NA WAANDISHI WETU, DODOMA
LEO ndiyo siku ambayo swali la nani atakuwa waziri mkuu mpya litapatiwa majibu, ambapo jina la kiongozi huyo anayerithi mikoba ya Waziri Mkuu mstaafu Kassim Majaliwa, litawekwa hadharani.
Kwa mujibu wa Spika wa Bunge, Mussa Zungu akiahirisha kikao cha pili cha mkutano wa kwanza wa Bunge la 13, bungeni jijini hapa jana, miongoni mwa shughuli zilizopangwa leo ni wabunge kuthibitisha uteuzi wa Waziri Mkuu.
Mbali na hatua hiyo, kitendawili cha nani atakayerithi mikoba ya naibu spika nacho kinatarajiwa kuteguliwa leo kwa kufanyika uchaguzi huo kabla ya kula kiapo.
Katika nafasi hiyo, mpaka sasa, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimempendekeza Mbunge wa Babati Vijijini, Daniel Sillo, kuwania kiti hicho ambacho awali kilikuwa kikishikiliwa na Zungu.
Kikao cha Tatu cha Mkutano wa Kwanza wa Bunge, kazi zitakazofanyika ni kuthibitisha uteuzi wa Waziri Mkuu, uchaguzi na kiapo cha Naibu Spika.
“Wabunge wote mnaombwa kuwepo katika ukumbi wa Bunge kuanzia saa tatu kasoro dakika 10 asubuhi,” alisisitiza Zungu huku wabunge wakigonga meza kuashiria kuunga mkono tangazo hilo.
MATARAJIO WAZIRI MKUU AJAYE
Wakielezea matarajio yao kuhusu Waziri Mkuu ajaye, Mbunge wa Mbeya Mjini (CCM) Patrick Mwalunenge, amesema wanatarajia Waziri Mkuu ambaye atawaunganisha Watanzania kuwajibika na kumsaidia Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Amesema Waziri Mkuu ndiye kiungo muhimu kwa serikali, hivyo lazima apatikane ambaye ni msikivu, mzalendo na mwenye kujali utu wa Mtanzania.
“Tunatarajia kumpata Waziri Mkuu ambaye ataenda kuwaunganisha Watanzania, pia kumsaidia Rais Dk. Samia katika kuhakikisha Watanzania wanapata maendeleo,”alisema.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mufindi Kaskazini (CCM) Exaud Kigahe, alisema wanatarajia kumpata Waziri Mkuu ambaye atamsaidia Rais Dk. Samia kuendeleza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Vilevile, amesema ni muhimu Waziri Mkuu ajae akazingatia na kuweka mkazo katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
“Tuna miradi mikubwa ya maendeleo ambayo inatekelezwa nchini, tunategemea Waziri Mkuu ajaye atamsaidia Rais kuhakikisha inatekelezwa kwa wakati. Hakuna asiyejua kuwa katika miaka minne iliyopita Rais Dk. Samia amefanya kazi nzuri katika sekta zote,” amesisitiza.
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, alisema wanatamani kupata Waziri Mkuu ambaye anaguswa zaidi mambo ya wananchi.
“Tunazijua changamoto zilizopo katika nchi yetu kwa sasa na tunajua nafasi ya Waziri Mkuu ni nafasi nyeti ni mtu anayekwenda kumsaidia moja kwa moja Rais kwenye shughuli za kila siku.
Amesisitiza: “Asilimia 70 ya wananchi ni vijana, Waziri Mkuu anapaswa kujua matatizo ya vijana na awe tayari kushirikiana na viongozi na wananchi kutatua changamoto za vijana hasa suala nzima la ajira.
“Kila mtu anatamani kuona Taifa moja lenye upendo mshikamano na lenye mwelekeo mmoja, tunatamani ajifunze kutoka kwa watangulizi wake,” amesema Nasari.
Kwa upande wake, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela alisema anatamani Waziri Mkuu ajae awe mchapa kazi amsaidie Rais Dk. Samia.
