Na VICTOR MKUMBO
WAKATI msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara ukielekea ukingoni, vita ya timu kuwania nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao, imezidi kunoga.
Tanzania ni moja ya nchi ambazo zinatarajia kupeleka timu nne msimu ujao katika michuano ya kimataifa inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Katika michuano hiyo msimu ujao, Tanzania inatarajia kuwakilishwa na timu mbili michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) huku zingine mbili zikiiwakilisha kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC).
Vita imezidi kunoga kufuatia timu saba kupambana vikali kuwania nafasi hizo kwa ajili ya kwenda kuiwakilisha Tanzania kimataifa msimu ujao.
Kwa mujibu wa msimamo, Yanga na Simba zinavutana vikali katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hata hivyo timu hizo kongwe ndizo zilizojiweka katika nafasi nzuri ya kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya CAFCL msimu ujao.
Yanga iliyopo kileleni mwa msimamo kwa pointi 54, tayari imeshacheza mechi 23 ikibakisha saba ambapo imepoteza mchezo mmoja, imeshinda mechi 16 na kutoa sare mara sita hadi hivi sasa.
Kwa upande wa Simba ambayo ipo nafasi ya pili, inaifukuzia Yanga kwa ukaribu zaidi katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambapo imefikisha pointi 49 katika mechi 22, imeshinda mara 14, imetoa sare mechi sita na kupoteza mchezo mmoja msimu huu.
Vilevile, Azam inayoshikilia nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, imejiwekea mazingira mazuri kuhakikisha inashiriki michuano ya CAFCC msimu ujao kama itaendelea kuchanga vyema karata zake.
Katika msimamo, Azam ipo nafasi ya tatu kwa pointi 43, ikicheza mechi 22, imepoteza mara moja, sare 10 na kushinda michezo 11.
Timu zingine zinazoiwania nafasi ya kucheza CAFCC msimu ujao ni Singida Black Stars, JKT Tanzania, TRA United na Dodoma Jiji ambazo zimepishana pointi chache katika msimamo.
Katika msimamo huo, Singida BS ina pointi 38, JKT Tanzania (36), TRA United (34) huku Dodoma Jiji ikifikisha alama 32, kila mmoja ikicheza mechi 23.
Kwa mujibu wa takwimu zilivyo, timu hizo zimepishana pointi chache na kwamba itakayozichanga karata zake vizuri, itakuwa na nafasi ya kukata tiketi ya kucheza kimataifa msimu ujao.
Mchezaji wa zamani wa Yanga, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’, alisema ushindani ni mkubwa katika michuano hiyo msimu huu na kwamba timu itakayojipanga vyema, ndiyo itakayofikia malengo.
Alisema pia, timu zinazowania nafasi ya kimataifa, zinatakiwa kujipanga kwa msimu ujao na kufanya usajili mzuri ili kuhakikisha zinazipa changamoto zile zilizozoeleka miaka yote.
“Ushindani ni mkubwa na kwamba timu itakayochanga karata zake vizuri ndiyo itafikia malengo, pia zifanye usajili wa kutosha kwa msimu ujao ili kuhakikisha zinazipa changamoto zile zilizozoeleka miaka yote,” alisema.



