NA MWANDISHI WETU
DODOMA
RAIS na Amiri Jeshi Mkuu, Dk. Samia Suluhu Hassan, ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida kuanzia leo, Novemba 3, 2025, kufuatia machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Ameonya kuwa waliohusika kuchochea uvunjifu wa amani watachukuliwa hatua kali za kisheria, akisisitiza kuwa vurugu huishia kupimana nguvu.
Akizungumza baada ya kuapishwa kuongoza kwa muhula wa pili katika Serikali ya Awamu ya Sita, Rais Dk. Samia amesema mchakato wa uchaguzi ni wa msimu mmoja tu ndani ya miaka mitano, hivyo maisha lazima yaendelee.
Amesisitiza kuwa jukumu la kujenga taifa ni la Watanzania wote, kwa kuimarisha umoja, upendo na mshikamano.
Rais Dk. Samia amesema matukio ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza katika baadhi ya maeneo nchini hayalingani na utamaduni wa Kitanzania, akibainisha kuwa baadhi ya vijana waliokamatwa wametoka nje ya nchi.
Amezielekeza Kamati za Ulinzi za Kitaifa, Mikoa na Wilaya kuhakikisha hali ya utulivu inarejea mara moja, huku akiwataka Watanzania kuchagua hekima, busara, upendo, uvumilivu na amani badala ya ghadhabu na chuki.
Aidha, amesisitiza kuwa ukuaji wa demokrasia haupimwi kwa matokeo ya uchaguzi pekee bali kwa jinsi taifa linavyoshughulikia masuala yake baada ya uchaguzi.
Ameishukuru jamii ya viongozi wa dini kwa kuhimiza amani na kupongeza viongozi wa mataifa jirani waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwake.
Katika halfa hiyo ya uapisho, viongozi kutoka mataifa mbalimbali walihudhuria wakiongozwa na Rais wa Burundi, Evaliste Ndayishimiye na Rais wa Zambia, Haikande Hichilema ambao walipata fursa ya kutoa salamu zao.
Katika salamu zao viongozi hao walimpongeza Rais Dk. Samia kwa ushindi wa kishindo huku wakitoa wito kwa Watanzania kuendeleza kudumisha amani, umoja na mshikamano.
Katika hatua nyingine, Rais Dk. Samia amempongeza Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuchaguliwa kuendelea kuongoza Zanzibar, na kuvipongeza vyama 17 vilivyosimamisha wagombea wa urais kwa kuonesha ukomavu wa kisiasa na kuendesha kampeni za hoja.