Kilango alimshauri Waziri Mkuu anayekuja kuiga mfano wa Majaliwa ambaye katika kipindi chake alifanya kazi kubwa.
Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu, (ACT) alisema anatamani Waziri Mkuu ajae awe mwajibikaji, mbunifu atakayeweza kuhakikisha serikali inatatua changamoto za wananchi.
IMANI KWA SPIKA
Katika hatua nyingine, viongozi mbalimbali wameendelea kueleza imani yao kwa Spika wa Bunge, Zungu ambapo Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, alisema ana imani kubwa kwamba Zungu ataendesha taasisi ya Bunge vizuri.
“Mimi sina tatizo kabisa na Zungu kwa sababu ameshakuwa Naibu Spika kwa muda mrefu akiwa na Spika Mstaafu Dk. Tulia Ackson nina hakika ana ujuzi na uzoefu wa kutosha.
“Sina sababu ya kuwa na hofu naye kwa kuwa namjua na ndiyo maana wabunge wamemchagua kwa sababu wangekuwa na wasiwasi naye wasingemchagua,”amesema Sumaye.
Mbunge wa Kakonko, Allan Mvano, amesema imani yake ni kwamba Zungu anakwenda kuongoza Bunge kwa mijadala ambayo itakuwa ya haki, bila kubagua wala upendeleo kuhakikisha sheria na kanuni zote zinazingatiwa.
“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpata Zungu kwa sababu ya uzoefu wake katika kuliongoza Bunge, ni jambo la heri kuona kwamba amekuja na maono ya kutaka kuisaidia serikali katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025/2050.
“Maana yake ni kwamba atakuwa mstari wa mbele kuhakikisha mawazo yanayotolewa katika Bunge yanaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo.
Amempongeza Zungu kwa kitendo cha kuona Bunge linakuwa na mchango katika Dira ya Maendeleo, huku akieleza kuwa hicho ni kiashiria cha kwamba anatamani kuona taifa linaendelea zaidi.
AHADI KWA WANANCHI
Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara, amesema atachapa kazi kulipa deni na imani ambayo wananchi wamempa kwa kumwaamini na kumchagua katika kipindi kingine kuwaletea maendeleo.
Kuhusu hoja kwamba Bunge halitakuwa na meno kwa sababu halina upinzani, amesema siyo kweli kwa sababu wabunge wengi wana uwezo wa hali ya juu katika kuishauri serikali kupitia masuala mbalimbali yatakayoibuliwa kwa maslahi ya wananchi.
“Kwa kuwa vijana ni wengi humu ndani na ni wasomi, tunatarajia Bunge litakuwa la moto sana kuliko watu wanavyofikiri huko nje, kutakuwa na ushindani mkubwa kujionyesha kwamba nimekuja bungeni sikuja kwa bahati mbaya natakiwa kufanya kazi,” amesema Waitara.
Mbunge wa Busokelo, Lutengano Mwalwiba, amewataka wananchi wa jimbo hilo watarajie maendeleo huku akiwasihi kumpa ushirikiano, hususan katika maeneo yenye changamoto mbalimbali.
Mbunge wa Kilolo, Ritha Kabati, amesema amekuwa mbunge kwa vipindi vitatu, hivyo wananchi wanamwamini kwa sababu amefanya kazi kubwa.
“Sipo kujifunza, naenda kufanya kazi moja kwa moja, tayari nilipokuwa naomba kura nilichukua changamoto kwa hiyo nakwenda kazini najua wapi pa kuzitatua, wawe na imani na mimi maana sitawaangusha,” ameeleza.
Ritha amesema kuwa kipaumbele chake cha kwanza atakachoanza nacho kwa sasa ni barabara ambazo zimekuwa hazipitiki hususani kipindi cha mvua hali inayoleta kero kwa wananchi.
“Kilolo ina uzalishaji mkubwa lakini ikifika wakati wa mvua barabara hazipitiki mazao hayafiki sokoni na wananchi hawapati pembejeo,”amesema Ritha.




