Na HANIFA RAMADHANI,
Zanzibar
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema wana matumaini kuwa CCM itashinda kwa kishindo katika Uchaguzi wa kesho kutwa.
Dk. Mwinyi alisema hayo, katika ufungaji kampeni za Uchaguzi Mkuu wa CCM, uliofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja, Mjini Unguja
Alisema kutokana na wingi wa wanachama na wananchi kwa ujumla katika mikutano ya kampeni, inadhihirisha CCM itapata ushindi wa kishindo.
Dk. Mwinyi alisistiza ushiriki mkubwa wa wananchi katika kupiga kura utasaidia kuondoa malalamiko yanayotolewa na baadhi ya vyama vya siasa kuhusu matokeo ya uchaguzi.
Aidha, aliwataka vijana wa hamasa wa CCM, kuendelea na kazi ya kuwahamasisha wananchi kwenda vituoni kupiga kura siku ya uchaguzi.
“Vijana wangu wa hamasa, mmefanya vizuri katika kampeni, sasa chukueni jukumu hili kwa kutumia hiyo hamasa yenu, kwenda kuwatoa majumbani watu kwenda kupiga kura,” alisema.
Dk. Mwinyi, alisema kampeni zimefanyika vizuri na CCM imenadi sera zake kikamilifu na kuelezea jinsi ilivyotekeleza kwa asilimia kubwa, Ilani yake ya Uchaguzi ya 2020/2025, hivyo hakuna sababu ya kushindwa katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
“Kama kuna chama chenye sera madhubuti, basi ni CCM, ninaamini mtatuchagua kwa kishindo tuendelee kuwatumikia,” alisema.
VIPAUMBELE 10 MIAKA MITANO IJAYO
Mgombea huyo aliyataja maeneo 10 ambayo CCM imeyawekea kipaumbele katika miaka mitano ijayo, ambayo ni kuendelea kuimarisha amani, umoja, mshikamano na maridhiano kwa kuhubiri amani na kuimarisha maridhiano kuleta maendeleo.
Eneo la pili ni kuimarisha miundombinu ikiwemo kiwanja cha ndege cha Kimataifa kisiwani Pemba, kuikarabati Bandari ya Mkoani na Wete, meli kubwa ziende moja kwa moja kisiwani Pemba na kuwa bandari za kimataifa na kuiimarisha Bandari ya Shumba.
Akizungumzia sekta ya miundombinu, Dk. Mwinyi alisema serikali itaendelea kujenga barabara kubwa za ndani kwa kiwango cha lami kurahisisha shughuli za kiuchumi na kujenga skuli za ghorofa kila sehemu, kujenga dahalia na kuajiri walimu kuona watoto wanaendelea kufanya vizuri.
Kwa upande wa sekta ya afya, alisema kuwa, serikali itajenga hospitali za mikoa na kuanza katika Mkoa wa Kaskazini na Kusini Pemba, kwa lengo la kuhakikisha watu wote wanaendelea kupata huduma bora afya.
Dk. Mwinyi, alisema katika awamu ijayo, serikali itahakikisha shehia na mikoa yote ya Pemba, hakuna tatizo la upatikanaji wa maji.
Alieleza kazi hiyo imeanza kwa lita milioni moja, watahakikisha wanaendeleza hilo kuona wananchi wanapata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.
Aliwahakikishia kuwa serikali itanunua mpunga kwa wakulima kipindi cha mavuno kudhibiti upandaji wa bei na kuongeza skimu za umwagiliaji.
Kwa upande wa uhifadhi wa mafuta ya petroli na dizeli, Dk. Mwinyi alisema serikali itahakikisha inajenga hifadhi ya mafuta Unguja na Pemba kuhakikisha nchi inakuwa na hifadhi hiyo kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu.
Kwa upande wa changamoto ya ajira, alisema katika kipindi cha miaka mitano inayokuja CCM itatengeneza ajira 350,000 kwa kuajiri serikalini, zikiwemo katika vyombo vya ulinzi na usalama na sekta nyingine, sekta binafsi kwa kushajihisha kujenga viwanda kuwawezesha vijana kupata ajira na kuwawezesha kwa mikopo isiyokuwa na riba wajiajiri wenyewe.
Mgombea huyo alisema serikali pia itaendelea kuyawezesha makundi mbalimbali yakiwemo wanawake, wavuvi, watu wenye ulemavu, wakulima wadogo wadogo na kujenga viwanda vya kusarifu dagaa na mwani wapate tija zaidi.
Mbali na hayo, aliahidi kuendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara, mikopo isiyokuwa na riba na kuwapa mafunzo ambayo yatasaidia kuendesha biashara zao na kukuza vipato.
Sanjari na hayo, alisema pia serikali itaendelea kuimarisha na kuboresha pencheni jamii, wafanyakazi wa serikali waliostaafu na kuongeza mishahara kwa wafanyakazi kutokana na ukuaji wa uchumi.
Aliahidi kujenga nyumba za maendeleo kila wilaya kwa gharama nafuu kwa wanaotaka kununua na wanaotaka kukodi kuhakikisha watu wanaishi mazingira mazuri.
Kwa sekta ya uchumi wa buluu, Dk. Mwinyi alisema wataiendeleza sekta hiyo kwa kuwa ndiyo sekta mama kwa uchumi wa nchi, ikiwemo kuwekeza katika sekta ya utalii.
Aliwaomba wananchi kumrudisha madarakani aendelee kuyatekeleza kwa kuwa katika awamu ya kwanza aliahidi na kutekeleza na mengine kuvuka lengo.
DK. DIMWA
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Mohamed Said Mohamed ‘Dimwa’ alisema wanahitimisha kampeni hizo baada ya kufanya kwa takriban siku 45 zenye manufaa makubwa.
Alisema Dk. Mwinyi amebebwa sifa nyingi ambazo ndiyo sababu ya Chama kumteua, huku akiitaja sifa kuu ni mtu mwenye hofu ya Mwenyezi Mungu na akiahidi jambo anatekeleza.
Aliwakumbusha wananchi kuichagua CCM kwa kuwa watakuwa wamechagua amani, utulivu na maendeleo ya nchi.
Alieleza kwamba, wananchi wana kila sababu ya kuichagua CCM kwa maendeleo ya kweli.




