Na IRENE MWASOMOLA
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dk. Asha- Rose Migiro, amekuja kivingine kuhakikisha wanachama wanashiriki usimamizi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ametumia kaulimbiu; ‘Shina lako linakuita,’ akitaka kila mwanachama kushiriki kusimamia miradi ya maendeleo ngazi ya mashina.
Amesema kuwa, mashina ndiyo chimbuko la uhai wa Chama kupima utekelezaji wa kazi za serikali zinazofanyika kuanzia ngazi za chini.
Dk. Migiro aliyasema hayo jijini Dar es Salaam, alipozungumza na mabalozi wa mashina na wanachama wa CCM, katika Wilaya za Temeke na Kigamboni, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu.
Alisema mabalozi ni watu muhimu katika usimamizi wa miradi kuanzia chini, hivyo ni vyema wakapewa ushirikiano na viongozi wengine kuanzia ngazi ya tawi hadi mkoa.
Pia, aliwataka viongozi wa mashina, kushirikiana na madiwani kufuatilia miradi inayotekelezwa na vitega uchumi vya Chama.
“Viongozi wa ngazi za wilaya na maeneo mengine tukiwa kwenye mashina, lazima tushiriki katika vikao, viongozi wa mashina, matawi na kata, tuwe madhubuti kuwavuta viongozi wenzetu washiriki mikutano na utatuzi wa yale tunayopitia katika mashina na matawi yetu,” alisema.
Dk. Migiro, alisema maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa viongozi wa Chama ni kuzingatia utaratibu wa kufanya vikao kwa mujibu wa kanuni na utaratibu za Chama.
“Tuzingatie kanuni za Chama tujitahidi kufanya vikao vyetu kama tunavyotakiwa kwa mujibu wa kanuni na utaratibu wetu wa CCM, kupitia vikao, tutakuwa tunapima utekelelezaji wa kazi za serikali na uimara wa Chama Cha Mapinduzi,”alisema.
Alisema dhamira ya Rais Samia ni kuhakikisha Chama kinakuwa madhubuti kuanzia ngazi ya shina.
Vilevile, aliwataka wanachama wa CCM, kutumia wazee waliopo ndani ya Chama kupata maarifa na ujuzi wa kukijenga Chama.
“Katika ujenzi wa Chama chetu, tuna wakereketwa wengi, tuwatumie kukijenga Chama,”aliongeza Balozi Dk. Migiro.
Balozi Dk. Migiro, aliwataka wanachama wa CCM, kuendelea kusimamia utekelezaji wa Ilani, kusoma na kufuatilia kwa karibu vitabu vidogo vya Ilani vilivyotolewa maeneo mbalimbali katika kipindi cha kampeni kabla ya kufanyika uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka jana.
Aliwataka viongozi wa mashina, kuhakikisha wanaendelea kuwaeleza wananchi mambo mazuri yanayofanywa na Chama katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Dk. Migiro, alisema ni muhimu viongozi wa shina na ngazi zingine, kufanya kazi kwa kuzingatia utu wa Mtanzania.
Chama kilitumia kaulimbiu yake ya ‘Kazi na Utu Tunasonga Mbele’ wakati wa kampeni ya chaguzi mkuu ambapo CCM ilipata ushindi wa kishindo.
Pia, Balozi Dk. Migiro, wakati wa kampeni, alikuwa na kinogesho akisema; ‘Samia eeeh..Samia rahaaa’.
KAULI YA MNEC DAR
Kaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Juma Simba, alimpongeza Dk. Migiro kuanza ziara yake mkoani humo na dhamira ya kukutana na wajumbe wa mashina.
Alisema kwamba, ziara hiyo, ina lengo la kuendelea kukijenga Chama.
Balozi wa Shina namba nne Temeke, Abdu Bilali, alimshukuru Balozi Dk. Migiro kwa kuona umuhimu wa kuzungumza nao.
RC CHALAMILA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema serikali chini ya CCM, inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali, ikiwemo ya barabara, ambayo inalenga kumaliza changamoto ya foleni kwa wakazi wa jiji hilo.
Alitaja baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa Daraja la Jangwani linalogharimu zaidi ya sh. bilioni sita, Daraja la Mzinga sh. bilioni 54 na Daraja la Mkwajuni sh. bilioni 11.
Ziara ya Balozi Dk. Migiro inatarajiwa kuendelea kesho na Januari 13 katika majimbo ya Ubungo, Kibamba na Kinondoni.




