NA MUSSA YUSUPH
DODOMA
SHANGWE zimetawala katika Jiji la Dodoma na viunga vyake baada ya ujio wa mwanasoka maarufu duniani, Reo Ferdinand, aliyewahi kusakata kabumbu katika klabu ya Manchester United na Timu ya Taifa ya Uingereza.
Mchezaji huyo ambaye amefanikiwa kushinda mataji sita ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na moja la Klabu Bingwa Ulaya, aliwasili jana jijini hapa akitokea Dar es Salaam.
Baada ya kuwasili katika Stesheni ya Samia Suluhu Hassan, Ferdinand alipokelewa kwa shangwe na mamia ya wananchi wakiongozwa na kikundi maarufu cha ngoma ya asili cha Nyota.
Wakati kikundi hicho kikitumbuiza kwa nyimbo za kabila la kigogo, Rio alitoa simu yake na kuanza kurekodi hali iliyoonyesha kuwa alikoshwa na burudani iliyoporomoshwa.
Saa sita mchana, mwanasoka huyo ambaye pia ni mchambuzi wa soka, aliwasili katika viwanja vya Bunge akiwa katika gari aina ya Toyota LandCruiser V8 lenye namba za usajili T. 758 EMJ na kupokelewa na mwenyeji wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda.
Makonda alisema baada ya ziara hiyo mkoani hapa, staa huyo atapata fursa kutembelea ujenzi wa uwanja wa AFCON uliopo Arusha na Hifadhi ya Taifa Serengeti.
“Tumeona ni muhimu akanyaje ardhi ya Arusha ashuhudie Rais Samia anavyowekeza kwa vijana kupitia soka,” alibainisha.
Staa huyo wa soka pia alipata fursa ya kuzungumza machache na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Profesa Paramagamba Kabudi.
Katika mazungumzo hayo nje ya viwanja vya Bunge, Profesa Kabudi alimweleza kwa ufupi namna ambavyo Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kuboresha mchezo wa soka nchini.
Pia, alimweleza kuwa akifika Serengeti atashuhudia vivutio vya kila aina ambavyo vinapatikana kwenye hifadhi hiyo.
“Ukifika Serengeti utashuhudia vivutio vyote vya uhifadhi vilivyopo Afrika katika eneo moja,” alisisitiza Profesa Kabudi.
Alisema Tanzania ni taifa lenye mchanganyiko wa tamaduni kwa sababu ya muingiliano wa watu mbalimbali. “Tunasema kwamba Tanzania ni ardhi ya Kilimanjaro, Serengeti na Zanzibar,” alisisitiza.




