Na WAANDISHI WETU
WAKUU wa Vyombo vya Habari na Wahariri Waandamizi nchini, wametoa maazimio yao kuhusu umuhimu wa kutunza amani kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu, huku wakiungana na viongozi wa dini na makundi mengine yaliyosisitiza kutunza amani.
Tamko hilo la maazimio lilisomwa kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa ITV na Redio One, Joyce Mhavile kwa niaba ya wakuu hao wa vyombo vya habari zaidi ya 20 na Wahariri Waandamizi.
“Sisi Wakuu wa Vyombo vya Habari na Wahariri Waandamizi tuliokutana wiki hii, tunaamini katika kushamiri kwa demokrasia ya vyama vingi.
“Ni dhahiri kuwa vyombo vyetu, vimetoa mchango mkubwa katika kuijenga na kuishamirisha demokrasia ya vyama vingi kwa miongo zaidi ya mitatu sasa,”alinukuu.
Akisoma maazimio mengine, Joyce alisema Watanzania kwa umoja wao, wakatae kuhudhuria karamu ya uchochezi wenye lengo la kuwashawishi kulewa ‘Uwendawazimu wa Kihalaiki’ unaoweza kulisambaratisha Taifa kama ilivyotokea katika mataifa mengine.
“Tanzania imekuwa kisiwa cha amani kwa sababu ya misingi iliyowekwa na waasisi wa taifa letu na utamaduni wa kukaa katika meza ya mazungumzo kumaliza tofauti zetu.
“Na kwa miaka mingi, Tanzania imekuwa ni makazi ya matumaini kwa wakimbizi wanaokimbia machafuko ya kisiasa na vita katika nchi zao.
“Zipo nchi nyingi zikiwemo jirani zetu wa Rwanda na Congo, Sierra Leone, Sudan, Somalia, Liberia, Ivory na nyinginezo ambazo zimebaki na makovu ya “Uwendawazimu wa Kihalaiki” ambayo hata pale amani iliporejea au itakaporejea, bado makovu hayo yataendelea kubaki kama sanamu ya kumbukumbu ya majuto,” alisoma Joyce.
Alieleza, katika siku za hivi karibuni, kumesikika kauli zinazochochea chuki na shari, jambo ambalo haliakisi kabisa utamaduni wa Watanzania.
“Kauli zinazohamasisha wananchi kufanya vurugu, kuchoma vituo vya mafuta, vituo vya polisi na mali nyinginezo, siyo tu ni makosa kisheria, bali ni kauli zisizoakisi Utanzania wetu, zinatakiwa kukemewa na kila Mtanzania,”alisema.
Joyce alieleza kuwa, kwa muda mrefu, vyombo vya habari vimeripoti matukio ya vurugu, uvunjifu wa amani, vita vya wao kwa wao na hata mauaji ya kimbari yaliyotokea katika mataifa ya Afrika, yaliyoathiriwa na siasa chafu na kuingiliwa na maadui wa nje.
Alifafanua kuwa, machafuko hayo, mateso na mauaji ya wananchi wasiokuwa na hatia katika nchi hizo, yalisababishwa na ubinafsi wa vikundi vya wanasiasa walioamua kutumia propaganda za kugawa watu, bila kujali maslahi mapana ya mataifa yao.
Alisisitiza kuwa, mara kwa mara, vyombo vya habari vimeendelea kuripoti na kuandika tahariri pale vyama vya siasa viliposuguana hasa nyakati za uchaguzi na kusababisha vurugu kama ilivyowahi kutokea Zanzibar mwaka 2001 baada ya Uchaguzi Mkuu.
Alieleza kuwa, demokrasia ya taifa bado ni change, inahitaji muda, kwani ni mchakato endelevu, unaotakiwa kujengwa kila siku kwa kuhakikisha kila hatua inalindwa na wadau wote.
Alisema ni vyema wanachi kukumbuka kuwa, Tanzania ilipata uhuru wake kwa jitihada za majadiliano, mazungumzo na hoja za wanasiasa, wakipingana bila kupigana, hivyo Watanzania wana wajibu wa kuendelea kujenga demokrasia kwa njia hizo za mazungumzo na siyo vinginevyo.
Awali akimkaribisha msomaji wa waazimio hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC), Ayoub Ryoba, alisisitiza vyombo vya habari kuendelea kuripoti maazimio hayo yenye msingi wa kudumisha amani nchini.
Alisema vyombo vya habari vina mchango mkubwa kwa jamii hususan kuhamasisha amani na utulivu katika jamii kuwepo maendeleo zaidi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Deodatus Balile, alisema maazimio hayo ni ya msingi katika kujenga amani na umoja wa kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu.




