kijamii, uchumi unapaswa usiwe chini ya asilimia nane hali ambayo wakati wa Uviko- 19 uchumi ulishuka hadi asilimia tatu.
Alieleza kuwa, baada ya Dk. Samia kuingia madarakani, uchumi umekuwa kwa kasi, kwani ripoti ya Shirika la Fedha Duniani (IMF), imekadiria uchumi wa Tanzania utakuwa kati ya asilimia sita hadi 6.1.
Alibainisha kuwa, maendeleo ya nchi, hayapimwi kama kipima joto cha mwili, isipokuwa yanapimwa kwa mwelekeo uliopo, wa sasa na ujao.
HUDUMA YA MAJI IMEIMARIKA
Mgombea Ubunge Jimbo la Pangani ambaye ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alisema maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam, yalikuwa yakikabiliwa na changamoto kubwa ya maji.
Alieleza kuwa, maamuzi ya Dk. Samia kutoa zaidi ya sh. bilioni 30 kujenga tanki la maji Bangulo, limeimarisha upatikanaji maji kwa wakazi wa Segerea, Ukonga na Kivule.
“Hapa nina salamu zenu ambazo Dk. Samia amenipa, anatambua tanki limekamilika. Maelekezo aliyoyatoa nenda kwa meneja wa DAWASA hata kama huna hela ya kuunganishiwa maji, utaunganishiwa kisha utalipa kidogo kidogo,” alisisitiza.
Vilevile, alitoa salamu kwa wasoma mita za maji tabia ya kuwabambikizia wananchi bili ya maji, imepatiwa mwarobaini, kwani serikali itaanza kufunga luku za maji.
Aweso, alisema Dk. Samia, ametoa sh. bilioni sita kununua pampu nane za kusukuma maji hatua ambayo itamaliza tatizo la presha ndogo ya maji.
MWENDOKASI HADI CHANIKA
Mgombea Ubunge Jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega, alisema Dk. Samia, ameleta maendeleo makubwa ya miundombinu Jiji la Dar es Salaam.
Ulega ambaye ni Waziri wa Ujenzi, alisema mradi wa mabasi ya mwendokasi, Dk. Samia ameagiza usiishie Pugu, bali ufike hadi Chanika.
Pia, alisema Dk. Samia, ameelekeza mradi huo, uingie Kinyerezi, Tabata Dampo hadi Kigogo, hivyo utaongeza kasi ya maendeleo kwa wananchi.
“Dar es Salaam itakupigia kura nyingi kwa sababu, hakuna mgombea mwenye rekodi nzuri ya kiutendaji kumzidi Dk. Samia,” alibainisha.
TASWIRA YA DAR IMEBADILIKA
Naye, Mgombea Ubunge Jimbo la Arusha Mjini, Paul Makonda, alisema Dk. Samia amebadilisha taswira ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema jengo la mama na mtoto lililopo Hospitali ya Amana ni kazi iliyofanywa na Rais Dk. Samia.
Alisema wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Samia ndiye aliyemhamasisha kuendelea kutoa huduma bure za matibabu kwa wananchi wasiojiweza.
AHADI KUTOKA KWA WANANCHI 300,000
Kwa upande wake, Mgombea Ubunge Jimbo la Ukonga, Jerry Silaa, alisema tangu uzinduzi wa kampeni, jimbo hilo limefanya mikutano zaidi ya 90.
Alisema wananchi wa jimbo hilo zaidi ya 300,000, waliojiandikisha kupigakura watajitokeza kumchagua Dk. Samia.
Alibainisha kuwa, kilometa 23.3 zimetumika kujengwa barabara ya njia sita za mwendokasi kutoka Ukonga hadi Kariakoo.
Vilevile, alieleza kuwa, wananchi wa jimbo hilo, wamenufaika kupitia miradi ya maji kuanzia Pugu huku sh. bilioni 36, zimetumika kujenga tanki kubwa la maji Bangulo, hali iliyowezesha upatikanaji maji kufikia asilimia 83 kutoka asilimia 42.
Kuhusu upatikanaji mawasiliano, Silaa ambaye pia ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, alisema imetoa fedha za mradi wa minara 738 zilizofanikisha mawasiliano.
WAGOMBEA UBUNGE
Mgombea Ubunge Jimbo la Segerea, Bonna Kamoli, alisema serikali katika jimbo hilo, imejenga shule tano za ghorofa na tano za msingi.
Katika sekta ya afya, alisema serikali imejenga vituo vitatu vya afya na kukarabati vituo viwili.
“Katika jimbo letu mikopo ya asilimia 10 tumetoa sh. bilioni 7.6. Tumefanya kampeni na kuwaeleza wananchi mambo yaliyofanyika.
“Katika maji, tulikuwa na uhaba mkubwa, lakini sasa maji yanapatikana baada ya ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji la Bangulo,” alisisitiza.
Bonna alitoa ombi kwa Dk. Samia kwamba miongoni mwa barabara zinazopita katika jimbo hilo itumike kwa usafiri wa mabasi ya mwendokasi.
Naye, Mgombea Ubunge Jimbo la Kivule, Deogratius Masabuli, alieleza kuwa, Dk. Samia, amefanya mambo makubwa katika jimbo hilo, ikiwemo kuanzisha jimbo jipya la uchaguzi Kivule.
Alieleza kuwa, wananchi wa jimbo hilo, wamekubaliana wajibu wao kumpigia kura za kishindo Dk. Samia, kwani jimbo hilo, limepatiwa Kituo cha Afya Msongola, Kipunguni na Mzinga ambacho ni ghorofa.
Alibainisha kuwa, katika elimu jimbo hilo, kumejengwa Shule ya Sekondari ya Ghorofa Kitunda na Kipunguni huku madarasa zaidi ya 250, yamejengwa.
Pia, alisema Dk. Samia, amejenga tanki kubwa la maji lenye ujazo wa lita milioni tisa ambalo limeanza kusambaza maji Kitunda, Mzinga na Kipunguni.
“Maji yalikuwa sifuri lakini leo ni asilimia 42 katika jimbo la Kivule. Barabara ya kutokea Kitunda – Buza mpaka Kwampalange, imewekwa katika ilani.
“Leo hii, makusanyo tumetoka sh. bilioni 75 hadi kufikia sh. bilioni 130, ukiwa ni utekelezaji wa maagizo yako ya kusimamia makusanyo ya halmashauri,” alisema.




