Na LILIAN JOEL,
ARUSHA
WATALII kutoka mataifa mbalimbali duniani wanaotembelea Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) wameendelea kufanya shughuli zao za utalii kwa amani, usalama na utulivu, huku wakifurahia vivutio lukuki vilivyopo katika hifadhi hiyo maarufu duniani.
Akizungumza katika lango kuu la Laoduare, Ofisa Uhifadhi Mkuu wa Idara ya Huduma za Utalii na Masoko wa NCAA, Peter Makutian, amesema katika kipindi chote cha uchaguzi mkuu wa Tanzania hadi kufikia Novemba 5, 2025, jumla ya wageni takribani 1,200 kutoka mataifa mbalimbali wametembelea hifadhi hiyo na kushiriki shughuli za utalii.
“Hifadhi ya Ngorongoro tunaendelea kupokea watalii wa ndani na wa kimataifa. Kwa sasa tuko katika msimu wa wastani, lakini tunaamini kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka idadi ya watalii itaongezeka zaidi,” amesema Makutian.
Kwa upande wake, Isabella Jerónimol, mtalii kutoka Colombia aliyefika nchini akiwa na familia ya watu 26, alisema walichagua kutembelea Tanzania kwa kuvutiwa na hali ya amani, ukarimu wa wananchi na utajiri wa vivutio vya asili.
“Safari hii tuliipanga kwa muda mrefu. Tumefurahi kufika Tanzania, nchi yenye vivutio vingi vya kipekee. Tulichagua Hifadhi ya Ngorongoro kwa sababu ni sehemu yenye historia kubwa na mandhari ya kuvutia. Tulikaribishwa vizuri na kupewa maelezo kuhusu wanyama na urithi wa hifadhi hii,” amesema Jerónimol.




