NA MWANDISHI WETU,
DODOMA
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imechukua hatua madhubuti za kurejesha utengamano wa kitaifa na kuhakikisha wananchi wanaishi chini ya misingi ya utawala wa sheria.
Dk. Nchimbi ametoa kauli hiyo akiwa mkoani Dodoma wakati akimwakilisha Rais Dk. Samia katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika kwa njia ya mtandao.
Amesema dhamira ya Rais Dk. Samia ni kuhakikisha mchakato wa mazungumzo ya maridhiano unafanikiwa ili kujenga taifa lenye amani, umoja na mshikamano na kuendelea kuwa mfano wa utulivu barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Aidha, Makamu wa Rais amesisitiza kuwa Tanzania inaendelea kuwa nchi salama na tulivu na ipo tayari kupokea wageni kutoka mataifa mbalimbali kwa manufaa ya nchi na wananchi wake.
Aidha, Makamu wa Rais, amewashukuru viongozi wa SADC walioshiriki uapisho wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wote waliotoa pongezi za dhati.
Amesema jitihada zote zitatumika kuhakikisha Tanzania inapata maendeleo na amani kuendelezwa.
Mkutano huo umempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa ushindi aliyoupata na uchaguzi wenye mafanikio.
Mkutano huo ulilenga kujadili kujiondoa kwa nchi ya Madagascar kama nchi Mwenyekiti wa SADC, ambapo nchi ya Afrika Kusini imependekezwa kuwa Mwenyekiti kwa kipindi cha mpito mpaka kufikia mwezi Agosti 2026.
Mkutano huo umekubaliana kuendelea kutumia kauli mbiu ya Mkutano wa 45 wa SADC uliyofanyika nchini Madagascar ambayo ni “Kuimarisha Viwanda, Mapinduzi ya Kilimo, Mabadiliko ya Nishati kwa SADC yenye Uhimilivu”
Mkutano huo umeongozwa na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa na kuhudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na Wawakilishi kutoka Nchi 15 za SADC.





