Na MWANDISHI WETU
CHAMA cha Mawakili wa Serikali (GAT) kimempongeza, Hamza Johari kwa kuteuliwa tena kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kikiuelezea uteuzi huo kuwa ni kielelezo cha ubobezi na uadilifu wake katika taaluma ya sheria.
Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho, uteuzi huo pia unaendana na matakwa ya Ibara ya 59 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayotaka Mwanasheria Mkuu awe na sifa za uwakili kwa angalau miaka 15.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Johari ana uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika utumishi wa umma, hususan katika masuala ya mikataba, sheria za anga, bahari na udhibiti.
Ana Shahada ya Sheria (LL.B) na Shahada ya Uzamili (LL.M) katika Sheria za Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Kiev, Ukraine, pamoja na cheti cha Uongozi na Usimamizi kutoka Chuo cha Utawala cha India.
Johari amewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania kwa kipindi cha miaka tisa, na pia amehudumu kama Mwenyekiti wa CANSO Afrika, CASSOA na kamati mbalimbali za kisheria za kikanda na kimataifa.
Aidha, amewahi kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Mzumbe na Chuo Kikuu cha Alexandria nchini Misri.
Mbali na hayo, Johari amekuwa Mlezi wa Chama cha Mawakili wa Serikali, Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, na Mwenyekiti wa timu za majadiliano ya Serikali katika mikataba mikubwa ya kimataifa ikiwemo ya DP World (U.A.E) na Bandari ya Adani (India).
Pia ameshiriki katika timu za kitaifa za kutatua migogoro ya mipaka na majadiliano ya miradi ya kimkakati ya kitaifa.
Johari ni Mmakonde, mzaliwa wa Wilaya ya Mtwara Vijijini, Tarafa ya Ziwani, Kata ya Nalingu.




