Na NASRA KITANA
SAA kadhaa kabla ya kuvaana na Nsingizini Hotspurs ya Eswatini katika mechi ya marudiano ya hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), benchi la ufundi la Simba, limesema linahitaji timu yake kupata ushindi wa mabao mengi leo.
Simba itachuana na Nsingizini Hotspurs saa 11:00 jioni katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Katika mtanange huo, Simba itaingia na mtaji wa mabao 3-0 iliyoupata katika mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Eswatini.
Akizungumza Dar es Salaam, Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, amesema timu yao imejipanga vyema kuhakikisha inapata ushindi mnono katika mtanange huo.
Matola alisema anajua hautakuwa mchezo mwepesi kwani kila timu inahitaji ushindi lakini watahakikisha wanafanya kila linalowezekana kuibuka na ushindi kujihakikishia nafasi ya kutinga makundi.
“Ni kweli tuna uzoefu mkubwa katika michuano hii lakini hatutaki kurudia kile kilichowahi kutukuta misimu kadhaa nyuma, hii ni mechi nyingine yenye uhitaji mkubwa kama ilivyokuwa ya ugenini,” alisema.
Kocha huyo alisema hana hofu na wachezaji wake kwani wanajua umuhimu wa mchezo huo hivyo watahakikisha wanapanga kikosi bora chenye ushindani mkubwa.
Matola alisema beki wa kikosi hicho, Wilson Nangu aliyepata majeraha mechi ya kwanza yupo fiti kucheza, huku kiungo mshambuliaji, Mohamed Bajaber akiendelea vizuri baada ya kupewa programu maalumu.
Nahodha wa timu hiyo, Shomari Kapombe, alisema pamoja na ushindi walioupata katika mechi ya kwanza ila wao kama wachezaji wamejipanga vizuri kuendeleza kiwango bora zaidi.
“Niwaombe mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kwa sababu mechi za kwanza hawakupata hiyo nafasi, hii ni fursa nyingine nzuri ya kuendelea kuandika historia mpya kwa umoja wetu,” alisema.
Naye kocha wa Nsingizini Hotspurs, Mandla Qhogi, alisema pamoja na kupoteza kwa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza, lakini bado wana nafasi ya kurekebisha makosa yaliyojitokeza kupata ushindi katika mtanange wa leo.
“Kabla ya mechi yetu ya kwanza hakuna aliyetarajia pia kama Simba ingeshinda ugenini kwa idadi kubwa ya mabao, hii ni mechi nyingine ngumu ila tutapambana kadri ya uwezo wetu,” alisema Mandla.




