Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Nishati, Salome Makamba amesema mfumo wa kidijitali wa kutoa huduma za mafuta na gesi wa PRIS uliozinduliwa na Puma Energy Tanzania ni hatua muhimu katika kuimarisha uchumi wa kisasa unaotegemea teknolojia ndani ya sekta ya mafuta nchini.
Salome alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa mfumo huo uliofanyika katika Johari Rotana jijini Dar es Salaam.
Amesema sekta ya nishati ni mhimili muhimu wa uchumi wa taifa, hivyo matumizi ya mifumo ya kidijitali yataongeza ufanisi wa utoaji wa huduma pamoja na kukuza matumizi ya teknolojia nchini.
Kwa mujibu wa Salome, mfumo wa PRIS ni teknolojia ya kisasa itakayosaidia kusimamia shughuli za vituo vya mafuta ikiwemo mauzo, malipo, usimamizi wa stoo za mafuta na upatikanaji wa taarifa za biashara kwa wakati halisi.
Amesema mfumo huo unalenga kuongeza ufanisi, uwazi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wateja sambamba na kuboresha usimamizi wa biashara ya mafuta nchini.
Aidha, ameipongeza Puma Energy Tanzania kwa kuendelea kuwekeza nchini kupitia ubunifu wa kidijitali, upanuzi wa vituo vya mafuta na uwekezaji katika nishati safi ya CNG.
Salome alisema mfumo huo unaendana na malengo ya Tanzania ya kujenga uchumi wa kidijitali kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na mkakati wa DESF 2024–2034.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Fatma Abdallah alisema kutambulishwa kwa mfumo huo ni hatua muhimu katika safari ya kampuni ya kuendelea kuboresha huduma kwa wateja kwa kuwekeza katika suluhisho la kisasa lenye kuleta thamani halisi nchini.
Amesema kampuni hiyo ni mshirika mkubwa wa maendeleo ya sekta ya nishati nchini, ikiwa na zaidi ya vituo 100 vya huduma kote nchini, pamoja na huduma za mafuta ya ndege katika viwanja vya ndege, nishati safi ya kupikia ya Puma Gas na uwekezaji katika miundombinu ya kisasa.
“Mafanikio ya kweli huanza na mteja. Ndiyo maana leo tunazindua PRIS, programu ya kwanza nchini Tanzania inayowezesha wateja kupata huduma za Puma pamoja na zawadi mbalimbali kupitia matumizi ya mafuta na bidhaa za Puma,” alisema Fatma.
Ameongeza kuwa kupitia mfumo huo, kila mteja atakayenunua mafuta katika vituo vya kampuni hiyo ataweza kukusanya alama na kuzitumia baadaye kupata manufaa ndani ya mtandao wa kampuni pamoja na washirika wake.
Fatma amesema uzinduzi huo unaunga mkono Dira ya Taifa ya kujenga uchumi wa kidijitali unaolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha teknolojia ya kidijitali katika ukanda wa Afrika.
Aidha, amesema mfumo huo tayari umepata mafanikio makubwa katika masoko mengine ya Afrika ambako kampuni hiyo inaendesha shughuli zake, ikiwemo Malawi, Zimbabwe na Botswana, na kwamba hali hiyo inatoa matumaini makubwa kwa Watanzania kunufaika na ubunifu huo.





