Na ATHNATH MKIRAMWENI
BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limesema uamuzi wa kutoa matokeo ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi mwaka 2025 kwa kutumia namba badala ya majina ya wanafunzi, umetokana na sababu za kulinda taarifa binafsi za wanafunzi hao.
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed, alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa kanuni za kulinda faragha ya mtu binafsi katika enzi ya maendeleo ya teknolojia na utandawazi.
“Sasa hivi tumetoa matokeo kwa namba za mtihani badala ya majina ili kulinda taarifa binafsi za wanafunzi. Tupo katika zama za utandawazi, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha taarifa za mtu binafsi zinabaki salama tangu utotoni,” alisema Profesa Mohamed.
Aidha, aliwasihi wazazi na walezi waliopoteza au kusahau namba za mitihani ya watoto wao, kufika kwa wakuu wa shule husika ili kupata namba hizo na kuweza kuona matokeo.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, jumla ya watahiniwa 937,581 sawa na asilimia 81.80 ya watahiniwa 1,146,164 waliofanya mtihani huo wamefaulu kwa kupata madaraja ya A, B na C.
Kiwango hicho kimeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2024 ambapo watahiniwa waliofaulu walikuwa asilimia 80.87.
“Hivyo, ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 0.93. Kati ya watahiniwa 937,581 waliofaulu, Wavulana ni 429,104 sawa na asilimia 82.51 na Wasichana ni 508,477 sawa na asilimia 81.21.
“Mwaka 2024 wasichana waliofaulu walikuwa asilimia 80.05 na wavulana waliofaulu walikuwa asilimia 81.85. Hivyo, ufaulu wa wasichana umeongezeka kwa asilimia 1.16 na ufaulu wa wavulana umeongezeka kwa asilimia 0.66,”amesema.
Kuhusu ubora wa ufaulu, watahiniwa 422,923 sawa na asilimia 36.90 wamepata madaraja ya A na B ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.07 ikilinganishwa na mwaka 2024.
Katibu huyo alisema ubora wa ufaulu kwa wasichana umeongezeka kwa asilimia 0.70, ambapo mwaka 2025 umefikia asilimia 33.71 ikilinganishwa na asilimia 33.01 mwaka 2024.
Alisema ongezeko hilo limechangiwa na kuimarika kwa ufaulu katika madaraja ya juu, ambapo daraja la A limeongezeka kwa asilimia 0.39 na daraja la B kwa asilimia 0.31 ikilinganishwa na mwaka 2024.
Kwa upande wa wavulana, ubora wa ufaulu nao umeongezeka kwa asilimia 1.52 hadi asilimia 40.73 ikilinganishwa na asilimia 39.21 mwaka 2024.
Ongezeko la ubora wa ufaulu limechangiwa na kuimarika kwa ufaulu katika daraja la A kwa asilimia 0.78 na daraja la B kwa asilimia 0.74 ikilinganishwa na mwaka 2024.
Profesa Mohamed alisema kati ya shule 19,436 zenye matokeo hayo shule nyingi ambazo ni 12,224 sawa na asilimia 62.89 zimepata wastani wa Daraja la C ikilinganishwa na madaraja mengine ya ufaulu.
Alisema shule zilizopata wastani wa madaraja ya A na B zimeongezeka kwa asilimia 3.78 kutoka idadi ya shule 4,645 sawa na asilimia 24.54 mwaka 2024 hadi
kufikia idadi ya shule 5,503 sawa na asilimia 28.32 mwaka 2025.
Adha, shule zilizopata wastani wa daraja A-C ni 17,727 sawa na asilimia 91.21.




